Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servacius Likwelile (katikati) akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kuhusu Serikali ilivyojipanga kuboresha na kuhudumia sekta mbalimbali nchini ikiwemo elimu, umeme, maji na miundombinu. Kulia ni Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alfayo Kidata na kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu akisistiza wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es salaam kuhusu mapato na matumizi ya Serikali yalivyoboreshwa na uchumi wa nchi kuimarika na kutengemaa.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Servacius Likwelile leo jijini Dar es salaam kuhusu Serikali ilivyojipanga kuboresha na kuhudumia sekta mbalimbali nchini ikiwemo elimu, umeme, maji na miundombinu.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Fedha na Mipango)
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI
YATOA VIPAUMBELE VYAKE KWA WANANCHI.
Serikali imetoa jumla ya Sh.
Bilioni 318.406 kwa mwezi wa Januari mwaka 2016, kwa ajili ya miradi ya
maendeleo nchini na Sh. Bilioni 538.5 kwa mishahara ya watumishi wa Umma.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji
Mkuu wa Serikali, Dkt. Servacius Likwelile alisema kuwa Serikali inajivunia
kufanikiwa kutumia fedha za ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo hadi
sasa Serikali imetumia kiasi cha Sh. Bilioni 71.2 tu kutoka fedha za nje.
Dkt. Likwelile alisema mapato
yanayokusanywa nchini yamewezesha kutekeleza sera ya elimu bure ambapo mwezi Desemba mwaka 2015 Serikali ilitoa
kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa shule za msingi na sekondari kwa ajili ya
ruzuku, ada na chakula kwa shule za bweni pamoja na mahitaji mengine ambapo
mwezi wa Januari 2016 Serikali imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 18.77 kwa ajili ya kutekeleza
Sera hiyo.
Aliongeza kuwa katika ulipaji
wa madeni ya wakandarasi nchini , Serikali imetoa Sh. Bilioni 130 kwa mwezi Januari
mwaka 2016 ambapo mwezi Desemba mwaka 2015 ilitoa Sh. Bilioni 193.
Kwa upande wa Mfuko wa Barabara,
Katibu Likwelile alifafanua mradi huo umetengewa kiasi cha Sh. Bilioni 47.89 na
kuongeza kuwa Benki kuu ina fungu la mfuko huo ambapo nayo imetenga kiasi cha Sh.
Bilioni 76.3.
Dkt. Likwelile alisema kuwa Halmashauri
zitapelekewa kiasi cha Sh. Bilioni 20.52 kwa ajili ya kuboresha barabara na jumla
mfuko huo kufikia kiasi cha Sh. Bilioni 274.71.
Akifafanua kuhusu miradi ya
umeme, Dkt. Likwelile alisema kuwa mwezi Desemba mwaka 2015 Serikali ililipa
deni la TANESCO kiasi cha Sh. Bilioni 80 za mradi wa Kinyerezi II na kwa mwezi Januari
mwaka 2016 kiasi cha Sh. Bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya mradi huo.
Hali hii imefikisha kiasi cha Sh.
Bilioni 120 kwa ajili ya kulipa madeni na kuendeleza uzalishaji wa umeme nchini.
Alisema kiasi cha Sh. Bilioni 21.959
kimetengwa kwa ajili ya mradi wa umeme vijijini na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina
mfuko wa mradi huo ambao kwa sasa una kiasi cha Sh. Bilioni 21.9 na kuongeza
kuwa huduma ya umeme kwa wananchi itaimarika.
Alifafanua kuwa Serikali imeanzisha
mfuko wa maji Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambapo mpaka sasa mfuko huo una jumla
ya kiasi cha Sh. Bilioni 46.3.
Aidha, BoT imetoa Sh. Bilioni 12.5
kuendeleza miradi ya maji ambapo kwa Januari mwaka 2016 Serikali imetenga kiasi
cha Sh. Bilioni 7.7.
