Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 16 September 2015

UFUGAJI ASILI, KILIMO VYAATHIRI ELIMU SIKONGE

Displaying SAM_0012.JPG
Moja mkokoteni wa kusukumwa na Ng`mbe ambapo watoto mara nyingi hawaendi shule na kulazimika kusoma mchanga,tofali za kuchoma, mkaa au Tumbaku ambayo imevunwa tayari kwa kukaushwa.Picha zote na Hastin Liumba.

Na Hastin Liumba, Sikonge
KUMTUMIKISHA  mtoto mdogo ni dhambi kubwa kwa sababu inamnyima  haki zake za msingi kama vile; kusoma, kupendwa, kushirikishwa, kuabudu, kuheshimiwa na kutoa maamuzi.

Sheria ya Haki za Watoto Na. 21 ya 2009 kifungu 78 (1) inakataza mtu yeyote kuajiri/  kuwatumikisha watoto katika shughuli yeyote ile ambayo inawadhalilisha au kuwanyima haki za msingi.

Akizungumzia hali ya utumikishwaji watoto wilayani Sikonge kwa mwandishi wa makala hii, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Shadrack Mhagama anasema vitendo vya kutumikisha watoto hufanyika katika ngazi ya familia, jamii na katika sekta za uzalishaji hususani kule vijijini, vitendo ambavyo vimekithiri wilayani humo.

Mhagama anasema kutumikisha watoto kunapelekea watoto kupata madhara mengi  ikiwemo kuacha shule, mimba za utotoni, kuolewa mapema, kuumia au kupoteza malengo yao ya baadae jambo ambalo husababisha umaskini katika taifa.

Mkurugenzi anataja sababu zinazochochea utumikishwaji watoto katika kilimo na mifugo kuwa ni hali ya umasikini inayowakabili wazazi walio wengi katika ngazi ya familia na kaya na ukosefu wa elimu kwa wazazi husika tatizo ambalo linazidi kuwa kubwa siku hadi siku hasa katika jamii ya wakulima na wafugaji.

Mhagama anabainisha kuwa utumikishwaji watoto upo na unafanywa na wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali hasa kule vijijini katika kilimo cha tumbaku na kuchunga mifugo hususani ng’ombe.

Anaongeza kuwa sasa hivi baadhi ya wazazi hawatumikishi watoto wao sanakatika kilimocha tumbaku ila wanawatumikisha katika kazi za kuchunga mifugo ama ujira mdogo au bila ujira.

‘Vitendo vya utumikishwaji watoto hufanywa na wakulima na wafugaji hasa wa jamii ya wasukuma ambao huishi kwa kuhama hama toka sehemu moja kwenda nyingine wakitafuta eneo linalowafaa kwa malisho na kwa shughuli za kilimo na ufugaji na wakishaliona huamua kuvamia na kuanzisha makazi mapya’, alisema.

Mhagama anafafanua kuwa wamejitahidi sana kujenga shule katika makazi (vijiji) ambavyo  havina shule au shule iliyopo iko umbali mrefu  toka kijiji kimoja hadi kingine, lakini tatizo lililopo hawa watu kila wakati wanaanzisha makazi mapya sehemu yoyote ile hususani maeneo ya porini ambapo huamua kuishi wakiwa na familia zao, ndugu, jamaa na marafiki zao.

‘Tukiwajengea shule katika maeneo hayo baadae wanahama tena na mifugo yao kuelekea sehemu nyingine hata kama watoto wao walikuwa wameanza shule ya msingi au sekondari’, aliongeza.

Athari za Utumikishwaji watoto:Kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi huyo Akionyesha kusikitishwa na vitendo hivyo Mhagama anaeleza kuwa watoto walio wengi hususani wale ambao wameshazoea kufanyishwa kazi za kilimo au za kuchunga ng’ombe hawasomi shule kabisa, hata wakiandikishwa hawaripoti, la, wakiripoti hawamalizi shule.

 ‘Hata ukikutana nao mitaani ukawauliza, ninyi mnasoma shule, watakwambia hatusomi na wataanza kuongea kisukuma tu, kwa kweli tunatengeneza taifa la watu mbumbumbu, wasiojua kusoma na kuandika kwani idadi yao inazidi kuongezeka’, aliongeza.

Mhagama anaeleza wazi kuwa utumikishwaji watoto hurudisha nyuma maendeleo katika eneo fulani hasa kijamii, kielimu na kiuchumi.

Aidha anasema maeneo yote yanayokaliwa na jamii hii ambayo hutumikisha watoto katika shughuli za kilimo na mifugo kwa kisingizio cha umaskini, mbali na kukosa elimu, jamii hiyo pia imeathiriwa na imani za kishirikiana tabia ambazo hurithishwa kwa watoto hao, imani za namna hii humdidimiza zaidi mtoto huyo.

Athari zinazochangiwa na wazazi kwa kuwa na mtizamo hasi kielimuAnasema wazazi wenye mtizamo hasi kielimu na kuendeleza vitendo vya utumikishwaji watoto huathiri zoezi zima la uandikishaji watoto wa kuanza shule hali inayochangiwa na wazazi hao kutowasukuma watoto wao kwenda shule.

Mtizamo hasi kielimu huchangia utoro wa wanafunzi shuleni ikiwemo kutochangia maendeleo ya shule hususani katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na matundu ya vyoo sambamba na kuongezeka kwa vitendo vya uhasama na uvamizi wa maeneo ya shule kwa ajili ya kilimo au shughuli nyinginezo.

Miradi mingi ya shule kubakia viporo kwa kukosa michango ya wazazi sambamba na kutochangia mahitaji mengine muhimu kama vile chakula cha mchana kwa watoto shuleni, ukosefu wa chombo madhubuti cha usafiri.

Athari nyingine ni matokeo duni ya wanafunzi darasani, mwamko mdogo wa baadhi ya wazazi au walezi na jamii, migongano kati ya shule na jamii ambayo huhatarisha usalama wa walimu na mali zao, wanafunzi wengi kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu, hali inayochangiwa na kuhamahama kwa jamii ya wafugaji na wananchi kuishi mbali na huduma ya elimu.

Athari nyingine ni baadhi ya walimu kutowajibika ipasavyo, utoro wa wanafunzi na baadhi ya walimu, upungufu wa nyumba za walimu unaosababisha walimu kusafiri umbali mrefu kila siku na kusababisha kutowajibika ipasavyo na wanafunzi kutokufanya mitihani yao ya mwisho ya kitaifa.

Athari nyingine ni baadhi ya wanasiasa kuingilia masuala ya kiutendaji katika utoaji wa elimu mfano wanafunzi watoro wanapofuatiliwa wazazi wao na watendaji wanatetewa

Upungufu wa vyumba vya madarasa.Anasema vitendo vya utumikishwaji watoto vimeshamiri sana katika maeneo mengi ya mkoa wa Tabora na wilaya zake zote.

Alisema kutokana na Shirika la kazi Duniani (ILO) taarifa ya hali ya utumikishwaji duniani ya mwaka 2006 (Integrated labour fource 2006), takwimu zinaonyesha kwamba takribani watoto milioni 2.5 wa umri kati ya  miaka  5-17 wanatumikishwa ambapo watoto milioni 2.3 wanatumikishwa vijijini na milioni 0.2 mijini.

Aidha utafiti wa awali uliofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Winrock International kupitia mradi wake wa PROSPER uliofanyika katika wilaya za Sikonge na Urambo mkoani Tabora mwaka 2012 ulionyesha kwamba asilimia 48.29 ya watoto wote waliosajiliwa katika shule za msingi wenye umri wa miaka 5-17 hutumikishwa ikiwa wavulana ni asilimia 49.77 na wasichana asilimia 46.69.

Anabainisha jitihada za kunusuru watoto hao wasiendelee kutumikishwa zimeendelea kufanyika na zoezi la uandikishaji watoto wa kuanza shule ya msingi limekuwa likifanyika ambapo zaidi ya asilimia 90-95 ya watoto wenye umri wa kuanza shule wamekuwa wakiandikishwa lakini ni asilimia 45 tu wanaobaki shuleni, jambo ambalo limeathiri hata  mahudhurio yao shuleni.

Kwa upande wa shule za sekondari hali iko hivyo hivyo, kwani takwimu za mwaka jana pekee zinaonyesha kwamba katika matokeo ya kidato cha nne kitaifa mkoa wa Tabora ulishika mkia huku wilaya ya Sikonge ikishika mkia kimkoa na shule nne za mwisho kitaifa zikitoka wilayani humo ambazo ni Mole, Mkolye, Mibono na Kamagi sekondari.

Aidha jitihada za wadau mbalimbali katika kutokomeza utumikishwaji huo; Mradi wa PROSPER unajitahidi sana kutoa mafunzo mbalimbali ya kilimo na ujasiriamali ili kuwawezesha vijana na akina mama kiuchumi lengo likiwa vikundi hivyo viwe chachu ya kuinua uchumi baina yao sambamba na kuboresha kipato cha familia zao.

Mradi huo pia umeweza kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi zaidi ya 10 vya akina mama katika wilaya za Urambo na Sikonge ili kuimarisha biashara zao waweze kusaidia watoto wao wasiosoma shule kwa kuwalipia ada, sare za shule na mahitaji mengine ya shule na ya familia zao.

Alisema mradi huo na wadau wengineo pia wamesaidia sana kuhamasisha uandikishaji watoto wapya shuleni sambamba na kugharamia mahitaji yao ya shule na kuhakikisha watoto waliofikia umri wa kufanya kazi ndiyo wanaofanya kazi tu, katika mkakati huu wa mwanzo walengwa waliofikiwa ni robo tu ya walengwa wote.

Nini kifanyike;Mkurugenzi huyo anasema licha ya watoto na wazazi wanakoelekea hakueleweki hata kama watawekewa mazingira mazuri ya kielimu kutokana na umaskini unaowakabili, bado suala la elimu ni la muhimu, kinachotakiwa ni  kuwaelimisha wazazi umuhimu wa kupeleka watoto shule na kuwashawishi ili kubadilika na kuacha mila, desturi, kwa wafugaji wakubali kuachana na ufugaji wa kuhamahama.

Aidha jitihada zote zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na halmashauri ya wilaya hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile mradi wa PROSPER katika kutokomeza vitendo vyovyote vinavyochochea utumikishwaji watoto katika kilimo na ufugaji zinapaswa kuungwa mkono na wadau wote.

Kwa mujibu wa maelezo ya mkurugenzi wa halmashauri, tayari serikali ya wilaya hiyo imeandaa mkakati maalumu wa kutambua na kuwakamata wazazi wote watakaowazuia watoto wao kwenda shule ili kulinda maslahi na hatma ya kizazi cha watoto hao sambamba na kudhibiti ufugaji wa kuhama kwa kuanza kutenga vijiji maalumu kwa ajili ya wafugaji.
hastinliumba@gmail.com.0788390788

No comments:

Post a Comment