IGP Ernest Mangu
NA
WILLY SUMIA, SUMBAWANGA
GEOFFREY Robert Mwakatenya
(15) anayesoma kidato cha pili katika shule ya sekondari Kilimani, Manispaa ya
Sumbawanga mkoani Rukwa, amepigwa hadi kufa na baba yake mzazi kwa kosa la
kukutwa na barua ya mapenzi aliyomuandikia mpenzi wake.
Tukio hilo lilitokea Aprili
26, 2015 majira ya saa sita usiku katika Mtaa na Kata ya Majengo baada ya baba
mzazi wa marehemu anayefahamika kwa jina la Robert Mwakatenya kufika nyumbani
kwake na kumkuta mwanaye akiwa ameshika barua mkononi ambayo alibaini haikuwa ya
kawaida.
Taarifa kutoka eneo la
tukio zimedai kuwa baba huyo alianza kumhoji mwanaye ambapo katika hali ya
kutubu alilazimika kueleza ukweli kuwa alikuwa amemuandikia binti ambaye ni mpenzi
wake wa siku nyingi (jina
linahifadhiwa) na wanawasiliana mara kwa mara.
Imeelezwa kuwa, baba
alianza kumpiga mwanaye kwa mateke na fimbo sehemu mbali mbali za mwili na
kusababisha kifo chake kabla ya kutoka nje ya nyumba na kutokomea
kusikojulikana.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa
wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa bado
jeshi la polisi halijafanikiwa kumkamata baba wa marehemu ili aweze kuchukuliwa
hatua za kisheria.
Kamanda Mwaruanda aliomba
ushirikiano kutoka kwa raia wema ili waweze kumtia nguvuni baba wa marehemu
kutokana na unyama alioufanya kwa mwanaye wa kumzaa.
“Ni kweli tukio hilo lipo
na tunaendelea na uchunguzi ili kuweza kumpata baba aliyefanya unyama kwa mtoto
wake mwenyewe, tunawaomba wananchi watupe ushirikiano ili tuweze kumpata maana
atakuwa amejificha sehemu walipo watu,” alisema.
Wimbi la wanafunzi wa shule
za sekondari katika Manispaa ya Sumbawanga kujiingiza katika mapenzi kabla ya
wakati limekuwa kubwa ambapo wazazi wengi wamekuwa wakilalamikia watoto wao
hasa wa kike kuwa na mahusiano ya mapenzi.
Kitengo cha Polisi Jamii
mkoa wa Rukwa kimesema kumekuwepo na malalamiko mengi ya wazazi kuhusu watoto
wa kike kuacha shule au kuwa watoro shuleni kutokana na wengi wao kushiriki
katika mapenzi na wanaume ambao aidha ni wanafunzi wenzao au wasio wanafunzi.
Mpaka tunakwenda mitamboni,
mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Mazwi, Christina
Sikazwe (17) anatafutwa na wazazi wake
kwa muda wa wiki tatu sasa hajulikani aliko ambapo hata shuleni haonekani
ingawa taarifa kutoka ndani ya familia yake zinadai kuwa aliwahi kupotea kwa
wiki mbili akapatikana kwa mwanamume mmoja.
No comments:
Post a Comment