Na Daniel Mbega, Iringa
CHINI ya
miti ya mikaratusi, kando ya Mto Mlowa, vijana wanaonekana wakijaza nyanya
kwenye matenga ya mbao huku pembeni yao kukiwa na malundo makubwa ya zao hilo.
“Hii ni
hasara kubwa, nimekuja na matenga hamsini, lakini inaonekana yametoka
thelathini tu, haya malundo yote ni nyanya zilizolainika (masalo) ambazo
haziwezi kwenda mahali popote,” anasema Jacob Kamota, mkulima wa nyanya kutoka
Kijiji cha Iyayi, Kata ya Image wilayani Kilolo.
Jacob
analalamika kwamba, huko shambani pia ameacha malundo ya nyanya zisizofaa
kusafirishwa, ingawa zinafaa kwa matumizi ya nyumbani au hata kwa kusindikwa,
hali ambayo inazidi kumtia umaskini badala ya kujikwamua kiuchumi.
“Sina
mahali pa kuzipeleka, laiti kungekuwepo na kiwanda ningeweza kuuza nyanya zote
na kupata faida, lakini sasa hata gharama zangu sidhani kama zinaweza kurudi,”
anasema.
Mkulima
huyo anasema, gharama za shamba lake lenye ukubwa wa ekari moja zilikuwa Sh. 1
milioni na kwamba alipovuna alipata jumla ya matenga 80, lakini matenga 30
yalionekana yameharibika tangu shambani huku mengine 20 yakiharibika wakati
alipozifikisha nyanya hizo kwenye soko dogo kando ya mto huu.
Bei ya
soko ambayo aliikuta kwa siku hiyo ilikuwa Sh. 5,000 tu kwa tenga moja, hivyo
kujikuta akiambulia Sh. 150,000 kwa matenga yake 30 ambayo yalionekana yanafaa
kusafirishwa.
Jacob ni
miongoni mwa wakulima wengi wa Mkoa wa Iringa wanaojishughulisha na zao la
nyanya ambao wamekuwa wakipata hasara kila mwaka kutokana na ukosefu wa soko la
uhakika.
Inaelezwa
kwamba, zaidi ya asilimia 70 ya zao hilo la nyanya, ambalo ndilo kuu la
biashara mkoani Iringa, inaharibika kutokana na ukosefu wa soko na miundombinu
bora, hasa barabara.
Wakulima
ndio wanaoathirika zaidi licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo.
Hali hiyo imewafanya
wakulima wengi kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini, huku wengine
wakipunguza ukubwa wa mashamba yao ama kutolima kabisa kutokana na kukosa uwezo
wa kuyahudumia.
Maulid
Kiboma ‘Papara’ ni mfanyabiashara ambaye anasema nyanya inayoharibika ni kiasi
kikubwa zaidi kuliko inayofika sokoni.
“Nyanya
ikifika hapa sokoni kutoka shambani kiasi kikubwa inakuwa masalo, hivyo inabidi
ichaguliwe na iliyo bora ndiyo inayosafirishwa.
“Kabla ya
kufika hapa sokoni mkulima anakuwa ameichambua na kuyaacha masalo shambani,
lakini ikishachambuliwa tena hapa, hata kama ana matenga 10, anaweza kujikuta
amebaki na manne tu ambayo ndiyo tunanunua,” anasema Papara.
Papara
anasema, wafanyabiashara pia wanapoifikisha nyanya hiyo kwenye masoko makubwa,
hasa Dar es Salaam, wanalazimika kuichambua, hivyo kiasi kinachobakia kwa ajili
ya matumizi kinakuwa kidogo zaidi ya kilichozalishwa.
Anaongeza
kwamba, wakati mwingine bei katika soko la Dar es Salaam inaporomoka kiasi
kwamba hata wafanyabiashara wenyewe huamua kutonunua zao hilo kwa ajili ya
kusafirisha kwa kuhofia kupata hasara.
Mfanyabiashara
huyo anasema, bei inaposhuka katika masoko makubwa inakuwa hasara zaidi kwao
wafanyabiashara wa kati, ambapo hata wakipewa nyanya hizo bure na wakulima
hawawezi kuchukua.
“Suluhisho
pekee litakalomkomboa mkulima ni kujenga kiwanda cha kusindika matunda na mboga
mboga ili wakulima waweze kuuza nyanya zote na kukuza kipato chao,” anasema.
Anasema
kiwanda pekee cha Dabaga kilichoko Iringa mjini hakitoshelezi, hivyo kuitaka
serikali na wadau wengine wa maendeleo kufikiria namna ya kuwakomboa wakulima
hao.
Masoud
Said, mfanyabiashara wa nyanya kutoka Dar es Salaam, anasema serikali, pamoja
na kufikiria kujenga viwanda, lakini pia ijenge masoko ya uhakika vijijini
ambayo yatawafanya wakulima wawe na mahali pa kupeleka bidhaa zao badala ya
eneo la sasa lililoko katikati ya vijiji vya Iyayi na Uhominyi katika Kata hiyo
ya Image.
