Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday 18 August 2014

MWALIMU NYERERE ALIPOMWAGA MACHOZI DODOMA KUPINGA HOJA YA TANGANYIKA

 
KIKAO CHA PILI DODOMA 14:10:I993

Nilipokwisha kuhakikishiwa kuwa sasa sera ya Serikali Tatu ndiyo sera rasmi ya Bunge la Muungano na Serikali ya Muungano, nilijaribu kupata maelezo kutoka kwa viongozi wetu; lakini sikufanikiwa. Waziri mkuu nilipomuuliza kama kweli wamebadili sera, alicheka tu!
Nilikuwa na safari ya kutembelea nchi za Asia kwa ajili ya shughuli zinazotokana na uenyekiti wangu wa Tume Nchi za kusini. Niliporudi kutoka safari nilijaribu tena kuonana na viongozi wetu ili nipate maelezo lakini sikufanikiwa kumpata kiongozi yeyote mhusika.
Nilipopata habari kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana Dodoma, nilihisi kuwa bila shaka viongozi wetu wataeleza kwa nini wameacha msimamo wa Chama na maagizo ya Kamati Kuu ya kupinga hoja ya Utanganyika, wakaamua kukubali hoja hiyo.
Basi nikaomba angalau nipatiwe nafasi nihudhurie kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya Taifa, ili nami nisikie maelezo watakayotoa. Baada ya maajabu ambayo haina maana kuyaeleza, nilikubaliwa nikaenda Dodoma.

KIKAO CHA FARAGHA

Safari hii tulikuwa na vikao viwili. Kwanza kikao cha faragha wakiwapo viongozi wakuu wote wa Chama na Serikali, na wengine wa nyongeza. Kilikuwa kikao kirefu na kigumu.
Sina kawaida ya kulizwa na mambo ya siasa, lakini katika kikao hiki nilishindwa kujizuia kulia. Sikupata maelezo ya maana ya kuwafanya watu wafanye walivyofanya. Nilipouliza kwa nini hawakupinga hoja ya Serikali tatu kama tulivyokuwa tumekubaliana, majibu ya viongozi wetu Wakuu yalikuwa ni ya ajabu kabisa. Ati wabunge wenye hoja baada ya kuonana na mimi Msasani walikwenda Bungeni wakiwa wakali kama mbogo! Tena walikuwa wakiwatukana wenzao (yaani wabunge wa Zanzibar), kwa kuwataja majina.
Hizi ni sababu za ajabu sana za kuwafanya viongozi watu wazima watekeleze msimamo mzima wa Chama chao na makubaliano ya watu makini kuutetea msimamo huo, na waamue kuikumbatia hoja ya mbogo wakali! Huu ni uongozi wa ajabu kabisa!
Nilipowabana zaidi niliahidiwa kuwa maelezo mazuri yatatolewa kesho yake na waziri wa Sheria na mambo ya katiba katika kikao cha Halmashauri Kuu ya taifa.

