Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe
Miraji Jumanne Mtaturu akisalimia na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi,
Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) mara baada ya kuwasili katika uwanja
wa Maonesho ya wakulima Nane Nane kwa ajili ya kufunga maonesho hayo.
Naibu waziri ofisi ya Waziri
Mkuu- Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) akisikiliza kwa makini
maelekezo ya namna ya kuchakata mihogo kutoka kwa mkulima wa zao hilo tangu mwaka
1980 kutoka Kijiji cha Nzuguni Josiah Malogo Ndoya.
Mhe Mavunde (Mb) akisikiliza
kwa makini namna ya kulima mahindi kwa mbinu bora na za kisasa ili kuwa na
mavuno yenye tija.
Naibu waziri ofisi ya Waziri
Mkuu- Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) akisikiliza maelekezo
katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Chemba kuhusu umuhimu wa matumizi ya
dawa katika kilimo cha kisasa.
Mhe Mavunde alipotembelea
banda la ushonaji la Jeshi la kujenga Taifa JKT katika Maonesho ya Nane nane
kabla ya kuyafunga rasmi.
Mhe Mavunde alipotembelea
banda la maonesho ya wanyama aina ya mbuzi, Ng’ombe na Kondoo la kampuni ya
Ranchi za Taifa (NARCO LTD).
Naibu waziri ofisi ya Waziri
Mkuu- Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) akipokea zawadi ya mboga
za majani kutoka kwa vijana wa Jeshi la kujenga Taifa (JKT) mara baada ya
kutembelea banda hilo.
Mhe Mavunde alipotembelea
banda la Maonesho ya kilimo cha Vitunguu.
Mhe Mavunde akisalimiana na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma marabaada ya
kutembelea banda la maonesho la Wilaya hiyo.
Mhe Mavunde akitazama ubora
wa matrekta yaliyofikishwa katika Maonesho ya wakulima ya Nane Nane.
Naibu waziri ofisi ya Waziri
Mkuu- Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde (Mb) akiwa katika picha ya
pamoja na viongozi mbalimbali walioshiriki katika maonesho ya Nane nane katika
uwanja wa Nzuguni Kanda ya kati Dodoma.
Na Mathias Canal,
Dodoma
Maonesho
na Mashindano ya mifugo Kitaifa sanjari na Maonesho ya Kilimo yametoa
changamoto ya kuleta mapinduzi katika Ufugaji, Uvuvi, na Kilimo na kutoa ajira
hususani kwa vijana kuwaongezea zaidi kipato na kuondoa umasikini.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana na Ajira Mhe Antony P. Mavunde wakati akifunga
maonesho ya wakulima Nane nane Kanda ya Kati Dodoma yaliyokuwa yanafanyika
katika uwanja wa Nzuguni kwa kauli mbiu ya "Kilimo, Mifugo na Uvuvi ni
nguzo ya Maendeleo, Kijana shiriki kikamilifu (Hapa Kazi Tu).
Amesema
kwa kuwa serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais John Pombe Magufuli
inatekeleza azma ya kuhamishia makao makuu mjini Dodoma ameishauri Wizara ya
Kilimo, Mifugo, na Uvuvi na ile ya Biashara na masoko kuangalia uwezekano wa
kuanzisha rasmi maonesho ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi ya Kimataifa
(International Agriculture Trade Fair) katika uwanja wa Nzuguni ambao ndio
uwanja wenye eneo kubwa kwa maonesho ya Kilimo hapa nchini.
Aidha
ametoa wito kwa Wizara, taasisi/Makampuni ya umma na binafsi, Mabenki na wadau
wote wa kilimo na mifugo kuendelea kuwasaidia wakulima na wafugaji hapa nchini
ili kuongeza uzalishaji kuwezesha upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda
vinavyokusudiwa kuanzishwa.
