Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 17 August 2014

NAWAKUMBUSHA TU: SERIKALI ILIKUBALI HOJA YA TANGANYIKA, LAKINI IKAMKEMEA MSEKWA!!


Pius Msekwa


Nchi mbili zinapoungana na kuwa Nchi moja mifumo ya kawaida ya miundo ya Katiba ni miwili: Muungano wa Serikali Moja, au Shirikisho la serikali Tatu. Kwa mfumo wa kwanza kila nchi itafuta serikali yake na nchi mpya inayozaliwa itakuwa ni nchi moja yenye Serikali moja. Katika mfumo wa pili kila nchi itajivua madaraka ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho na itakuwa na serikali ambayo ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yaliyobaki.

Mambo yatakayoshikwa na serikali ya Shirikisho ili yale ambayo yatashikwa na serikali ya shirikisho ni yale ambayo yakibaki katika nchi zilizoungana basi kwa kweli nchi hizo zitakuwa hazikuungana kuwa nchi moja bali zinaendelea kuwa nchi mbili zenye ushirikiano mkubwa katika mambo fulani fulani.

Nchi za Afrika Mashariki zilikuwa katika hali kama hiyo kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Zilikuwa ni Nchi Tatu zenye ushirikiano mkubwa, lakini hazikuwa Nchi Tatu zilizoungana kuwa Nchi Moja yenye muundo wa Shirikisho. Shirikisho halisi la nchi mbili litakuwa ni Nchi Moja yenye Serikali tatu, Serikali ya Shirikisho, na Serikali mbili za nchi mbili za awali zilizoungana kuzaa nchi mpya moja.

Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa Nchi Moja, tungeweza kufuata mmojawapo wa mifumo hiyo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zan­zibar na ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali Moja ungefanya ionekane kama Tangan­yika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania Uhuru na Umoja wa Afrika; hatukutaka tuuhaniwe hata kwa makosa, kwamba tunaanzisha ubeberu mpya!

Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali Moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzi­bar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya vivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tan­ganyika ndio hasa ungeendesha SerikaIi ya Shirikisho. Kwa hiyo Tan­ganyika ingeendesha Serikali yake ya watu 12, 000, 000 na pia ndiyo ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu 12,300,000.

Ni Watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizo ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tan­ganyika isingekuwa ndogo, (waulizeni Wazanzibari), na wala ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo. Hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tan­ganyika.

Kwa hivyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na SerikaIi yake, itaonekana kuwa imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali Moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute mfumo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa, bila kuibebesha Tanganyika mzigo wa kuendesha Serikalli mbili zenye uzito unaolingana.

Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndiyo asili ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazamia hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo uliotufaa zaidi.

Labda ni vizuri kukumbusha kwamba shabaha ya baadhi yetu ilikuwa ni kuunganisha nchi za Afrika Mashariki ziwe nchi moja. Na wakati Zanzibar na Tanganyika zinaungana, Kenya, Uganda na Tanganyika zilikuwa katikati ya mazungurnzo ya kutafuta uwezekano, wa kuungana. Kama jambo hilo, lingetokea, nina hakika kabisa kwamba mfumo wa nchi mpya ambayo ingezaliwa ungelikuwa ni Shirikisho; au la Shirikisho la Nchi Tatu zenye Serikali Nne, na Shirikisho la Nchi Nne zenye Serikali Tano.

Kwa kweli hata kesho Nchi za Afrika ya Mashariki zikiamua kuungana, na Tanzania ikawa ni mshiriki, naamini kuwa ni rahisi zaidi kushirikisha Tanzania yenye Serikali Mbili - ya Zanzibar na ya Tanganyika - kuliko Tanzania yenye Serikali Mbili, ya Tanzania na ya Zanzibar. Wapendao Utanganyika watakuwa wazalendo zaidi, badala ya kuwa wasaliti, wakiazimia Afrika ya Mashariki iliyoungana kuwa Nchi Moja. Kuliko Tanzania iliyotengana ikawa nchi mbili.

Siku ya pili yake tarehe 15:8:1993, Wabunge wenye hoja yao na wengine zaidi, waliomba tena kuja 'Tunywe chai'. Na baada ya mazungurnzo nao ilikuwa ni dhahiri kabisa kwangu kwamba hata kama hawakuondoa hoja yao. (wala mimi sikuwaomba waiondoe), wataitumia kutoa dukuduku zao tu; hawataitumia kung'ang'ania kudai Serikali ya Tan­ganyika. Kwa hiyo sikushangaa baadaye niliposikia kuwa waliiondoa hoja yao ya awali, na badala yake wakaleta hoja ya kutafuta maoni ya wananchi. Mimi kwa upande wangu nilihisi kuwa hoja mpya hii ilikuwa na shabaha ileile ya "kunawa uso", kama Zanzibar kusema kuwa wanatoka katika OIC, lakini utafanywa uchunguzi wa kuona kama Tanzania inaweza kuingia katika OIC.

Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum Zanzibar kuhusu Muungano. Tukakataa kwa sababu safi kabisa. Maoni haya ya Wabunge wa Bara ambao mimi naamini kabisa si wapinzani wa Muungano, nayo yangeweza kukataliwa na Chama na SerikaIi, kwa sababu zile zile na mambo yakesha.

II SERIKALI INASARENDA

Baadaye, nadhani siku iIiyofuatia, niliitisha kikao cha Watangazaji wa Habari, nikapinga kwa kirefu hoja ya Utanganyika. Wakati naondoka Dar es Salaam ili kurudi Butiama, nilitumaini kabisa kwamba Serikali ingeendeleza Bungeni, na kama na kama hapana budi nchini, kazi tuliyoanza pamoja, ya kupinga hoja ya Tanganyika. Sikuwa na sababu yoyote ya kuhofia kuwa siku chache tu baadaye Serikali itageuza msimamo wake na kufanya "abautani".

Sijui lililotokea, maana kila nilipouliza sikupata maelezo. Kama nilivyokwisha kusema hapo nyuma baadaye wabunge wahusika waliiondoa hoja yao ya awali ya kutaka Bunge lipitishe azimio la kudai Serikali Tatu, wakaleta hoja mpya ya kutaka Serikali ifanye referendamu ya kutafuta maoni ya wananchi kuhusu suala hili. Nasema, SerikaIi ingeweza kuikataa hoja hii kwa maelezo safi kabisa na mambo yakesha.

Au kama wangeona kuwa si siasa nzuri kuipinga hoja hii nayo, wangeweza kuikubali, na mimi nina hakika, wananchi wangeikataa na mambo yakesha. Lakini Serikali ya Muungano, bila maelezo ilikataa hoja mpya ya wabunge ya kutaka maoni ya wananchi, na yenyewe ndiyo ikafufua hoja ya Utanganyika, na kupendekeza kwamba badala ya hoja ya Serikali Tatu kujadiliwa Bungeni na kupigiwa kura, Bunge zima, pamoja na Serikali yenyewe, likubali hoja hiyo, bila mjadala!

Kumbe jambo ambalo viongozi wetu walikuwa wanahofu kabisa kabisa ni mjadala, maana huo ungewalazimisha kujitambulisha kama si katika mjadala wenyewe, basi wakati wa kupiga kura, hasa ikiwa ni kura ya kuita mbunge mmoja mmoja kwa jina, pamoja na mawaziri wetu! Badala ya kupita katika adha hiyo wakaona afadhali wakubali Serikali Tatu, bila ya mjadala. Basi SerikaIi yetu ikanywea ghafIa, kama mpira uliotoboka au puto lililopasuka. Nadhani hata wabunge wenye hoja ya awali walishangaa!

Kuongoza ni kuonyesha njia. Viongozi wetu walikuwa Wametumwa na chama chao waende bungeni, Bunge Ia wanachama watupu wa CCM wakawaonyeshe njia. Wakawaambie wabunge wahusika kwamba hoja yao ya kutaka Serikari Tatu ni kinyume cha sera ya chama chao, na ina hatari ya kuigawa na kuiangamiza Nchi yetu.

WaIiagizwa wazi wazi wakaipinge hoja hiyo. Wakapata mtihani mdogo sana bungeni. Wakasarenda. Wakatupa silaha chini; wakasalimu amri. Viongozi hawa hawawezi kusimama mbele ya Kamati Kuu, au mbeIe ya Halmashauri Kuu ya Taifa kusema kwa fahari kama wao ni hodari: Kazi mliyotutuma tumeikamilisha! Wala hawataki kukubali matokeo ya kusarenda kwao.

Kwa sababu uamuzi wa kutaka Serikali ya Tanganyika ‘ndani ya muungano’ ulifanywa na viongozi wetu kwa hila, na kupitishwa bungeni bila mjadala, sisi wengine hatukujua lililotokea. Baadaye tulifahamishwa kuwa huo ndiyo ulikuwa uamuzi wa ‘bunge zima” kutokana na kauli ya Pius Msekwa aliyekuwa msimamizi wa kikao cha Bunge kilichofikia uamuzi huo.


Nadhani viongozi wetu walitaka kuendelea kuficha na kuuvuga vuga, lakini yeye akatoboa. Nasikia baadaye aliitwa akakemewa. Sijui kwa nini.

REJEA: NYERERE, J.K.; UONGOZI WETU NA HATMA YA TANZANIA

No comments:

Post a Comment