KIKAO CHA HALMASHAURI KUU:
Hakika siku ya pili yake waligawiwa ‘TAARIFA YA SERIKALI JUU YA AZIMIO LA BUNGE KUHUSU HAJA YA KUUNDA SERIKALI YA TANGANYIKA NDANI YA MUUNDO WA MUUNGANO’. Taarifa yenyewe ni ndefu ina maelezo mengine ya mapambo tu, au ya kiini macho. Lakini vipengele vinavyohusika na suala lenyewe vilikuwa vichache na nimevinukuu kwa ukamilifu.
9. “Tarehe 30 Julai, 1993 wakati wa mkutano wa bunge la bajeti ukiendelea, zaidi ya wabunge 50 kwa pamoja walitoa taarifa ya kusudio la kuwasilisha hoja Bungeni ambayo inadai, miongoni mwa mambo mengine;
Kwa kuwa kuendelea mfumo huu wa Muungano usiowaridhisha wananchi wengi wa upande mmoja ni kuhatarisha kuendelea na kudumu kwa Muungano na pia kuathiri uelewano kati ya watu pande zote mbili; na
Kwa kuwa uwezekano wa kuunda serikali moja ya Jamhuri ya Muungano kwa nchi nzima kwa mambo yote haujajionyesha;
Hivyo basi wabunge hawa wanaliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano katika mkutano wake wa kumi na mbili unaofanyika Dar es salaam liazimie kwamba;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilete Muswada Bungeni, kabla ya Februari 1994, kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ili kuwezesha uundaji wa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muungano.
Tarehe 12 Agosti, 1993 hotuba ya kuwasilisha Makadirio ya Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba ilisomwa Bungeni. Katika hotuba hiyo Serikali ilieleza kusudio la kuandaa Waraka wa Serikali (White Paper) kutafuta maoni ya wananchi kuhusu muundo wa Muungano. Tarehe 20 Agosti, 1993 wabunge wahusika waliwasilisha taarifa nyingine inayobadilisha ile hoja ya awali iliyosambazwa kwa wabunge wote. Hoja mpya ilikuwa inalitaka Bunge zima liazimie kwamba:
Serikali ya Jamhru ya Muungano iandae kura ya maoni ambayo itafanyika kabla ya 31 Desemba, 1994 ili kupata maoni ya wananchi wa Tanzania juu ya kuundwa kwa “Serikali ya Tanganyika” ndani ya Muundo wa Muungano utakaozingatia mabadiliko hayo. Kutokana na taarifa hizi, Baraza la Mawaziri lilifanya kikao cha dharura ili kutafakari taarifa hizi na athari zake kama zingewasilishwa Bungeni na kupigia kura.
Kwanza kabisa, inaonekana kwamba hoja ya awali ingekuwa vigumu kutekelezeka kutokana na muda mfupi uliowekwa kufikia Februari, 1994, na pia haikutoa fursa kupata maelekezo ya Chama wala serikali zetu mbili kushauriana. Kwa kutambua kwamba Bunge linafanya maamuzi yake kwa njia ya kura baada ya mijadala ya wazi, Serikali iliona kwamba hoja yoote kati ya hizi ingewasilishwa Bungeni, ingeweza kuligawa Bunge, kukigawa chama chetu na kuwagawa wananchi katika suala zito kama hili la Muundo wa Muungano.
Kuhusu suala la kura ya maoni, serikali iliona kwamba utekelezaji wake ni sawa na kufanya uchaguzi mkuu, jambo ambalo ni la gharama kubwa. Aidha, kwa kuzingatia kwamba kura ya maoni kupigiwa suala linalohitaji jibu la ‘NDIYO’ au ‘HAPANA’ , ni vigumu kupata swali lililo wazi kwa wananchi ambao hawana uzoefu wa utaratibu huo wa kura ya maoni.
Pamoja na hayo, kwa kuzingatia kwamba uamuzi wa kura ya maoni ni lazima ukubalike katika sehemu zote mbili za Muungano, itakuwa vigumu kupata uwiano wa kura utakaokubalika pande zote mbili kuwa ndio kiwango cha uamuzi.
10. Pamoja na juhudi za Serikali rote mbili kupitia Kamati ya Pamoja, Serikali zetu pia zilifikia makubaliano na kufanya maamuzi kuhusu baadhi ya matatizo mazito yaliyokuwapo katika Muungano wetu. Maamuzi hayo ni:
(a) Serikali ya Mapinduzi Zanzi­bar kukubali Zanzibar kujitoa katika uanacharna wa 'OIC';
(b) Utaratibu wa kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano uwe ni kwa njia ya kupigiwa kura kwa pamoja na mgombea urais (running mate).
11. Kwa msingi huu na kwa kuzingatia maamuzi ya awali ya Serikali ya kutaka kupata maelekezo ya chama na maoni ya wananchi kuhusu muundo utakaotatua matatizo ya Muungano, Serikali iliona kuna umuhimu wa kushauriana na wabunge waliohusika ili kupata muafaka wa maudhui ya hoja yenyewe. Muafaka huo ulifikiwa katikaKikaochaKamati ya Wabunge wakikaa kama Kamati ya Chama tarehe 2218/93. Kutokna na muafaka huo, hoja ya wabunge ilirekebishwa na azimio la Bunge kupitisha kwa kauli moja kwamba:
"Selikali iandae na kusimamia utaratibu utakaoshirikisha wananchi na taasisi mbali mbali ili kufikisha Bungeni kabla ya Aprili, 1995, mapendekezo ya muundo muafaka wa Muungano ambao utazingatia haja ya kuwapo Selikali ya Tangan­yika ndani ya Muungano pamoja na mambo mengine.
12. Azimio hili linaagiza mambo mawili yaliyo wazi:
(a) kupatikana kwa muundo muafaka wa Muungano ambao unazingatia haja ya kuwapo Serikali ya Tanganyika.
(b) Kuwapo na utaratibu wa kushirikisha wananchi na taasisi mbalimbali utakaosimamiwa na Serikali kabla ya mapendekezo ya mwisho kufikishwa Bungeni.
13. Kwa kuwa suala la muundo wa nchi ni zito na ni la kikatiba, ushirikishwaji wa wananchi ni jambo lisiloweza kuepukwa. Aidha kwa uzoefu wetu na hali halisi ya nchi yetu, ni lazima utaratibu wo wote utakaokubalika, uwezeshe Serikali ya Jamhuri ya Muungano kushauriana na Chama na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.


REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA

No comments:

Post a Comment