Makala na Nassor Gallu
SIKU ya Agosti 8, mwaka huu kutakuwa na bonge la mechi
litakalopigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar ambapo wabunge
wanaoshabikia Yanga, watakuwa dimbani kupepetana na wenzao wa Simba.
Wabunge wa timu ya Simba wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Hebu jaribu kuvuta picha katika
ubongo wako, waheshimiwa wabunge watakapoweka kando masuala ya ‘Ukawa’
na ‘Tanzania Kwanza’, kisha kukutana katika uwanja kuonyeshana umwamba
kwa kusakata gozi la ng’ombe katika mchezo huu wa kihistoria.
Kila timu tayari imeingia
mafichoni kujiwinda na mchezo huo ili kuhakikisha inaibuka kidedea na
kujenga heshima mbele ya watani wao huku Simba wakiahidi kulipiza kisago
cha bao 1-0 walichokipata mwaka jana kutoka kwa Yanga.
“Tayari tumeingia kambini
kujiwinda na mchezo huu ili kuziba midomo na kelele za Yanga ambao
wamekuwa wakitamba tangu watubahatishe mwaka jana,” alijinasibu Hamis
Kigwangala ambaye ndiye nahodha wa Simba.
Kwa upande wa mlezi wa Yanga
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Temeke, Abassi Mtemvu, alijigamba kuwa
ni lazima waendeleze moto wa ushindi kwa kuwa wapo na kikosi imara na
tayari wameshaingia kambini kwa kuwa mchezo huu ni siriazi kwao.
“Kwa kweli mchezo huu
tumeuchukulia kwa mtazamo wa juu kabisa na lazima tuwapige kwa kuwa tuna
damu changa nyingi, hatuna masihara, maana wakitufunga hatutakaa
bungeni.
“Tupo katika maandalizi ya mwisho kwa sasa ingawa tulipoweka kambi yetu itabaki kuwa siri,” alisema Mtemvu kwa kujiamini.
Baadhi ya wabunge wanaounda timu
ya Yanga ni pamoja na Abassi Mtemvu, Ridhiwani Kikwete, Freeman Mbowe
na Mwigulu Nchemba, huku kikosi cha Simba kikiundwa na wakali kama
Zitto Kabwe, Hamisi Kigwangalla, Wiliam Ngeleja, Juma Nkamia, Amos
Makalla na Ismail Aden Rage.
Mbali na mchezo huo ambao utakuwa
kivutio kikubwa kwa wadau wa soka, pia kutakuwa na mchezo mwingine wa
kusisimua pale Bongo Fleva chini ya mkali wao, Peter Manyika
itakapopepetana na Bongo Movie FC chini ya Jacob Steven JB.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Bongo
Movie, Fatuma Makongoro ‘Bi Mwenda’, tayari ameanika wachezaji wake huku
akisema kuwa hahofii kwani kikosi chake kipo kamiligado kuelekea mchezo
huo ambao wameuchukulia kwa umakini mkubwa.
“Sisi tumeuchukulia ‘serious’ sana
mchezo huu kwa kuwa mashabiki wetu watakuja wengi na hatutakubali
kuwaangusha.“Wachezaji waliopo kambini mpaka sasa ni Mzee Majuto,
Kingwendu, Bambo, JB, Steve Nyerere, Dk Cheni, Ray, Mtitu, Cloud pamoja
na Muhogo Mchungu,” alisema Bi Mwenda.
Wabunge wa timu ya Yanga wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Akijibu mapigo ya wapinzani wao,
kocha wa Bongo Fleva ambaye pia anakinoa kikosi cha Yanga, Juma
Pondamali ‘Mensah’, alisema Bongo Movie wajiandae kupata kipigo cha
mshangao kwa kuwa wao hawatakwenda kuigiza uwanjani.
“Hawa waigizaji wajiandae na
kipigo cha ‘sapraizi’, maana pale sisi hatuendi kuigiza, tunaenda kupiga
kazi kwa kuwa mpira hauigizwi, unachezwa kila mmoja anaona, sasa acha
wapige domo wataona kitakachowakuta,” alisema Pondamali.
Baadhi ya mastaa wanaounda kikosi cha Bongo Fleva ni pamoja na Peter Manyika, H-Baba, Ali Kiba, Rich One, Kalapina na wengineo.
Ukiachana na soka, pia kutakuwa na burudani mbalimbali ambapo mastaa kibao kutoka ndani na nje ya nchi watakuwepo kulipamba jukwaa la Usiku wa Matumaini.
Baadhi ya mastaa hao ni pamoja na
Yemi Alade kutoka Nigeria, Madee, Ali Kiba, Roma Mkatoliki, Shilole,
Menninah, Juma Nature na kundi zima la TMK Wanaume Halisi.
Mgeni rasmi katika tamasha hili
atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed
Gharib Bilal.Tamasha la Usiku wa Matumaini limedhaminiwa na Clouds FM
(88.5), Times Fm (100.5), Vodacom, Pepsi, Azam TV pamoja na Syscorp.
Credit Source: Fullshangwe
No comments:
Post a Comment