Katibu wa CCM Wilaya ya Sumbawanga, Bi. Lucy Mfupe
Diwani wa Kata ya Pito, L. Ndasi
Na Prosper
Mgimwa, Sumbawanga
CHAMA cha
Mapinduzi (CCM) wilayani Sumbawanga kimewaonya wanachama wake kuwa makini na
wagombea wa nafasi mbalimbali wanaojitokeza na kwamba wafanye uamuzi sahihi
kumpata mgombea makini atakayekisaidia kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu.
Akizungumza na
viongozi na watendaji wa chama hicho wa Kata ya Pito katika kikao cha ndani
kilichofanyika katika Kijiji cha Malagano hivi karibuni, Katibu wa CCM Wilaya
ya Sumbawanga, Bi. Lucy Mfupe, alisema ingawa muda wa kura za maoni haujafika,
ni vyema wanachama hao wakawa makini kuwapata wagombea wanaokubalika na jamii
badala ya kurubuniwa.
“Tunahitaji
tupate ushindi wa kishindo kuanzia ngazi za chini, hivyo lazima kuteua watu wanaokubalika
kuwa wawakilishi wetu katika udiwani na ubunge, chagueni mtu anayeweza kuleta
maendeleo, anayekubalika na jamii na ambaye hataweza kutuangusha,” alisema.
Bi. Mfupe
aliwataka viongozi na watendaji wa chama hicho kuwahamasisha wananchi
kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura pamoja na kuipigia kura
Katiba Pendekezwa.
Alisema ingawa
muda umebaki mfupi, lakini viongozi hao wanapaswa kuandaa mikutano na kuwasomea
wananchi Katiba Pendekezwa ili waielewe na kuwahamasisha wajitokeze kuipigia
kura.
“Siyo wakati
wa kubweteka, ni lazima kuandaa mikutano hata katika makundi na kuwasomea
wananchi Katiba Pendekezwa waielewe ili waweze kuipigia kura,” alisema Bi.
Mfupe.
Awali akitoa
taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2010 hadi
2015, Diwani wa Kata ya Pito, L. Ndasi, alisema sekta ya elimu kwa shule za
msingi na sekondari kwenye kata hiyo imeendelea kuboreshwa ikiwa ni pamoja na
uandikishwaji wa watoto wa madarasa ya awali hadi darasa la kwanza.
“Wastani wa
uandikishwaji watoto kwenye madarasa ya awali umeongezeka kutoka 250 hadi 440
wakati ule wa kuingia darasa la kwanza umeongezeka kutoka 240 hadi kufikia
442,” alisema Ndasi.
Aidha, Diwani
huyo alisema kwamba, ufaulu wa wahitimu wa darasa la saba kwenda kidato cha kwanza
umeongezeka kutoka 80 hadi 175 na kwamba ufaulu kwa wahitimu wa kidato cha nne
katika shule ya Itwelele umeongezeka kutoka daraja la tatu mwaka 2010 hadi
kufikia daraja la kwanza kwa mwaka 2014.
Diwani Ndasi
alisema kwamba miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezwa katika kipindi hicho
ukiwemo ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa ya shule za msingi Mpwita na Malagano
uliogharimu Shs. 46 milioni, ambapo Shs. 17 milioni kati ya hizo ni michango ya
wananchi.
“Tumejenga
vyoo katika shule za msingi Azimio, Tamasenga, Pito, Malagano na Mpwita kwa
gharama ya Shs. 50,750,000 na kati ya hizo michango ya wananchi ni Shs.
14,750,000,” alisema na kuongeza kwamba halmashauri ya wilaya pia ilitoa jumla
ya madawati 157 kwa shule hizo.
Miradi mingine
iliyotekelezwa ni ukarabati wa madarasa, ujenzi wa maabara katika shule ya
sekondari Itwelele, ujenzi wa zahanati na nyumba za watumishi na kituo cha
rasilimali za kilimo na mifugo huku barabara zenye urefu wa kilometa 51 zikiwa
zimechongwa kuunganisha vijiji vya kata hiyo.
No comments:
Post a Comment