Na Lorietha Laurence-Maelezo
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
imeandaa kampeni kwa ajili ya ugawaji wa vyandarua vya hati punguzo
katika kaya nchini, inayotarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe.Dkt Kebwe Stephen, amesema kampeni hiyo
imeanzishwa ili kuziba pengo kutokana na kusitishwa kwa huduma ya hati
punguzo iliyokuwa ikifadhiliwa na Mennonite Economic Development
Associates (MEDA) mapema mwezi Juni 2014 .
Dkt. Kebwe aliongeza kuwa jamii pamoja na wakina akinamama
wajawazito watanufaika na kampeni hiyo, ikiwemo ile ya ugawaji wa
vyandarua kwa wanafunzi shuleni ambayo imeanza kutekelezwa tangu mwaka
2013 kwa mikoa ya Lindi,Ruvuma na Mtwara.
“kampeni hii ni muhimu na ni mojawapo ya njia mbadala ya
kuendelea kuwasaidia akinamama wajawazito na watoto wachanga kujikinga
na ugonjwa wa malaria ikiwa ni mkakati wa kupunguza vifo vya akinamama
na watoto”alisema Mhe.Dkt. Kebwe
Aidha, jumla ya vyandarua milioni 13 vimesambazwa kupitia mpango
huo, ambapo imechangia katika kuongeza matumizi ya vyandarua kwa
akinamama wajawazito kutoka 16% mwaka 2004 hadi 75% mwaka 2012 na kutoka
16% hadi 76% kwa upande wa watoto.
Pia alifafanua kuwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua
itaendelea kutolewa Kwa watumiaji wa vyandarua hivyo, kwani baadhi ya
watu wamekuwa wakitumia tofauti kwa kufugia kuku na hata wengine kuweka
katika bustani ili kukinga ndege waharibifu badala ya kujikinga na mbu.
Mpango huu wa hati punguzo ni mkakati ulioendelevu kuhakikisha
kuwa makundi ya akinamama wajawazito na watoto wachanga wanaendela
kupata vyandarua ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa malaria na umekuwa
ukitekelezwa kupitia ufadhili wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana dhidi ya
ugonjwa wa Ukimwi, Kifua kikuu na Malaria, Shirika la Maendeleo la
Serikali ya Watu wa Marekani (USAID), Shirika la Maendeleo la Uswisi
(SDC) na Idara ya Maendelao ya nchi ya Uingereza.
No comments:
Post a Comment