Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Tuesday 8 September 2015

WADAU WA MBOLEA NCHINI WATAKIWA KUJADILI CHANGAMOTO

Mgeni Rasmi Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Misaada ya Maendeleo na Mashirikiano ya Kimataifa ambaye pia ni Mchumi Mkuu Bi. Magret Ndaba akitoa hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa wadau wa sekta ya mbolea nchini kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bibi Sophia Kaduma leo jijini Dar es salaam.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wadau wa sekta ya mbolea nchini wakifuatilia mkutano wa wadau hao ulifanyika leo jiji Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Misaada ya Maendeleo na Mashirikiano ya Kimataifa ambaye pia ni Mchumi Mkuu Bi. Magret Ndaba akiwawa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa wadau wa sekta ya mbolea nchini mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo leo jijini Dar es salaam.
(Picha na Eleuteri Mangi- MAELEZO)


Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
8/9/2015.
Wadau wa sekta ya mbolea nchini wameaswa kujadiliana kwa kina changamoto zinazoikumba sekta hiyo na kuzipatia ufumbuzi ili kuinua sekta ya kilimo iwe na tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Misaada ya Maendeleo na Mashirikiano ya Kimataifa ambaye pia ni Mchumi Mkuu Bi. Magret Ndaba wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa sekta ya mbolea nchini kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bibi Sophia Kaduma leo jijini Dar es salaam.
 “Unajua mbolea kazi yake ni kurutubisha udongo, ni vema iwafikie wakulima ambao ni walengwa kwa wakati na kwa bei nafuu” alisema Bi. Magret.
Bi. Magret alisema kuwa washiriki wa mkutano huo wajikite kujadili vitu vinavyokinza utumiaji wa mbolea kumfikia mkulima waviibue na wajadili kwa pamoja kwa kushirikiana Serikali na sekta binafsi lengo likiwa ni mbolea kuwafikia wakulima kwa wakati na kwa bei nafuu ili kilimo kiwe cha tija kwa wakulima na  taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na masuala ya mbolea (AFAP) Dkt. Andrew Msolla alisema kuwa mkutano huo ni wa kwanza kufanyika hapa nchini kwa kuwashirikisha wadau wa sekta hiyo ya mbolea.
Dkt. Msolla alisema kuwa Azimio la Abuja nchini Nigeria lililowekwa mwaka 2006 lilizitaka nchi zote za Afrika kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwa hekta ambapo inatakiwa kuwa ni kilogram 50 kwa hekta moja.
“Mwaka 2006 matumizi ya mbolea kwa nchi za Afrika yalikuwa ni kilogram 8 kwa hekta ambapo hadi sasa Tanzania inatumia kilogram 19.6 ambazo ni chini ya makubaliano ndiyo maana hasa ya mkutano wetu wa leo” alisema Dkt. Msolla.
Naye Mkuu wa Shirikisho la Mapinduzi ya Kijani katika Kilimo Afrika (AGRA) nchini Tanzania Dkt. Mary Mgonja alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi sita za kipaumbele katika mapinduzi ya kijani kati ya 17 za Afrika zilizo katika shirikisho hilo.
Kwa mujibu wa Dkt. Mary, nchi nyingine za kipaumbele katika shirikisho hilo ni Msumbiji, Ethiopia, kwa ukanda wa Afrika ya Mashariki pamoja na Ghana, Burkina Faso na Mali kwa ukanda wa Afrika ya Magharibi.
Akichanganua changamoto zinazoikabili sekta ya mbolea nchini, Meneja Mkuu wa Chama cha Makampuni yanayoingiza mbolea nchini Bw. Salum Mkumba alisema kuwa zipo changamoto kuu sita zinazoikabili sekta hiyo nchini.
Changamoto hizo ni uwepo wa taasisi nyingi za udhibiti wa mbolea, namna ya usajili wa mbolea ambapo ili isajiliwe ni lazima ifanyiwe majaribio kwa muda wa miaka mitatu, mfumo wa ruzuku ya mbolea ambao hubadilika mara kwa mara na kuathiri wakulima, suala la namna ya kusafirisha mbolea ambapo hutumika magari badala ya reli pamoja na mikopo kwa wakulima yenye riba kubwa.
Bw. Salum Mkumba alisema kuwa mkutano huo umeazimia kutatua changamoto hizo zinazoikabili sekta ya mbolea kwa kushirikisha sekta binafsi na Serikali kwa kuweka sheria, kanuni na taratibu ambazo zitamsaidia mkulima mdogo na hatimaye kuwa na tija kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
 Mkutano huo wa siku moja ulikuwa na washiriki zaidi ya 70 kutoka sehemu mbalimbali nchini ukijumuisha wahadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine kilichopo Mkoani Morogoro na Chuo Kikuu cha Dar es salaam, sekta binafsi zinazoshughulika na masuala ya mbolea, wahisani na wadau wa maendeleo kutoka nchi mbalimbali pamoja na wakulima.

No comments:

Post a Comment