Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 8 August 2014

WANASAYANSI KUKUTANA DAR KONGAMANO LA 25 LA WAJIOLOJIA DUNIANI

Mtendaji  Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST ) na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya makongamano  ya Wajiolojia  Afrika na  wanasayansi vijana Duniani, Profesa Abdulkarim Mruma (katikati) akisisitiza jambo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu  kongamano la 25 la Wajiolojia Afrika na   mkutano wa tatu  wa vijana wanasayansi  kutoka nchi mbalimbali duniani. Makongamano hayo yanatarajiwa kufanyika tarehe 11- 16 Agosti, 2014 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud. Wengine, kwanza kulia ni Mwenyekiti wa mtandao wa Vijana wanasayansi kwa upande wa Tanzania Steven Nyagonda, Rais wa Vijana wanasayansi Duniani  Meng Wang na Katibu wa Kamati ya Maandalizi, Profesa Nelson Boniface.
2 (9)Rais wa Wanasayansi Vijana duniani, Meng Wang (wa pili kulia) akiongea jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelezea kuhusu mkutano wa tatu wa wanasayansi vijana kutoka nchi mbalimbali duniani, kulia ni Mwenyekiti kongamano la vijana wanasayansi upande wa Tanzania Steven Nyagonda, wengine wanaosikiliza niMtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Katibu wa kamati ya maandalizi, Profesa Nelson Boniface.
3 (8)Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Nishati na Madini Badra Masoud akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati wakitoa taarifa kuhusu kufanyika kwa kongamano la 25 la Wajiolojia Afrika na kongamano la tatu la wanasayansi vijana kutoka mataifa mbalimbali duniani. Kushoto ni Michael Msambi mjumbe wa kamati ya maandalizi na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya makongamano hayo, Profesa Abdulkarim Mruma (kulia).
Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Tanzania imepata fursa ya kuwakutanisha wanasayansi kutoka nchi mbalimbali za Afrika na duniani katika kongamano la 25 la Wajiolojia litakalokwenda sambamba na mkutano wa tatu wa kimataifa wa mtandao wa wanasayansi vijana.
Mtendaji Mkuu  wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya makongamano hayo, Profesa Abdulkarim Mruma, ameeleza kuwa, kongamano la Wajiolojia  litafanyika tarehe 15-16 Agosti, 2014, likijikita katika
kujadili masuala ya Jiolojia na namna Afrika inavyoweza kunufaika na taaluma hiyo kupitia sekta za nishati, madini, maji, utalii, na masuala mengine yanayohusu sekta hiyo.
Aliongeza kuwa, kutokana na mada mbalimbali zitazowasilishwa, na tafiti mbalimbali zitakazoainishwa katika kongamano hilo la wajiolojia, zitasaidia kuziwezesha nchi za Afrika kutangaza na kuhamasisha maeneo ya uwekezaji kupitia sekta za madini, mafuta, gesi ikiwemo kuendeleza masuala ya utalii na kuangalia namna inavyoweza kurithisha taaluma hiyo kwa kizazi kijacho.
“Tanzania ina masuala mengi ya kijiojia, utafiti mwingi wa kisayansi kupitia taaluma hii, umefanyika Tanzania, hivyo lazima tuiambie dunia kuhusu masuala ya kijiolojia na utalii lakini hasa kile tulichonacho hapa kwetu kwa maendeleo yetu na dunia,” aliongeza Mruma.
Aliongeza kuwa, zipo tafiti ambazo zimefanywa na kampuni mbalimbali zinazofanya utafiti wa mafuta vikiwemo vyuo vikuu mbalimbali kutoka Afrika ambazo zinatarajiwa kuwasilishwa katika kongamano hilo.
Akielezea kuhusu kongamano la vijana wanasayansi litakalofanyika kuanzia tarehe 11-14 mwezi huu, Profesa Mruma alieleza kuwa, linafanyika kwa mara ya 3 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2009 na kwamba, lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba masuala ya sayansi ya dunia yanarithishwa ipasavyo katika kizazi kijacho kwa lengo la kuendeleza rasilimali asilia zikiwemo mafuta, nishati ya jotoardhi ikiwemo kuendeleza sayansi ya jiolojia kwa vijana kwa maendeleo ya Afrika na dunia.
Aliongeza kuwa, kongamano hilo litawashirikisha vijana wanasayansi kutoka katika nchi 45 Afrika na mabara mengine na litatoa fursa kwa vijana wanasayansi kujadili masuala mbalimbali ya kisayansi.
Naye Rais wa vijana wanasayansi duniani,  Meng Wang, alieleza kuwa, kongamano la vijana    ni muhimu kwa Afrika na hususani Tanzania  kutokana na kuwa ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mwingi wa masuala ya kijiolojia na masuala ya utalii.
“Mengi yanayotarajiwa kuzungumzwa katika makongamano haya yanaigusa Tanzania moja kwa moja, hii ni fursa kubwa hasa kwa vijana wanasayansi na wasio wanasayansi kutokana na kwamba jambo hili litachangia kujenga ari ya vijana kuingia katika taaluma hii”, alisisitiza Wang.
Akieleza zaidi kuhusu kongamano la vijana Mwenyekiti wa   mtandaohuo wa vijana kwa upande wa Tanzania Steven Nyagonda, alieleza vijana, waliona ipo haja ya kukutana kuangalia namna masuala mbalimbali yanayoikabili dunia kupitia taaluma ya sayansi ili kuunganisha jitihada za kizazi kilichopo na kijacho jambo ambalo litawezesha kizazi kijacho kuirithi taaluma hiyo.
Aliongeza kuwa, kongamano hilo litaangalia masuala mbalimbali ikiwemo kujadili matatizo yanayotokana na taaluma hiyo, kupata uzoefu wa namna nchi nyingine duniani zinavyotumia sekta ya nishati, namna elimu ya sayansi inavyoweza kuisaidia dunia, katika mazingira, mabadiliko ya tabia nchi pamoja na masuala mengine yanayohusu dunia kupitia sayansi na jiolojia.
“Zaidi pia tunalenga kuwavutia vijana wengi wapende masomo ya sayansi hususani somo la hisabati, lakini zaidi sisi vijana wanasayansi wa Tanzania tunataka vijana wa kitanzania waipende sayansi,” alisisitiza Nyagonda.
Aliongeza kuwa, zaidi ya tafiti 400 kutoka kwa vijana wanasayansi sehemu mbalimbali duniani zimewasilishwa kwa kamati ya vijana ya dunia, ambapo kati yake tafiti 50 ziliwasilishwa na vijana wanasayansi wa Watanzania.
Makongamano yote la Wajiolojia Afrika na wanasayansi vijana kutoka nchi mbalimbali duniani yanatarajiwa kufunguliwa rasmi  tarehe  11 Agosti, 2014, na Makamu wa Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohamed Gharib Bilal akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Jakaya  Mrisho Kikwete.
CREDIT: FULLSHANGWE

No comments:

Post a Comment