“Walikuja
hapa watu sijui wa Techno Save, wakajenga kijibanda kidogo pale Iyayi kwamba
ndilo soko. Pale wamewachezea tu wananchi na kutafuna bure fedha za mradi kwa
sababu nyanya zinazozalishwa kwenye maeneo haya ni nyingi kuliko kijibanda
kile.
“Jambo
jingine ni kujenga barabara imara ambazo zitapitika katika majira yote, tofauti
na sasa ambapo barabara ya kutoka Ilula hadi huku Image iko kama mgongo wa
mtumbwi kiasi ambacho magari mawili hayawezi kupishana,” anaongeza Masoud.
Martin
Kazingumu Kutika, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Image, akizungumzia changamoto ya
soko la nyanya, anasema inawatesa wakulima wengi, ingawa juhudi mbalimbali
zimekuwa zikifanywa na serikali kuboresha mazingira ya soko hilo.
“Nyanya
nyingi zinaharibika japokuwa wakulima wanakuja huku kuzifuata. Bei nayo
inapanda na kushuka kiasi kwamba ni vigumu kwa mkulima kunufaika moja kwa
moja,” anasema.
Anaongeza
kwamba, kujengwa kwa soko katika Kijiji cha Iyayi kutapunguza kero kwa wakulima
na wafanyabiashara, kwani eneo lililopo soko la sasa siyo rasmi na linamilikuwa
na Shule ya Msingi Uhominyi.
Ofisa
Kilimo wa Mkoa wa Iringa, Shenal Nyoni, anakiri kuongezeka kwa uzalishaji wa
nyanya mkoani humo, ambapo anasema kwa msimu wa 2011/2012, jumla ya hekta 6,817
zililimwa kwa umwagiliaji na tani 115,514 zilivunwa.
Hata
hivyo, anasema changamoto ya masoko inaendelea kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga
masoko madogo vijijini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kama
mashirika ya Techno Save, Muvi na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido).
Anasema
kujengwa kwa masoko hayo kutawawezesha wakulima kufikisha mazao yao mahali
pamoja na kujua bei inayozunguka sokoni, hivyo kuwaepusha na walanguzi ambao
wanawapunja.
“Kuna
mwekezaji mmoja ambaye alikuwa amejitokeza kutaka kujenga kiwanda katika Kijiji
cha Viwengi, ingawa sijajua amefikia hatua gani, lakini naamini kikijengwa
kitasaidia uchumi hasa kwa zao la nyanya ambalo kwa kweli linategemewa na wakulima
wengi mkoani Iringa,” anasema.
Lakini tayari kampuni ya Darsh Industries Limited
inayozalisha bidhaa maarufu nchini za Redgold imekamilisha ujenzi wa kiwanda katika
Kijiji cha Ugwachanya, Kata ya Mseke, takriban kilometa 12 kutoka Iringa mjini
na iko katika hatua za mwisho kuanza uzalishaji.
Mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo anayeshughulikia masuala ya
ujenzi huo, Pratap, anasema uzalishaji utakapoanza kiwanda hicho kitahitaji
jumla ya tani 200 (kilogramu 200,000) za nyanya kwa siku, sawa na kreti 4,500
au magari 20 aina ya Fuso yenye uwezo wa kubeba tani 10 kila moja.
“Tunahitaji tani 200 kwa siku, ndio uwezo wa kiwanda, na
tunawahakikishia wakulima kwamba soko la uhakika litapatikana wala wasiwe na
hofu,” anasema Pratap.
Ofisa huyo anasema, kiwanda kitanunua nyanya za madaraja
yote bila kubagua, hivyo hakutakuwa na ‘masalo’ yatakayomwagwa na kwamba wakulima
wawe na imani watapata tija kutokana na kilimo hicho.
Anaongeza kusema kwamba, watapeleka makreti ya kubebea
nyanya kwenye vituo vyote vya kukusanyia zao hilo ambavyo vitateuliwa na kwamba
wakulima hawatagharamia usafiri wa kupeleka kiwandani.
“Wakulima kazi yao itakuwa kupeleka nyanya kwenye vituo
ambako tutakuwa tumepeleka makreti ya kubebea, usafiri utakuwa ni juu ya kiwanda,”
anafafanua na kuongeza kwamba, pamoja na kununua nyanya kwa wakulima, ambayo ni
malighafi ya kiwanda hicho, lakini uongozi utatoa huduma za ugani kwa wakulima
ukishirikiana na Mradi wa Tanzania Agricultural Productivity (TAPP) pamoja na
maofisa ugani wa vijiji na kata husika linakolimwa zao hilo.
Ujenzi wa viwanda ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao
yanayolimwa Tanzania ni moja ya ahadi za serikali ya sasa chini ya Rais John
Magufuli, ikiwa na lengo pia la kuzalisha ajira kwa Watanzania.
Aidha, uzalishaji wa bidhaa za ndani ukiimarika, kuna
uwezekano wa kuuza bidhaa hizo nje, hivyo kuongeza pato la serikali pamoja na
fedha za kigeni.
0656-331974
No comments:
Post a Comment