TARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Young
Scientists Tanzania (YST) - Shirika la Wanasayansi Chipukizi Tanzania-
linapenda kuwafahamisha wanafunzi, walimu na wananchi kwa ujumla kuwa onesho la
wanasayansi chipukizi la mwaka 2016 litafanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere
International Convention Centre (JNICC) jijini Dar es Salaam tarehe
10-11/08/2016. Tukio hili ni muhimu kwa kuonyesha kazi za ugunduzi wa kisayansi
na teknolojia zilizotengenezwa na wanafunzi wa shule za sekondari kutoka mikoa
yote ya Tanzania. Tunawashukuru Irish Aid na BG Tanzania kwa kuendelea
kudhamini mashindano haya, sambamba na wadhamini wengine. Tunawakaribisha watu
wote waje wajionee vipaji vya vijana wetu siku ya tarehe 11/08/2016 kuanzia saa
2:00 asubuhi hadi saa 6:30 mchana.
Mwaka
huu wanafunzi 300 wataonyesha kazi zao za ugunduzi wakiwa na walimu/washauri
wao 150. Hili ni ongezeko kubwa la washiriki ukilinganisha na mwaka jana. Kwa
siku mbili, wanasayansi chipukizi wataonyesha ugunduzi wao katika sayansi ya
kemia, fizikia na hisabati; biologia na ekolojia; sayansi ya jamii na
tekinolojia. Ugunduzi huu umejikita hasa hasa kutafuta njia za kutatua matatizo
yahayohusiana na masuala ya afya, kilimo na usalama wa chakula, mawasiliano na
usafirishaji, nishati na mazingira, elimu, na matatizo ya kijamii.
Ili
kutambua kazi nzuri zilizofanywa na wanasayansi chipukizi, zawadi zitatolewa
kwa wanafunzi watakaoonyesha ugunduzi mzuri zaidi. Wanafunzi wapatao 50
watashinda zawadi za pesa, medali, vikombe, vifaa vya maabara, na kutengezewa
maktaba kwa shule itakayoshinda zawadi ya maktaba. Wanafunzi wanne watashinda
zawadi za udhamini wa kusomeshwa chuo kikuu katika fani za sayansi ili
kuwawezesha kuwa wanasayansi mahili miaka ya badae. Washindi wa jumla wa
mashindano ya mwaka huu watalipiwa gharama zote kwenda kuiwakilisha Tanzania
kwenye mashindano ya BT Young Scientists huko Ulaya nchini Ireland mwezi
Januari 2017 na pia watapewa udhamini wa kusomeshwa chuo kikuu.
Mashindano
ya mwaka huu ni ishara tosha kuwa namna ya ufundishaji sayansi katika nchi yetu
umeanza kubadilika. Utamaduni wa sayansi umeanza kujengeka miongoni mwa
wanafunzi kwani wameanza kusoma sayansi kwa wingi na kwa vitendo kwa kutumia
sayansi kutafuta suluhisho la matatizo ya kiuchumi na kijamii yanayozikabili
jamii zetu. Hii imefanya sayansi ifanyike kivitendo zaidi na kuwafanya
wanafunzi wapende kujihusisha katika masula ya sayansi na tekinolojia.
Tunawakaribisha
watu wote wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla kuwa kujionea ugunduzi huu wa
sayansi na teknolojia uliofanywa na wanasayansi chipukizi.
Mawasiliano: Dr.
Gosbert Kamugisha, Mkurugenzi & Mwanzilishi Mwenza - YST, +255767708579.
No comments:
Post a Comment