Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday, 31 January 2016

UWEKEZAJI KATIKA ARDHI NI MAJANGA


Na Daniel Mbega, Morogoro

SERIKALI, kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) iko kwenye mchakato wa kupitia zabuni kwa ajili ya uwekezaji kwenye mradi mkubwa wa kilimo cha miwa na mpunga wa Mkulazi, Wilaya ya Morogoro Vijijini, mkoani Morogoro katika eneo la hekta 60,000.
Taarifa zinasema, hekta 40,000 katika mradi huo zimetengwa kwa kilimo cha miwa kitakachokuwa na mashamba mawili yenye hekta 20,000 kila moja na hekta 20,000 zilizosalia zimetengwa kwa kilimo cha mpunga katika mashamba manne yenye ukubwa wa hekta 5,000 kila moja.
Eneo hilo la Mkulazi lililoko umbali wa kilometa 60 kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam – Morogoro pembezoni mwa reli ya Tazara linaelezwa kuwa linafaa kwa kilimo cha mazao hayo kwa kutumia Mradi wa Bwawa la Kidunda na kwamba miradi hiyo itakapoanza itasaidia kuleta uhakika wa akiba ya chakula pamoja na kupunguza uhaba wa sukari nchini.
Hata hivyo, kwa mujibu wa waziri wa zamani wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, mradi huo hautawaathiri wakazi 5,166 wa Kata ya Mkulazi kwa ama kumega maeneo yao au kuwahamisha na kwamba ni sehemu ya utekelezaji wa Kilimo Kwanza kupitia Mpango wa kuendeleza Kilimo wa Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Kwa mujibu wa TIC, uhawilishaji wa mashamba hayo utakuwa wa miaka 66 na mashamba yanayotajwa kwa kilimo cha miwa ni Shamba Na. 217/1 na Na. 217/2 ambayo kila moja lina ukubwa wa hekta 20,000 wakati mashamba Na. 217/3, 217/4, 217/5 na 217/6 yenye ukubwa wa 5,000 kila moja yatahusika na kilimo cha mpunga.
Uwekezaji huo unakuja wakati tayari TIC imesema imesajili jumla ya miradi 885, ikiwemo ya kilimo, inayotegemea kuzalisha ajira 198,573 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 88,134.92 kwa kipindi ambacho hata hivyo hakijabainishwa ni cha kuanzia mwaka gani.
Taarifa za uchunguzi zinaonyesha hata hivyo kwamba, ingawa miradi ya uwekezaji katika kilimo ni michache kulinganisha na sekta nyingine, lakini ndiyo inayowatafuna Watanzania walio wengi kutokana wawekezaji hao, wengi wakiwa wageni, kumegewa mapande makubwa zaidi ya ardhi.
Hatua hiyo imewafanya baadhi ya wananchi kuishauri serikali kutunga sheria zitakazozuia umilikaji wa ardhi kwa wageni ambao wanaichukua kwa ajili ya kilimo kupitia mpango wa uwekezaji wa moja kwa moja, kwani inaweza kuzua majanga makubwa katika miaka ijayo.
Mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira, Mchungaji William Mwamalanga, anakiri kwamba, kwa miaka takriban kumi iliyopita kumekuwepo na kasi kubwa ya uwekezaji wa wageni katika kilimo.
Ardhi imebaki kuwa rasilimali pekee kwa watu wananchi, lakini imekuwa ikitolewa kiholela kwa vigezo vya uwekezaji. Uuzaji wa ardhi kwa watu binafsi wa ndani na nje kwa kigezo cha uwekezaji wa moja kwa moja lazima uwe na mipaka na ikibidi ardhi iliyouzwa irejeshwe haraka. Tunahitaji wawekezaji, lakini hii siyo aina ya uwekezaji ambao utawanufaisha wananchi,” anasema Mchungaji Mwamalanga.
Anasema serikali inapaswa kuweka ukomo wa ununuaji wa ardhi ya vijijini kwa makampuni ama watu binafsi kutoka nje ambao wanataka kuzalisha chakula na mazao mengine ya biashara kwa ajili ya masoko yao.
Kasi ya kununua maeneo makubwa ya ardhi hapa nchini imeongezeka katika miaka ya karibuni kutokana na kupanda kwa bei ya chakula ulimwenguni inayosababishwa na ukame na mabadiliko ya tabia nchi na kutokuwepo kwa mikakati imara ya uwekezaji katika sekta hiyo, hali inaonekana kuwa mbaya zaidi.
Hata hivyo, Ally Keissy Mohammed, Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), anaonya kwamba ardhi haikui, hivyo serikali haipaswi kuiuza kwa wageni kwa sababu wananchi pia wanaihitaji.
“Tulipopata uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita tulikuwa watu milioni tisa tu, lakini sasa tuko zaidi ya milioni 45. Tunaweza kulima wenyewe na hakuna haja ya kuwauzia ama kuwakodisha wageni. Kuna hifadhi za taifa nyingi ambazo zimechukua maeneo makubwa ya ardhi. Mahali pengine ardhi haina rutuba kwa kilimo, wakulima wetu waende wapi? Viongozi wetu lazima walielewe hili,” anasema mbunge huyo.
