Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 17 September 2015

DK. SLAA KAPASUA JIPU, KASHINDWA KULIKAMUA... KAKIMBIA!

Dk. Slaa

Na Daniel Mbega
WASWAHILI wanasema, ‘Msemea sikioni, siyo majinuni’! Maana yake ni kwamba, yeyote anayekunong’oneza kuhusu jambo fulani, katu siyo mjinga.
Septemba Mosi, 2015, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, aliibuka baada ya ukimya wa mwezi mmoja na kueleza msimamo wake katika siasa na mambo yaliyomfanya akimbie.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa muda wa saa 1:30 kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa, pamoja na mambo mengine, alieleza namna mchakato wa kumkaribisha Edward Lowassa ndani ya Chadema na hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulivyogubikwa na hila kutoka kwa viongozi wa chama chake.
Aliwatuhumu viongozi wake hao kuuchakachua mchakato na hata hoja alizozitoa, ikiwemo kupewa orodha ya watu ambao Lowassa aliokuwa anakwenda nao Chadema, ilizimwa huku Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari, akiichana barua yake ya kujiuzulu aliyomkabidhi.
Kubwa zaidi lililoleta mtikisiko ni maelezo ya Dk. Slaa kwamba, kumbe mchakato wote huo ulifanywa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, ambaye Slaa mwenyewe anamwita ‘mshenga’.
Alimnukuu Gwajima akimshawishi amkubali Lowassa kwa vile anakubalika na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kwamba maaskofu 30 kati ya 34 wa Kanisa Katoliki walikuwa wamelambishwa sukari guru na wanamkubali.
Hali hiyo ndiyo iliyozusha mtafakaruku mkubwa wa kisiasa ambao wapinzani waliuelezea kwamba una lengo la kuligawa taifa.
Slaa hakuwa majinuni alipotoa tuhuma hizo. Alikuwa sober, hakuwa amekunywa kileo wala hakuwa anaumwa, tena hakulazimishwa na yeyote… alimaanisha alichokuwa anakisema.
Hata hivyo, Septemba 8, 2015 Askofu Gwajima naye aliibuka kujibu mapigo ya tuhuma za Dk. Slaa, akisema kwamba Paroko huyo mstaafu wa Kanisa Katoliki hana hoja kwa sababu ‘ametekwa na mkewe’ ambaye alitamani sana kuwa ‘Mke Namba Moja wa Tanzania’ (First Lady).
Akasema, siku Lowassa alipopokelewa Chadema, Dk. Slaa alitupiwa nguo nje na mkewe na kwamba alilala kwenye gari huku kitendo hicho kikishuhudiwa na walinzi, ambao yeye Gwajima ndiye aliyempatia Slaa ingawa walikuwa wanalipwa na Chadema.
Gwajima ameruka futi 100 kwamba hajawahi kumweleza Dk. Slaa kwamba kuna maaskofu 30 waliohongwa, hivyo maneno hayo ni ya kutungwa.
“Dk Slaa anasingizia kuwa maaskofu 30 wamehongwa na Lowassa, hii ni kuwaondolea maaskofu kuaminika (credibility) ili waonekane kuwa hawafai,” alisema Gwajima na kuongeza kuwa; “Maaskofu Wakatoliki hawakupewa rushwa, maaskofu wa KKKT hawakupewa rushwa, mimi sikupewa rushwa.”
Ukiangalia mambo yanayoendelea unaweza kusema hizi ni ngonjera ama malumbano na majigambo, sanaa ambazo zimetoweka nchini mwetu kwa vile mitaala imebumundwa na wajanja na Kiswahili kinaelekea kupoteza misingi hata shuleni.
Dk. Slaa alikwishasema kwamba alikuwa anamsubiri kwanza Gwajima ajibu, halafu atarejea kumwaga mboga na kulivunja kabisa jungu.
