Na Daniel Mjema
Moshi. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Buni Ramole anayewania Ubunge Jimbo la Moshi Mjini, juzi alitinga mkutanoni na helkopta inayomilikiwa na Mbunge wa Moshi mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema).
Ramole alitua na usafiri huo saa 10.37 jioni katika viwanja vya Pasua mjini hapa.
Hata hivyo, Ndesamburo alikiri helkopta iliyotumiwa na Ramole ni mali yake.
Ndesamburi alisema kada huyo aliikodisha kwa dakika 30 kwa maelezo kuwa anataka kuona mandhari ya mji wa Moshi.
Kabla ya helkopta kutua eneo la mkutano, Ramole ambaye ni mfanyabiashara, alianza kwa kuzunguka na helkopta hiyo eneo hilo.
Helkopta ilizunguka mara mbili ikipeperusha bendera ya CCM na kutua jirani na eneo la mkutano.
Awali wakati ikiwa angani, baadhi ya viongozi wa CCM waliokuwa jukwaani waliambia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa helkopta siyo upinzani kwa upinzani tu, hata wao wanayo.
Akizungumza katika mkutano huo, Ramole alisema ameilipia helkopta hiyo kuanzia sasa hadi Oktoba.
Alisema wataitumia kufanya kampeni kutoka kata mbalimbali hadi ushindi upatikane.
“Tutazunguka kata zote, pesa nimeshazilipa. Imetosha sasa. Chadema wakae mbali. Safari hii tutashinda kwa kishindo na kuchukua uongozi wa halmashauri.
“Naomba niwahakikishie nitakuwa na ninyi moja kwa moja na mtaletewa mgombea anayekubalika na tutashinda kwa kishindo na tukishinda tuna mpango kabambe wa maendeleoa,” alisema.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment