Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 3 September 2015

UKWELI WA MWANASIASA NI JINA LAKE TU



Na Daniel Mbega
KAMA ni shule ya sanaa, basi wanasiasa wawili waliopata kuwa mawaziri wakuu – Edward Lowassa na Frederick Sumaye – wamefuzu vya kutosha. Bora Lowassa tunajua alisomea sanaa, lakini Sumaye alisomea kilimo!
Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, wanasiasa hao ambao wamejitoa Chama cha Mapinduzi na kwenda Chadema kuliko na mwavuli wa Ukawa, wametamka mambo ambayo binafsi yamenichanganya.
Kwa nyakati tofauti wamesimama kwenye majukwaa na kuikandia Serikali ya Awamu ya Nne kwamba haifai, lakini wenyewe kwa wenyewe pia wamesahau kauli zao za nyuma walizopata kuzitoa.
Huko nyuma, Lowassa – ambaye ni mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ukawa – alipata kumsifu Rais Jakaya Kikwete akisema: “Rais Kikwete ni Visionary Leader ana uwezo wa kuona mbali”.
Hata hivyo, baada ya kuianza upya ‘safari ya matumaini’ akiwa Ukawa, amesahahu maneno hayo na sasa anasema: “Rafiki yangu Jakaya Mrisho Kikwete ameuharibu uchumi wan chi hii”.
Yako mengi aliyowahi kuyasema akiwa ndani ya CCM ikiwemo kuapa kwamba asingetoka ndani ya chama hicho na ikiwa kuna mtu hamtaki, basi aondoke yeye.
Hata ukienda leo Maktaba na kupitia vichwa vya habari kwenye magazeti mbalimbali kuanzia mwaka 2007 hadi sasa, hakika utachanganyikiwa.
Na utachanganyikiwa zaidi wakati utakapolinganisha kauli za wanasiasa kwa wakati huo mpaka sasa, kuona kama zinawiana.
Tatizo kubwa ni kwamba, kwa Lowassa hata useme vipi hakuna anayekusikiliza, wanaomshabikia wanakuona wewe ndiye ‘boya’. Wamesahau kila kitu na wanachoangalia ni namna ya kuingia Ikulu tu. Wote waliomsema wamefumba macho kwa makusudi, hata kama wanaujua ukweli, kwa sababu wanaamini kukumbusha ufisadi wa Lowassa ni kujiwekea vikwazo vya kuingia Magogoni.

