Mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe, lakini mtaji wa tajiri ni jasho la maskini!
Na Daniel Mbega
“Siku zote tajiri ndiye atakayeamua huyu alipwe
mshahara kiasi gani, huyu apate kiasi gani. Na itaendelea kuwa hivyo mpaka
wafanyakazi tena wamgomee, waje juu waseme; “Wewe siyo tajiri mzuri!” Sijui
kama kuna tajiri mzuri na tajiri mbaya, na hivyo nawaambieni kwamba hakuna
tajiri mzuri, tajiri wote ni wezi!”
Hii ni
sehemu ya hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere akihutubia wafanyakazi katika
sherehe za Mei Mosi. Sikumbuki ni lini.
Hata
hivyo, maneno haya yamenifanya nitafakari sana mambo yanayoendelea katika siasa
za nchi yetu, hususan za vyama vingi, tangu mfumo huo ulipoanza Julai Mosi,
1992.
Nakumbuka
mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi kulikuwa na
wagombea urais wanne. Kila mgombea alikuja na kauli mbiu yake: Benjamin Mkapa
wa CCM alikuja na kauli mbiu ya ‘Ukweli na Uwazi’; Profesa Ibrahim Lipumba wa
CUF (Haki Sawa Kwa Wote); Augustine Mrema wa NCCR (Mageuzi); na John Cheyo wa
UDP (Kuwajaza Wananchi Mapesa) kauli mbiu ambayo ilimfanya apachikwe jina la
‘Bwana Mapesa’.
Ni kauli
mbiu ya Cheyo ya ‘kuwajaza watu mapesa’ ambayo ilikuwa imewavutia wananchi
wengi na kumpatia umaarufu mkubwa kiasi kwamba wananchi wa kawaida walihisi
huyo ndiye mkombozi wao.
Pengine
kwa sababu tu hakuwahi kuchaguliwa ndiyo maana ‘mapesa’ hayo hayakuweza
kupatikana, lakini Cheyo kwa miaka 10 aliyokaa Bungeni tangu mwaka 2005 hadi
2015 ameshindwa hata kuwajaza mapesa wananchi wa Jimbo la Bariadi Mashariki
(sasa Itilima).
Kauli ya Cheyo
haina tofauti na ile ya mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Mimi si mwanasiasa, ingawa ninapenda siasa. Hakuna mwanasiasa
anayependa siasa, wote wanapenda madaraka! Najaribu tu kuchambua kwa kutumia
taaluma yangu.
Tangu
alipotangaza nia yake ya kuwania urais kupitia CCM, kauli kubwa ya Lowassa imekuwa
kuuchukia umaskini na kutamani kila Mtanzania awe tajiri kama walivyo akina
Said Bakhressa, Reginald Mengi, Nazir Karamagi na wengineo, kwa kuwataja
wachache.
“I hate (nachukia) umaskini. Nataka
uongozi ili kuwaondoa Watanzania katika umaskini. Kama mtu amepata utajiri kwa
njia za uhalali, amejinyima, ni nzuri sana. Nachukia watu wanaopata fedha na
kuishia katika ulevi na wanawake. Kina mama mnisamehe. Sitaki kupata uongozi
kwa kudanganya, nachukia umaskini.”
Hata alipokwenda Chadema, Lowassa ameendelea kuinadi
Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa kurejea kauli yake ya kuuchukia umaskini.
Hili ni jambo jema sana kwa kiongozi, maana kwa kuuchukia kwake umaskini,
hawezi kuona jamii ikiwa maskini.
Hata hivyo, kauli hiyo inatia mashaka kutokana na ukweli
kwamba, hizo ni ndoto za mchana na maneno matamu ya wanasiasa ili tu wapate madaraka.
Lowassa ni mwanasiasa kama wanasiasa wengine, tena
amesomea sanaa za maonyesho (performing
arts) Chuo Kikuu. Tunafahamu wasanii ambavyo wanaweza wakafanya ‘accapela’
kwa kumwaga machozi hadharani hata kama hakuna cha kuwaliza!