Lakini naye Gwajima, wakati alijibu tuhuma hizo, akasema Dk. Slaa anatumiwa na kuonya kwamba kama atajibu hayo, basin aye atarejea tena kueleza kila kitu ambacho Dk. Slaa alikifanya akiwa Afrika Kusini na vijana wa Usalama wa Taifa kabla hajarejea na kushusha tuhuma.
Wakati alipojitokeza kwa mara ya kwanza baada ya ukimya mkubwa Agosti 3, 2015, Dk. Slaa alisema kwamba, ujio wa Lowassa kwenye Chadema na Ukawa bado una harufu ya ufisadi, kwani fedha zinazotumika, ambazo zimeingizwa huko ni za mafisadi wale wale waliokuwa kwenye Orodha ya Mafisadi, lakini akakanusha kwamba hafanyi hivyo kwa kukosa nafasi ya kugombea urais.
“Kwangu mimi kuingia Ikulu ni tunda la lengo kuu ambalo ni kurudisha maadili ndani ya nchi hii. Nani hajaona matumizi ya rushwa kwenye mchakato wa Lowassa kutafuta wadhamini? Leo fedha zinazotumika ni za kina Rostam Aziz – wale wale ambao tukisimama jukwaani tumekuwa tukiwaita mafisadi. Nimeheshimu na kutii dhamira yangu kwa kuwa naamini Mungu huzungumza nasi kupitia dhamira zetu,” alisema Dk. Slaa.
Kauli inayofanana na hiyo ilitolewa pia na aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Agosti 6, 2015 wakati akijiuzulu: “Nawaomba radhi sana wanachama na wananchi walioniamini na kuonyesha mapenzi makubwa kwangu na uongozi wangu. Nimeshiriki vikao vya Ukawa vilivyotufikisha hapa. Hata hivyo, dhamira na nafsi yangu inanisuta kuwa katika uamuzi wetu tumeshindwa kuenzi na kuzingatia tunu za Taifa za utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi na uwajibikaji.”
Binafsi naona hapa bado kuna hoja muhimu zinazohitaji kujadiliwa, kwa kina. Gwajima na Dk. Slaa wanatuchezesha shere tu kutuchelewesha, na wanaweza wakayumbisha mawazo ya Watanzania wasisikilize Sera zinazotolewa na wanasiasa kwa mustakabali wa taifa letu wabaki wakijadili vitendawili ambavyo haviteguliki.
Kwa kuzingatia maelezo ya Gwajima, naamini Dk. Slaa atakuwa ‘amepewa mji’ kwani inaonekana Gwajima hakujibu hoja zilizotolewa, na inawezekana hajui siri ambazo Dk. Slaa alisema anazo kuhusiana, kwanza na Lowassa na ushiriki wake kwenye Richmond, lakini pia kuhusiana na Frederick Sumaye, Meneja wa Kampeni wa Lowassa ambaye naye amejiunga Chadema hivi karibuni.
Dk. Slaa umelipasua jipu, lakini kwa nini linakushinda kulikamua? Unadhani kwa kutoa tuhuma na kuziacha zinaelea bila kueleza kwa undani utakuwa unawatendea haki unaowatuhumu ama hata Watanzania kwa ujumla wao ambao pengine hawajui kilicho nyuma ya pazia?
Gwajima ameshindwa kutegua kitendawili chako, sasa rudi kutoka huko Marekani uje utupatie jibu, kwani ulisema kwamba, ulikuwa unamsubiri ajibu zile za awali ndipo ushuke.
Shuka sasa na ‘silaha zako za maangamizi’ ili Watanzania wapime, watafakari na waamue lililo la haki.
Kukaa kimya kunazidi kuzalisha maswali mengi, hivyo njoo upesi utupe jibu la kitendawili… na ulikamua jipu ulilolipasua, maana bado linauma!
Wasalaam.
0656-331974
NB: Makala haya yalichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la WAJIBIKA la Septemba 14, 2015.

No comments:

Post a Comment