Sumaye ndiye amenishangaza kabisa na nitaendelea kumshangaa daima katika maisha yangu. Nachelea kusema wanasiasa ni waongo, lakini nasikitika kusema ukweli wa mwanasiasa ni jina lake tu, mengine yote mbwembwe na uongo mwingi!
Amesahau kwamba Juni 2, 2008 alinukuliwa na gazeti la Tanzania Daima akisema “Urais basi”, kwamba hakuwa na nia ya kuwania tena nafasi ya urais hata itakapofika mwaka 2015, na badala yake anataka kuwa mtu wa msaada kwa nchi za Afrika, ili ziweze kujikwamua katika lindi la umaskini. Maneno haya aliyasema kwenye mkutano na waandishi wa habari pale kwenye Hoteli ya Protea, zamani Court Yard, jijini Dar es Salaam.
Lakini ghafla bin vuu akajitokeza kuwa miongoni mwamakada 42 wa CCM waliojitokeza kutaka kupokea kijiti cha Jakaya Kikwete. Wakati akiwa na harakati za kuwania urais, alipata kukaririwa akisema: “Endapo CCM itampitisha Lowassa kugombea urais mimi nitahama chama.” CCM haikumpitisha Lowassa, wala yeye hakupitishwa. Akabakia huko kwa muda na baada ya kutafakari akahama kumfuata Lowassa Chadema! Tena basi ameteuliwa kuwa Meneja wa Kampeni wa mtu aliyedai hafai kuwa rais akiwa CCM. Amesahau aliyoyasema na daima nawakumbusha tu wanasiasa, Ukiwa mwongo usiwe msahaulifu!
Baada ya kwenda Chadema, Sumaye huyo huyo katika uzinduzi wa kitaifa wa kampeni za Ukawa, ndiye aliyempigia kampeni Lowassa akisema: “Lowassa anastahili urais yeye ndiye Jemedari wetu”.
Alimpamba kwa maneno mengi mno, lakini akasahau maneno yake aliyopata kuyasema huko nyuma, ikiwemo kulalamika kuhusu rushwa na ufisadi kiasi cha yeye kushindwa hata kuchaguliwa kwenye ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) mwaka 2012 kupitia Wilaya ya Hanang’.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari Oktoba 7, 2012 aliouitisha mahususi kueleza yaliyojiri katika uchaguzi wa mjumbe wa NEC Wilaya ya Hanang’, mkoani Manyara, uliofanyika Septemba 29, 2012 alieleza kuwa CCM inaandamwa na rushwa mpya aliyodai imetoka kwa mtu kuhonga ili achaguliwe katika eneo lake na sasa kuna rushwa za kimtandao.
Alisema rushwa za kimtandao ni zile ambazo mtu hutoa fedha katika maeneo mbalimbali nchini ili watakaochaguliwa wawe wafuasi wake mbele ya safari atakapowahitaji katika safari za ndoto zake za kuwania uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema rushwa hiyo ndiyo iliyotumika katika uchaguzi huo wa NEC Hanang', ambako aliyekuwa mpinzani wake mkubwa katika kinyang’anyiro hicho, Dk. Mary Nagu alimwangusha.
“Suala la rushwa katika nchi yetu na katika chama chetu siyo geni, lakini sasa nahisi tatizo hili sasa limeota mizizi na linazidi kuwa kubwa. Mimi binafsi nilizungumza tatizo hili mara kadhaa,” alisema Sumaye. “…Katika uchaguzi wa kidemokrasia wapiga kura humchagua mwakilishi wanayemtaka kwa sababu ya uwezo wake, yaani humchagua mwakilishi wao kwa ajili yao. Katika demokrasia iliyopondeka kwa rushwa, fedha huwachagulia watu mwakilishi kwa ajili ya waliotoa fedha. Wapiga kura ni wapiga mihuri tu,” alisema Sumaye na kuongeza: “Zamani kulikuwa na rushwa ya mtu kuwahonga watu fedha wa eneo fulani ili achaguliwe, lakini leo hii kuna rushwa ya kimtandao.”
Alisema watu wanaochaguliwa kwa utaratibu huo, utumishi na uaminifu wao siyo kwa wale waliopiga muhuri kuidhinisha zile kura alizopata, bali ni kwa fedha zilizonunua zile kura na hasa kwa aliyetoa au waliotoa fedha, hivyo Watanzania kuwa na wawakilishi wa mtu au watu na siyo wa umma.
Nakubaliana naye kwa hoja ya CCM kukumbwa na wimbi la rushwa, lakini napingana naye anaposema zamani kulikuwa na rushwa ya mtu mmoja mmoja lakini sasa kuna rushwa ya kimtandao.
Hivi kumbe hata wakati wake alikuwa anaiona hiyo rushwa ya mtu mmoja mmoja lakini akaisamehe? Ameamua kupiga kelele kwa sababu alikosa ushindi kwa nguvu ya mtandao kama ule wa Urais 2005?
Sumaye ananishangaza sana: Hivi miaka yote ambayo amekuwa kada wa chama mpaka kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi serikalini hakuwahi kuiona rushwa hiyo? Nini hasa kilichomshtua sasa kiasi cha kuamua kutoa matamko mfululizo kuipinga rushwa hiyo?
Ninavyojua, Sumaye amesomea Stashahada ya Uhandisi katika Kilimo kati ya mwaka 1970 hadi 1972 pale Egerton Agricultural College, Kenya (sasa Chuo Kikuu cha Egerton) baadaye akajiendeleza na kupata Stashahada ya Juu. Amekuwa mwalimu wa Kilimo Nyegezi, amekuwa meneja wa idara na mhandisi wa karakana katika Kiwanda cha Sukari Kilombero, amekuwa mkuu wa idara katika kiwanda cha Nishati Vijijini cha Camartec pale Arusha na kadhalika kabla ya kuwa naibu waziri wa kilimo na ushirika kuanzia mwaka 1985 hadi 1994 na baadaye akawa waziri kamili wa kilimo na ushirika mwaka 1994 na 1995.
Leo asema alifanya kitu gani kuboresha kilimo? Atueleze ilikuwaje yale mashamba ya Ranchi za Taifa (Narco), mashamba ya kilimo (Nafco) na mashamba ya ng’ombe wa maziwa (Dafco) yamekwenda wapi?
Migogoro inayoendelea kule Kapunga, Mbarali na hata Mvomero anaifahamu siri yake, aje atueleze basi ni kwanini shamba la Kapunga (Nafco) lililotumia mamilioni ya fedha lilidumu kwa miaka miwili tu kabla ya kuanza kutafunwa na wajanja, tena wengi wao kutoka wizarani yeye akiwa waziri mwenye dhamana ya kilimo. Historia haidanganyi hata kidogo.
Sumaye ndiye Mtanzania pekee kuwa Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo, tena basi ni miaka 10, mwezi mmoja na siku tatu (Novemba 27, 1995 hadi Desemba 30, 2005). Ni rekodi nzuri na ya kujivunia, kwani tangu tupate Uhuru mwaka 1961, hakuna waziri mkuu aliyepata kuongoza kwa kipindi chote hicho MFULULIZO.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwanza alikuwa Waziri Kiongozi kwa miezi tisa tu (Septemba 2, 1960 hadi Mei Mosi, 1961) wakati wa utawala wa Mwingereza, halafu akawa Waziri Mkuu kwa miezi nane na siku 22 (Mei Mosi, 1961 hadi Januari 22, 1962) baada ya kupata Uhuru kabla ya kumpisha Rashid Mfaume Kawawa ambaye alidumu kwenye nafasi hiyo hadi Desemba 9, 1962 siku Tanganyika ilipokuwa Jamhuri na nafasi hiyo ikaondolewa.
Baada ya nafasi hiyo kurudishwa tena Februari 17, 1972, Kawawa akarudishwa na kushikilia hadi Februari 13, 1977 (takriban miaka saba) akampisha Edward Moringe Sokoine ambaye aliongoza kwa vipindi viwili -  Februari 13, 1977 – Novemba 7, 1980, na Februari 24, 1983 – Aprili 12, 1984 mauti yalipomkuta  - alikaa kwa miaka 4 na miezi 9 na siku 19!
Cleopa David Msuya naye alikaa kwa vipindi viwili – Novemba 7, 1980 – Februari 24, 1983, na Desemba 7, 1994 – Novemba 28, 1995 baada ya uchaguzi mkuu – miaka 3 miezi 3 na siku 8! Dk. Salim Ahmed Salim yeye alikaa kwa mwaka mmoja na miezi sita na siku 11 (Aprili 24, 1984 – Novemba 5, 1985 baada ya uchaguzi mkuu). Joseph Sinde Warioba alikaa kwa miaka mitano na siku nne (Novemba 5, 1985 – Novemba 9, 1990) akampisha Cigwiyemisi John Samuel Malecela aliyedumu kwa miaka minne na siku 28, yaani Novemba 9, 1990 hadi Desemba 7, 1994!
Edward Lowassa alikaa kwa miaka miwili na mwezi mmoja na siku 8 tu (Desemba 30, 2005 – Februari 7, 2008) kabla ya kulazimishwa kujiuzulu na kumpisha Mizengo Kayanza Peter Pinda, ambaye bado yuko madarakani!
Kwa hiyo ukitazama kwa makini utaona kwamba, Sumaye ndiye pekee ambaye amekaa pale Magogoni kwa miaka mingi zaidi, tuseme kwa kipindi chote cha awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa – waliingia wote wakatoka wote!
Katika masuala ya utawala, rekodi kama hii ni ya kujivunia kabisa japokuwa ina sura mbili: Kwanza, inawezekana utendaji wake ulikuwa mzuri, akatimiza wajibu wake ipasavyo. Lakini, Pili, yawezekana alikuwa ‘anaiva’ na kuaminiwa na Rais mwenyewe katika nafasi hiyo, vinginevyo angeweza hata akabadilishwa katika nafasi nyingine ya uwaziri kama tulivyoshuhudia kwa Mzee Kawawa na wengineo.
Najiuliza tu, inawezekana Sumaye ameamua kuibamiza Serikali ya Awamu ya Nne kwa sababu ilimsahau hata kumpa ubalozi? Hili linawezekana, pengine.
Sumaye, katika kipindi chake, tulishuhudia sheria nyingi za ajabu ajabu zilizoihalalisha rushwa kwa majina mbalimbali, ikiwemo ile Sheria ya Takrima. Aseme leo kama yeye mwenyewe hakuwahi kutoa takrima, tena aseme kama hakuwahi kupewa takrima!
Lakini ni Sumaye huyu huyu ambaye wakati inapitishwa sheria hiyo Bungeni mwaka 2000 chini ya Spika Pius Msekwa, yeye alikuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Leo hii ndipo anakumbuka kwamba kumbe rushwa haifai hata kama ikiwa imebatizwa majina mengine.
Sumaye alikuwa mtendaji mkuu wa Serikali wakati wamiliki wa vyombo vya usafiri walipolazimishwa kufunga Speed Governor eti kupunguza ajali. Watu wakapiga dili wakatokomea, ajali zikawa pale pale.
Sumaye alikuwa mtendaji mkuu wa Serikali wakati Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma iliposhika kasi na wakuu wa nchi  wakajigawia mashirika wapendavyo. (Rejea mgodi wa Kiwira).
Sumaye alikuwa mtendaji mkuu wa Serikali wakati mikataba mibovu iliposainiwa: mkataba wa IPTL ambao ndio uliozaa akaunti ya Escrow anayoisema; mikataba ya Songas, Meremeta, Mwananchi Gold; uuzwaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC); ukodishwaji wa Shirika la Ndege (ATC) na Shirika la Umeme (Tanesco) kwa Makaburu; ununuzi wa Radar ambayo kama si huruma ya Waingereza ‘kuomboleza kwa niaba yetu’ hata chenji tusingeweza kupata; ununuzi wa Ndege ya Rais ambapo waziri wa fedha wakati huo Basil Mramba alisema hata Watanzania wakila nyasi, lazima ndege inunuliwe.
Sumaye alikuwepo serikalini wakati dili la kuchota fedha kutoka kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA) kwenye Benki Kuu linapigwa na ndipo ulipozaliwa ‘Mtandao’ ndani ya CCM uliokifanya chama hicho kiwe jinsi kilivyo sasa huku Lowassa ‘akishangaa’ na Sumaye akilalamika.
Najaribu kutoa ushauri – siyo kwamba naunga mkono vitendo vya rushwa, bali Mzee Sumaye angeweza kutulia kuliko kunyoosha kidole CCM ambayo mwenyewe alikuwemo. Kwangu mimi, sidhani kama anastahili kutamka anayoyatamka sasa wakati yeye alikuwa miongoni mwao na hakuweza kujitoa kipindi kile kasubiri mpaka sasa.

Mtu mwingine anayenishangaza ni Joseph Mungai, ambaye Jumapili Agosti 30, 2015 aliibuka kwenye jukwaa la Ukawa pale Mafinga na kumnadi mwanaye William.
Mungai of all people, ambaye aliiparaganya elimu ya Tanzania wakati akiwa waziri kwa kuondoa hata michezo, leo hii ana ujasiri wa kutosha kuinyooshea kidole CCM, ambayo kama isingekuwa kesi ya rushwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 huenda angekuwa kwenye duru za siasa akiendelea kuinadi.
Mungai alipata kumpinga Lowassa kuhusu kauli kwamba ndiye aliyeleta shule za Kata akisema: “Lowassa ana mawazo mgando na akili ya kusahau, shule za Kata zilijengwa na wananchi chini ya Mkapa.” Lakini alipopanda jukwaani pale Mafinga akasema: “Kwa sababu mwanangu anagombea kupitia Ukawa, Lowassa anastahili urais.”
Siyo wakati wa kumchambua mzee huyu, lakini utakapofika nitatoa maoni yangu kama Mtanzania, vinginevyo ningemshauri atulie kama alivyokuwa ametulia tu.
Ni ushauri tu, na haya ni maoni yangu tu.

0656-331974

No comments:

Post a Comment