Kama alivyosema Mwalimu Nyerere katika hotuba yake hiyo,
hakuna tajiri mzuri, tajiri wote ni wezi. Tena basi hakuna tajiri ambaye yuko
tayari kuona utajiri wake unatishiwa, atafanya kila njia kuulinda – kwa gharama
yoyote iwayo.
Matajiri wengi ni wanyonyaji wakubwa. Wanapenda
kuwafanyisha watu kazi ngumu kwa ujira mdogo, na ndiyo sababu ya kuanzishwa kwa
vyama vya wafanyakazi duniani ili kutetea na kudai maslahi bora zaidi kwa kazi
wanazozifanya.
Mwalimu Nyerere alikuwa muumini wa harakati za
wafanyakazi na wakulima. Alikuwa mjamaa, siasa ambayo wajanja waliizika kule
Zanzibar. Mwalimu alikuwa mpigania ukombozi wa binadamu. Alikuwa anapinga
dhuluma na ukandamizwaji. Ujamaa ni imani, ndivyo alivyoamini Mwalimu. Lakini ubepari
ni mfumo, si imani.
Matajiri wote, kwa kutafsiri kauli ya Mwalimu Nyerere, ni
mabepari na ili mfumo wa ubepari uendelee hakuna budi bepari ajilimbikize mtaji
unaotokana na ziada anayonyonya kutoka kwa wafanyakazi ambao ataendelea
kuwekeza ili aendelee kuwanyonya wavujajasho.
Viwango vya ubepari vinatofautiana kulingana na nchi
yenyewe. Viwango hivyo ni kama vifuatavyo:
Ubepari wa
uangalizi: Kwa Kifaransa inajulikana kama Laissez-faire. Huu ni mfumo
ambao masuala yote ya uchumi yako mikononi mwa sekta binafsi ambayo haiingiliwi
na serikali katika kupanga sheria, taratibu, vipaumbele, kodi na hata mgawanyo
wa mapato. Sekta binafsi
ndiyo inayosimamia mfumo wote na kazi ya serikali ni kuangalia tu.
Ubepari wa Ustawi
(Welfare capitalism): Ni utaratibu wa mabepari kutoa huduma za
kijamii kwa wafanyakazi wao na ulikuwa umeanzishwa kwa nchi za viwanda ambako
waliajiriwa watu wenye ujuzi tu. Mfumo huu ulikua zaidi katikati ya karne ya
20. Hapa Tanzania ni ndoto kwa mfumo huu kutumika kwa sababu viwanda vyote
vimekufa, mashirika ya umma yameuzwa, mabepari wenye viwanda nchini ndio
wanaoongoza kwa kulipa ujira mdogo kwa wafanyakazi, tena basi wanapenda zaidi
kuwa na vibarua, wenye elimu ndogo. Mtu yeyote mwenye ujuzi hawezi kuajiriwa
kwenye viwanda vya mabepari wa Tanzania kwa sababu wanaogopa kwamba hawa ni
wasomi, wanajua haki zao na wanaweza kuwasumbua baadaye.
Ubepari wa uswahiba
(Crony capitalism): Huu ni mfumo unaoelezea uchumi kwamba
kukua kwa biashara kunategemea urafiki wa karibu uliopo baina ya mabepari
(wafanyabiashara wakubwa) na viongozi walioko madarakani. Huu unaongozwa na
upendeleo zaidi wa maofisa wa serikali kwa mabepari hao ambapo hutoa vibali,
ruzuku za serikali, misamaha ya kodi pamoja na upendeleo mwingine. Mfumo huu
ndio unaotumika hapa nchini.