Anaonya kwamba katika miaka 10 au 15 ijayo migogoro ya ardhi inaweza kuwa mikubwa kuliko ilivyo sasa baina ya wananchi na wawekezaji kama ilivyotokea Kenya wakati wa Mau Mau au hata hali iliyotokea Zimbabwe.
“Tazama mauaji yanayoendelea kati ya wakulima na wafugaji huko Mvomero, Kilosa na Kiteto wakigombea ardhi. Idadi ya watu nchini Tanzania inakua kwa kati ya asilimia 2.5 hadi 4.2. Sasa huu uwekezaji wa wageni utaleta vita kwa sababu Watanzania hawatakubali kuwa watwana katika nchi yao. Wakulima wote watavamia mashamba ya wawekezaji kama inavyotokea kwenye migodi ya madini.”
Anaongeza kwamba, Tanzania ina ng’ombe, kondoo na mbuzi wengi na haina mahali pa kuuza hivyo kuitaka serikali kutengeneza mazingira mazuri kwa wakulima na wafugaji ili waweze kuendeleza shughuli zao kwa uhuru na amani.
Kwa upande wake, Basil Mwanakambe, mtumishi wa umma, anasema uwekezaji wa wageni katika kilimo unapaswa kujikita katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa za kilimo pamoja na kuweka masoko ya uhakika kwa bidhaa hizo ili kuongeza mnyororo wa thamani na kuwapa tija wakulima wazalishe kwa wingi.
Anasema wakulima wa Tanzania hawana masoko ya uhakika kwa mazao yao, hivyo ni wakati muafaka kwa wawekezaji kuangalia sekta ya viwanda na masoko na kuwaacha wananchi wazalishe wenyewe ili kupanua wigo wa masoko na kuongeza bei.
“Uzoefu unaonyesha kwamba bei zinapanda na kushuka kila mwaka na kila msimu. Bei zinapokuwa hazieleweki, mipango inakuwa changamoto kubwa kwa wakulima wadogo wasio na mitaji. Mwanzoni mwa msimu wakulima hawajui wategemee nini kwenye bei ingawa wanatumia gharama kubwa, hali ya hewa inapobadilika na mvua kushindwa kunyesha inaleta majanga makubwa kwa wakulima ambaye ni muhanga wa majanga yote,” anasema
Kwa kutazama kundi hili la wakulima linalounda asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania wote, inaonekana wazi kwamba Sera za Kilimo la Mifugo hazijaweza kufikiwa kwa sababu hata uhakika wa usalama wa chakula nao umekuwa tatizo sugu.
Uboreshaji wa hali ya maisha ya wananchi wa vijijini kupitia kilimo na mifugo, viwanda na masoko haujaweza kufikiwa kwa sababu wakulima hawajapewa msaada wa kutosha kutoka serikalini na hata taasisi nyingine, hususan za fedha. Mipango mingi ya serikali imeendelea kubakia kwenye makaratasi na wakati huo huo wanawalaumu wakulima kwa kushindwa kuzalisha kiasi cha kutosha kwa chakula na ziada ya kuuza.
“Kushindwa kwa Tanzania kufanya vizuri kwenye kilimo kunatokana na makosa ya kisera. Sera nyingi haziakisi hali halisi ya mazingira yetu na hata wananchi wetu. Sera kwa asilimia kubwa zinapaswa kuchochea tabia. Kwa hiyo ni vigumu kuona ni kwa namna gani mkulima huyu mdogo anaweza kunufaika na sera hizo. Sasa kama utawakaribisha wawekezaji wajikite kwenye kilimo kwa sababu wana mtaji mkubwa kuliko wazawa, lazima watawafunika wakulima wetu na matokeo yake Watanzania wataendelea kuogelea kwenye dimbwi la umaskini. Serikali inapaswa kuwawezesha wakulima wa ndani,” anafafanua Mwanakambe.
Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), anaonya kwamba uwekezaji wa wageni unaweza kuleta machafuko mbele ya safari kwa sababu wawekezaji wageni wanakimbilia kujitwalia maeneo makubwa ya ardhi yenye rutuba na kuwaacha wananchi wa kawaida wakiendelea kuhangaika na jembo la mkono.
Lissu, mwanasheria na mwanaharakati, anasema kama serikali ina dhamira ya kuwakomboa wananchi kutoka katika umaskini, lazima ifikirie kuwawezesha kwa kuwapa elimu na mitaji badala ya kuendelea kuwaalika wageni waje wawekeze kwenye kilimo.
“Nchi zinazoendelea kama Tanzania hazihitaji misaada. Tunahitaji wawekezaji wengi makini lakini siyo wageni. Wawekezaji wazawa wanapaswa kupatiwa fursa kama kweli tunataka kulinusuru taifa letu. Mambo yote yanatakiwa kufanyika kwa uwazi,” anasema.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni 900 wanatoka katika nchi zinazoendelea kama Tanzania, lakini nusu yao wanaishi kwa kipato cha chini ya dola mbili kwa siku, na kwa muongo uliopita, asilimia 60 ya wakimbizi wote duniani wametokea kwenye nchi hizo.

0656-331974


No comments:

Post a Comment