THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S OFFICE,
STATE HOUSE,
Tanzania.
|
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
JK: Acheni woga na udhaifu wa kusimamia sheria
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewataka viongozi nchini kuacha woga na ulegevu katika kusimamia sheria
za kulinda mazingira na vyanzo vya maji ambavyo ni namna ya uhakika ya
kuwawezesha wananchi kuendelea kupata maji ya uhakika, safi na salama.
Aidha,
Rais Kikwete amewataka watu wanaokopa fedha katika vyama vya ushirika
vya akiba na mikopo kuhakikisha kuwa wanarudisha fedha hizo kwa wakati
kwa sababu kushindwa kurudisha mikopo hiyo kwa wakati kunawarudisha
nyuma wengine ambao pia wanahitaji mikopo hiyo.
Rais Kikwete amesema hayo jana, Ijumaa, Agosti 22, 2014 kwenye siku yake ya tatu ya ziara yake ya
kikazi
katika Mkoa wa Morogoro ambako ametembelea, amekagua na kuzindua miradi
ya maendeleo ya wananchi katika Wilaya ya Morogoro na Manispaa ya
Morogoro.
Akizindua
mradi mkubwa wa maji ambao umegharimiwa na Serikali ya Marekani kupitia
Shirika la Changamoto za Milenia Tanzania (MCA-Tanzania) katika
Manispaa ya Morogoro, Rais Kikwete aliwaambia viongozi wa Manispaa ya
Morogoro na wengine nchini:
“Acheni
ulegevu, acheni woga, kazi yenu haiwezi kutoa simulizi kwa sababu
mamlaka yote ya kuzuia watu kulima na kujenga katika maeneo ya vyanzo
vya maji mnayo. Yatumieni.”
Rais
Kikwete ambaye pia alirudia ujumbe huo kwa viongozi kwenye mkutano wa
hadhara kwenye Uwanja wa Jamhuri aliwaambia viongozi hao:
“Shughuli
za binadamu za kilimo na makazi haziwezi kuruhusiwa katika vyanzo vya
maji. Acheni tabia hii ya kushindwa kusimamia sheria na kutumia mamlaka
ambayo mnayo. Mkiendekeza tabia hii iko siku wananchi wa Morogoro mjini
watakosa maji kabisa.”
Rais
Kikwete alikuwa anajibu malalamiko ya awali ya uongozi wa Manispaa ya
Morogoro ambao ulikuwa umemwomba Rais alitangaze eneo la Milima ya
Uluguru na Bwawa la Mindu kuwa hifadhi za taifa kutokana na kuwa vyanzo
vikuu vya maji kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro.
“Hamna
mtu wa kumnung’unikia. Kazi yake haiwezi kuwa kumsubiri Rais ili
kumsimulia kuhusu haya. Najua mkichukua hatua wako wanasiasa ambao
watajitia wanawatetea wananchi, lakini kwenye hili la kulinda vyanzo vya
maji hakuna la msalie Mtume.Kama sehemu nyingine kama kule Kinole
(Wilaya ya Morogoro) wameweza, nini kinawashinda nyie kuwaondoa watu
kwenye vyanzo vya maji?”
Mradi
huo wa Ukarabati wa Miundombinu ya Maji Safi katika Manispaa ya
Morogoro ulioanza kujengwa mapema mwaka 2011 kwa gharama ya sh. bilioni
56 kutoka Serikali ya Marekani na kupitia MCA-Tanzania, utaongeza
kiwango cha kupatikana kwa maji safi na salama kwa wakazi wa Manispaa
kutoka mita za ujazo 29,000 hadi 33,000 kwa siku na kunufaisha maelfu ya
wananchi.
Hata
kama ni kweli kuwa mradi huo hautamaliza mahitaji yote ya maji kwa
Manispaa ya Morogoro, ambayo ni mita za ujazo 39,400 bado zitawezesha
upatikanaji wa maji kwa kiasi cha asilimia 85 kwa wakazi wa Manispaa
hiyo na hivyo kuboresha maisha ya wakazi hao.
Rais
Kikwete amewaomba wananchi wa Manispaa ya Morogoro na viongozi wao
kutunza miundombinu hiyo na kuhakikisha kuwa maji yanaendelea kupatikana
kwa wakazi wa Manispaa.“Tukifanya hivyo, hata hao waliotusaidia wataona kuwa tumewaheshimu.”
Mapema
jana hiyo hiyo, Rais Kikwete alitembelea eneo la Kinole na kuzindua
Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Kinole – SACCOS- ambacho
kilindikishwa rasmi mwaka 2001 na mpaka sasa kimetoa mipoko ya kiasi cha
Sh. bilioni nne kwa wanachama wake wapatao 1,700.
Rais
Kikwete amekuwa kiongozi mkuu wa pili wa Tanzania kutembelea Kinole
tokea Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye alitembelea eneo hilo mwaka
1961 na wananchi walionyesha furaha yao kwa ujio huo kwa kumsimika Rais
Kikwete kuwa Chidukila, yaani chifu msaidizi wa eneo hilo.
Rais
Kikwete aliwapongeza wananchi wa Kinole kwa kuendesha SACCOS yenye
mafanikio makubwa na manufaa kwa wakulima wa eneo hilo ambao miongoni
mwa mambo mengine huingiza sokoni kiasi cha fuso 10 za ndizi kila siku.
“Huu
ni ukombozi kwenu. Haya ndio maisha bora kwetu kwa sababu hii mikopo
ambayo mnapata msingeweza kuipata kwa mabenki. Benki hiyo rafiki wa
masikini. Benki haikopeshi masikini, asiyekuwa nacho hapati kutoka
benki.”
Rais
Kikwete alihimiza kurudishwa kwa wakati kwa mikopo inatolewa na chama
hicho akisisitiza kuwa wale ambao wanachelewesha kurudisha
mikopo“wanawarudisha nyumba wenzao ambao nao wanataka mikopo.”
Rais
Kikwete amekatisha ziara hiyo ya siku saba Mkoani Morogoro kwenda
Arusha, Tanga na Dar Es Salaam kwa siku moja kwa shughuli nyingine za
kitaifa. Ziara hiyo itaendeleo tena kesho, Jumapili, Agosti 24, 2014.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
23 Agosti,2014
No comments:
Post a Comment