Zanzibar. Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
Amani Abeid Karume jana alifika Kituo cha Polisi Madema kumjulia hali
shemeji yake, aliyewahi kuwa Waziri wa SMZ, Mansour Yusuph Himid ambaye
alikamatwa na silaha mbili za moto na risasi 412, nyumbani kwake
Chukwani hivi karibuni.
Karume alifika katika kituo hicho ambacho ni Makao
Makuu ya Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi saa 5.30 asubuhi na kumjulia
hali Himid ambaye amewekwa mahabusu akisubiri uchunguzi wa polisi dhidi
ya tuhuma zinazomkabili.
Habari za uhakika kutoka ndani ya polisi zinadai
kuwa Rais Karume alizungumza na shemeji yake kwa muda usiopungua dakika
tano na kumtaka kuwa mstahimilivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na
utaratibu wake.
Viongozi wengine waliofika katika kituo hicho
ambacho kimeimarishwa ulinzi tangu alipofikishwa juzi, ni pamoja na
wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CUF; Hija Hassan Hija (Kiwani),
Saleh Nassor Juma (Wawi), Hassan Hamad Omar (Kojani ) na Naibu Waziri wa
Maji, Nishati, Makazi na Ardhi, Haji Mwadini Makame ambao walimpa mkono
wa pole 6.30 mchana.
“Mansour anastahili pongezi na siyo kupewa pole,
inashangaza mambo ya ulinzi na usalama ni ya Muungano kwa nini upande
mmoja uruhusiwe kumiliki silaha na upande mwingine uzuiwe, ndiyo maana
tunasema Zanzibar haitendewi haki,” alisema Hija muda mfupi baada ya
kutoka kituoni.
Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi linapaswa
kuendelea na operesheni ya kuwasaka viongozi wengine wanaomiliki silaha
na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa vile tukio hilo limewafunza
mambo mengi na kutaka haki itendeke.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai
Zanzibar, Salum Msangi alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio
hilo na matokeo yake ndiyo yatakayoamua wapi pa kufunguliwa mashtaka
kati ya Zanzibar au Tanzania Bara.
“Kwa mujibu wa sheria za Zanzibar, hairuhusiwi raia yeyote kumiliki bastola,” alisema.
Himid alipekuliwa nyumbani kwake juzi baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za kiintelejensia kuwa anamiliki silaha za moto.
Taarifa kutoka katika eneo la tukio zinaeleza kuwa
kazi ya upekuzi wa nyumba mbili zilizopo katika eneo moja ilifanywa kwa
kutumia mashine maalumu.
Credit: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-Karume-atinga-polisi-/-/1597296/2407664/-/9fx58ez/-/index.html
Credit: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-Karume-atinga-polisi-/-/1597296/2407664/-/9fx58ez/-/index.html
No comments:
Post a Comment