Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 29 August 2014

NAWAKUMBUSHA TU: NYERERE ALITAKA MWINYI AMFUKUZE KAZI MALECELA


IV. MSIMAMO WA RAIS

Wakati wa mgogoro wa Zanzibar kuingia katika OIC, na utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais, yawezekana kuwa Rais mwenyewe alikuwa akipendelea msimamo wa "Wazanzibari". Na hasa kuhusu suala la OIC, maelezo yake kwa Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye alipowahutubia wananchi siku ya Mei Mosi, Mtwara, yalifanya watu wengi waamini hivyo. Na washauri wake wa karibu walitaka tuelewe hivyo: kwamba ugumu wa suala la OIC ulikuwa unaletwa na Rais mwenyewe, maana alikuwa akiliona suala hilo kwa jicho la Uzanzibari, badala ya kuliona kama Rais wa Tanzania na mlinzi mkuu wa katiba yake.
Lakini pamoja na kwamba hivyo ndivyo washauri wake wakuu walivyotaka tuelewe, na yawezekana kuwa walikuwa wakisema kweli, kila tulipojaribu kuelewa kwa nini wao hawajiuzulu, hatukupata jibu lolote, achilia mbali jibu la maana. Waziri akihitilafiana na Rais wake katika jambo la msingi, kwa kawaida anatazamiwa kujiuzulu na kueleza kwa nini hawezi kuendelea kuwa Serikalini. Hawa hawakufanya hivyo. Lakini walitaka tuelewe kuwa mwenye hatia ni Rais.
Katika suala la Utanganyika, inaelekea kuwa Rais si miongoni mwa mrubani, yeye anakokotwa tu, moyo wake haumo. Lakini washauri wake wamemfikisha pagumu. Kutokana na msimamo wake wa awali kuhusu OIC, inaelekea kuwa Rais anaambiwa, ama ni washauri wake au na dhamiri yake mwenyewe: "Madhali suala la OIC ulilifumbia macho, huna budi ulifumbie macho na suala la Utanganyika pia. Usipofanya hivyo 'Watanganyika' hawatakuelewa."
Kwa hiyo washauri wake walipomshauri akubali hoja ya kufufua Tanganyika na kuipa Serikali yake, badala ya kukataa na kumfukuza Waziri Mkuu kwa ukigeugeu wake, Rais wetu alikubali! Alifanya hivyo akijua athari za kufufua Utanganyika, na baada ya yeye mwenyewe kusimama mbele ya wabunge siku chache tu zilizopita, na kupinga hoja ya Serikali Tatu. Na alifanya hivyo baada ya kukiri na kusahihisha kosa la Zanzibar, hatua ambayo nilitazamia kuwa itampa nguvu ya kupinga hoja ya Utanganyika.
Hatuwezi kuwa wakweli tukisema kuwa Rais hana hatia, Rais wa Tanzania si sawa na Malkia wa Uingereza. Huyo ni Mkuu wa Nchi kikatiba ambaye hana madaraka ya kuongoza nchi yake. Kwa mujibu wa Katiba na mazoea ya nchi yao, hana budi akubali ushauri wa Waziri Mkuu wake, Hata kama yeye mwenyewe binafsi hakubaliani na ushauri huo. Rais wa Tanzania sivyo alivyo. Yeye ni Mkuu wa nchi Mtendaji. Kikatiba halazimiki kukubali na kutekeleza agizo la Rais ambalo hakubaliani nalo, hasa kama tofauti yenyewe ni kwa jambo la msingi, kama vile jambo la maadili na dhamiri, au sheria, au Katiba ya Nchi.
Waziri akiagizwa na Rais kufanya jambo la namna hiyo ana haki na wajibu wa kukataa na kujiuzulu. Rais hawezi kuagizwa na Waziri ye yote, yeye hushauriwa tu na Mawaziri wake. Akikubali ushauri mbaya hawezi kujitetea kwa kumtupia lawama Waziri aliyemshauri, maana uamuzi wa mwisho ni wake. Alikuwa na hiari kukubali au kukataa ushauri huo. Na ingawa Waziri hawezi kumfukuza Rais wake anayehitilafiana naye katika jambo kubwa, Rais anaweza, na mara nyingi anawajibika kumfukuza Waziri wake anayepingana naye katika suala kubwa na la msingi. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba Rais hawezi kukubaIi ushauri mbaya, halafu aepuke lawama, na amsukumie lawana Waziri aliyemshauri vibaya. Kanuni hii ni ya wazi, na ni vizuri ikaeleweka hivyo.
Lakini pamoja na hayo, katika suala hili ni kosa kutanguliza na kusisitiza zaidi uwajibikaji wa Rais. Kuwajibika kuna ngazi yake. Hatuwezi kusema ati kwa sababu Mkuu wa Nchi yetu ni Rais Mtendaji, basi atawajibika kwa kila kosa la Serikali yake na Mawaziri wake, hata pale, ambapo mkosaji halisi na wa wazi wazi ni Waziri. Rais hawezi kuwajibika kwa makosa ya Uongozi wa Serikali Bungeni, kama kwamba yeye naye ni Mbunge.
Viongozi wa chama na Serikali waliomo Bungeni, hasa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu, ndio wanaostahili kuwajibika moja kwa moja. Kwa vyo vyote vile hatuwezi kujenga utaratibu ambapo Waziri akikosa Rais ndiye anayewajibika. Mara mbili sasa Rais amelazimika kukiri hadharani makosa ya Serikali yake; na Mawaziri wahusika hawana wasi wasi. Kwanza, Rais ndiye aliyekiri kosa la Zanzibar kuingia katika OIC, na pili, ndiye aliyelazimika kukiri kule Dodoma kwamba utaratibu wa kushughulikia hoja ya Utanganyika ulikosewa. Lakini Mawaziri wake, mara zote mbili, walitulia tu na kumwacha Rais ndiye akiri kosa na ­kubeba lawama.
Katiba ya Nchi yetu, na utaratibu tunaojaribu kujenga, vinataka kuwa katika hali kama hiyo Mawaziri ndio wawajibike, na hivyo kumlinda Rais, si Rais awajibike, na kuwalinda Mawaziri wake, na tena kwa kosa ambalo si lake. Watu walioshindwa uongozi Bungeni, hata tukafikishwa hapa tulipo leo, ni Waziri Mkuu na Katibu Mkuu wa CCM. Hawawezi kukwepa matokeo ya kusarenda kwao Bungeni, na wamtupie Rais, ati kwa sababu Rais wetu ni Rais Mtendaji na walipomshauri kusarenda kama wao, alikubali. Tukikubali hoja hiyo hakuna Waziri ye yote atakeyetakiwa kuwajibika kwa kosa lo lote; maana kila wakati Rais atatakiwa awajibike badala yake.


REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA (1994)

No comments:

Post a Comment