Serikali imetenga kiasi cha Sh
Bilioni 82.2 kwa mwezi wa Januari ili kuweza kulipa pensheni za wastaafu, na
kwa wale wastaafu walio katika daftari la kudumu ambapo wametengewa kiasi cha Sh.
Bilioni 33.3 kwa ajili ya malipo yao.
Wabunge wametengewa kiasi cha Sh.
Bilioni 35.5 kwa ajili ya mkopo wa magari ambapo kila mbunge atapata kiasi cha Sh.
Milioni 90, kiasi cha Sh. Milioni. 45 ni ruzuku na Sh. Mil. 45 ni
mkopo ambao utalipwa ndani ya miaka 5.
Aidha, Serikali imetenga kiasi
cha Sh. Bilioni 784.3 kwa ajili ya kulipa deni la taifa.
Naye Kamishna wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata alibainisha kuwa hali ya makusanyo ya
mapato nchini iko vizuri ambapo kwa mwezi Januari 2016, makadirio yalikuwa Sh.
Trilioni 1 na Bilioni 45 na hadi kufikia sasa kiasi cha Sh. Trilioni 1 na Bilioni
31 zimeshakusanywa.
Matarajio ya TRA ni kukamilisha
kukusanya kiasi cha Sh. Billioni 14 zilizosalia.
Aidha, Kidata alibainisha kuwa
uingizaji wa bidhaa kupitia bandarini bado uko vizuri licha ya minong’ono kuwa
uzuiaji wa mianya ya ukwepaji kodi imepunguza uingizaji bidhaa ambapo kwa mwezi
Januari Bilioni 111 zimekusanywa kutokana na ushuru wa forodha.
Kidata alitoa wito kwa kila
mtanzania kulipa kodi na kutoa taarifa za wakwepa kodi ili kuweza kukuza mapato
ya nchi.
Kwa upande wake Gavana wa Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Benno Ndulu amepongeza juhudi za ukusanyaji wa
mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali.
Alisema kuwa uchumi umekua na
unazidi kuimarika licha ya changamoto za kiuchumi duniani ambapo uchumi wa nchi
umekua kwa asilimia 7 na unategemewa kukua miezi ijayo kutokana na kuongezeka
kwa uzalishaji nchini.
Mfumuko wa bei unaendelea
kubaki ndani ya kiwango cha tarakimu moja, licha ya ongezeko dogo katika miezi
ya hivi karibuni kutokana na kupanda kwa bei za vyakula.
Alisema kuwa mfumuko wa bei ulikuwa
asilimi 6.8 mwaka 2015, ukilinganishwa na asilimia 6.1 kwa mwaka wa fedha ulioishia
Juni 2015.
Wakati huo huo mfumuko wa bei
usiojumuisha chakula na nishati uliendelea kubaki katika viwango vya chini ya
asilimia 2.5 kutokana na hatua mbalimbali za kisera zilizochukuliwa na BoT.
Prof. Ndulu alifafanua mapato
ya fedha za kigeni yanaendelea vizuri ingawa bei ya dhahabu imeshuka kutoka Bilioni
2.5 hadi Bilioni1.3.
Sekta ya utalii imesaidia
kuimarisha fedha za kigeni kwani mapato yameongezeka kutoka Bilioni 1.5 hadi Bilioni
2.2.
Sekta ya viwanda nayo imeshika
nafasi ya pili katika kuongeza fedha za kigeni nchini ambapo mwaka 2015 mapato yalikuwa Bilioni 1 na kwa sasa
yamefikia Bilioni1.5.
Aidha, Prof. Ndulu aliongeza
kuwa sekta ya usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi imesaidia kuimarisha fedha za
kigeni ambapo mapato yamefikia Dola Bilioni11 kwa mwaka.
Hadi kufikia sasa Tanzania imenufaika
kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika uingizaji bidhaa hiyo kwa
asilimia 44.
Serikali inatarajia kuendelea kuimarisha
uchumi ili kufikia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati hadi ifikapo 2025.
Imetolewa
na Wizara ya Fedha na Mipango
Kitengo
cha Mawasiliano
No comments:
Post a Comment