"Naomba
niwaambie wakulima na wafugaji wetu kuwa maonesho ninayoyafunga hii leo ni
muafaka na fursa nzuri kwao hususani vijana kwenda kuanza mara moja kutumia
mlichojifunza na kuleta mapinduzi yenye maendeleo chanya yanayotarajiwa
kiuchumi, hivyo napenda kuchukua nafasi hii kuzikumbusha Halmashauri za
serikali za mitaa zote kuwahamasisha wakulima, Wafugaji na wadau wengine
kutumia teknolojia zilizooneshwa hapa kuongeza ufanisi wao katika Kilimo,
Mifugo na Uvuvi” Alisema Mavunde
Naibu
waziri huyo pia ametoa zawadi kwa washindi katika Halmashauri za Mkoa wa Dodoma
na Singida, Wizara za serikali, Taasisi za uzalishaji wa serikali, Makampuni ya
pembejeo za Kilimo na Mifugo, Makampuni ya zana za Kilimo na Mifugo, Taasisi za
serikali na Mashirika ya Umma, Taasisi za fedha na Mabenki, Taaisisi za mafunzo
na utafiti, Taaisisi zisizo za kiserikali (NGOs na CBOs), Taasisi za
mawasiliano ya kibiashara, Mamlaka za udhibiti, Vyombo vya habari, na Kampuni
za nishati mbadala kwa kufanya vizuri katika maonesho hayo.
Pia
zawadi hizo zimetolewa pia kwa watu wenye mashamba makubwa ya ufugaji ng'ombe
wa maziwa, Wafugaji wadogo wa ng'ombe wa nyama, Wafugaji bora, na Wakulima
bora.
Sambamba
na hao pia Jeshi la Kujenga Taifa JKT limeibuka kidedea kwa ushindi wa jumla
likifuatiwa na Jeshi la Magereza ambapo nafasi ya tatu imechukuliwa na Wizara
ya Kilimo, Mifugo na Uvuvu.
Akitoa
maelezo ya awali kuhusu maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa
Malengo ya maonesho hayo ni utoaji elimu ya matumizi ya teknolojia mbalimbali
kwa wadau wengi kwa muda mfupi lakini pia wadau kujionea na kujifunza huduma
zitolewazo na serikali, mashirika ya umma na binafsi.
Mtaturu alisema kuwa mpaka
tarehe 7 hapo jana jumla ya watu waliokuwa wametembelea inakadiriwa kuwa 40,000
huku matarajio ya siku ya ufungaji ikitarajiwa kuongezeka watu 12,000 na
kufikia idadi ya watu 52,000.
Dc Mtaturu amesema kuwa
Teknolojia/Bidhaa zilizooneshwa ni pamoja na zana za Kilimo, Mbegu bora za
mazao mbalimbali, Uzalishaji wa mazao katika mazingira yaliyodhibitiwa (JKT
Kondoa) Taasisi za kitafiti ambazo zimeonyesha teknolojia mbalimbali za
kuongeza tija zenye ukinzani dhidi ya magonjwa mbalimbali, Utengenezaji wa
chanjo dhidi ya magonjwa ya mifugo, Uboreshaji wa viasilu ili kupata mifugo na
mazao ya kilimo yanayostahimili hali ya hewa ya kanda ya kati na udhibiti wa
magonjwa.
Pia
uzalishaji bora wa mazao ya nafaka, ubunifu wa teknolojia rahisi za kutotoa
mayai, Kuongeza thamani mazao ya mifugo, Makampuni ya mawasiliano, Taasisis za
elimu zimeonyesha ubunifu wa kumsaidia mfugaji, Tiba za asili, Wasindikaji
wakubwa na wadogo wa mazao ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Asali, na Nta.
Akitoa
salamu za shukrani kwa niaba ya waandaaji wa Maonesho hayo Mkuu wa Wilaya ya
Singida Elias Tarimo amemshukuru mgeni rasmi Antony P. Mavunde kwa kuitikia
wito wa kufunga maonesho hayo ambapo pia ameishukuru Benki kuu ya Tanzania
(BOT), Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, LAPF,
Mkuu wa Mkoa wa Singida na Chuo kikuu cha Dodoma kwa uwakilishi na uchangiaji
kwa ajili ya maonesho hayo.
Maonesho
ya sikukuu ya wakulima Nanenane Kanda ya kati Dodoma yaliyohusisha shughuli za
wakulima, wafugaji wa mifugo, wafugaji wa nyuki, wavuvi, wanamazingira,
wasindikaji wa bidhaa za mazao ya kilimo na mifugo, wizara taasisi/makampuni ya
umma, makampuni binafsi, mabenki, Taasisi za umma na binafsi na mashirika
yasiyo ya kiserikali yalifunguliwa tarehe 03 Agosti 2016 na Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe.
No comments:
Post a Comment