Ubepari wa Dola
(State capitalism): Ni mfumo wa uchumi ambamo shughuli zote
za biashara zenye tija zinasimamiwa na Dola, ambamo njia za uzalishaji mali
zinapangwa na kusimamiwa kama njia za biashara, zikiwemo za ukuzaji wa mitaji,
ujira kwa wafanyakazi, na usimamizi. Mfumo huu ni mgumu kutumika hapa Tanzania
kwa sababu serikali siyo mwajiri mkubwa tena kama ilivyokuwa zamani, bali sekta
binafsi ndiyo iliyoshika hatamu.
Lowassa anaposema anatamani Watanzania wawe matajiri
ananishangaza hasa katika kipindi hiki ambacho ubeberu umegeuzwa jina na kuitwa
‘Uliberali mamboleo’ (Neo-Liberalism)
au kwa lugha inayofahamika zaidi ni ‘Soko Huria’.
Kwa kuruhusu soko huria, serikali imelegeza masharti ya
biashara ya nje na ndani na sasa haiwezi kudhibiti tena biashara.
Wafanyabiashara wanajipangia wenyewe bei, serikali haipaswi kuingilia, na
madhara yake ndiyo ile migomo ya wafanyabiashara nchini ambayo inaendelea kwa
kupinga kodi na mashine za kielektroniki.
Gharama za maisha zimepanda kwa Watanzania siyo kwa
sababu serikali ni mbovu, ila ni kwa sababu ya soko huria. Kuilaumu moja kwa
moja serikali wakati mwingine tunafanya makosa makubwa, lazima tuangalie nini
chanzo.
Sekta za elimu, afya, maji na umeme zimebinafsishwa na sasa
zimekuwa bidhaa ambazo wananchi wanapaswa kuzilipia, na siyo huduma za jamii
tena zilizopaswa kutolewa bure.
Soko huria limeruhusu ujio wa wawekezaji kutoka nje na
ndani, yote haya yakiwa ni masharti ya wafadhili na taasisi za kibeberu. Serikali
imepoteza uwezo na haki yake ya kujiamulia mambo muhimu ya sera na mwelekeo wa
nchi kwa faida ya watu wake. Hii si Tanzania peke yake, bali nchi zote ambazo
zililazimishwa na mabepari hao ambapo hapa Tanzania Sera ya Ubinafsishaji
ilianzishwa mwaka 1992. Lowassa analielewa hili vyema kwa sababu alikuwa ndani
ya Baraza la Mawaziri, wakati huo akiwa na miaka 39!
Wakati wa utawala wa Mwalimu hakukuwepo na ufisadi,
japokuwa kweli rushwa ilikuwepo. Mwalimu aliipigia kelele rushwa.
Tumejifunza tangu shuleni na kama nilivyoeleza hapo
awali, ubepari ni mfumo wa uchumi ambamo biashara, viwanda na vitegauchumi
vingine vinatawaliwa na watu binafsi kwa kiasi kikubwa na kwa lengo la kupata
faida. Nafasi ya serikali ni ndogo, na vilevile lengo la kuhudumia jamii katika
mahitaji yake haliongozi mipango.
Kwa kuwa Tanzania imeingia katika soko huria ambalo
limeruhusu uliberali mamboleo ambao ndio ubepari wenyewe, pengine Lowassa
angetueleza anawezaje kuondoa tabaka la maskini na kuwafanya matajiri halafu
aseme ni kwa namna matajiri hao, akiwemo yeye mwenyewe, watakuwa salama.
Lowassa atueleze, kati ya viwango hivi vinne vya ubepari,
ni kipi ambacho atakitumia kuwaletea utajiri Watanzania, kwa sababu hakuna
ubishi kwamba yeye hawezi kuufuta ubepari kamwe na sifa za ubepari tunazijua.
0656-331974
NB: MAKALA HAYA YALICHAPWA KWA MARA YA KWANZA NA GAZETI LA MWANANCHI SEPTEMBA 16, 2015 INGAWA HAPA IMEREKEBISHWA KIDOGO.
No comments:
Post a Comment