Na Anna Nkinda – Maelezo aliyekuwa Lindi
Wanawake wenye tatizo la
ugonjwa wa Fistula wametakiwa kutokuogopa na kukaa kimya bali
wajitokeze hadharani kwa kwenda Hospitali kupata matibabu au kuwaambia
viongozi wao ili waweze kuwasaidia kwani ugonjwa huo unatibika na
matibabu yake ni bure.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni
na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa
nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya chama hicho
katika matawi ya Mkoimba, Ng’apang’apa, Mbuyuni B, Mkanga, Mtutu na
Rutende.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema ugonjwa wa Fistula unatokana na
uzazi, mwanamke akishikwa na uchungu wa kujifungua kwa muda mrefu kibofu
cha mkojo kinaharibika na mgonjwa hutokwa na haja ndogo mara kwa mara
bila kutegemea.
“Mnapoona katika jamii yenu kuna
mwanamke anatatizo hili muwasiliane na uongozi wa wilaya ili tuweze
kumsaidia mama huyu kwa kumpeleka Hospitali ya CCBRT ambako atafanyiwa
upasuaji na kurudi katika hali yake ya kawaida kama alivyokuwa zamani”,
alisema Mama Kikwete.
Kuhusu ugonjwa wa saratani
aliwasisitiza viongozi hao kuwa wajumbe wazuri ili wawahimize wanawake
kujitokeza kwa wingi kupima saratani ya shingo ya kizazi na matiti
kwani kina mama wengi wanakufa kutokana na ugonjwa huo kwani unatibika
endapo mgonjwa atawahi kupata matibabu .
Alisema , “Nanyi Kina baba
muwasisitize na kuwapa ushirikiano wake zenu ili waende kupima na kama
utaona mkeo anadalili za saratani ya kizazi awahi Hospitali mapema
kupata matibabu.
“Kina mama mkienda Hospitali
waombeni wauguzi wawaelekeze jinsi ya kupima saratani ya matiti, ni
rahisi na hii itakusaidia hata wewe mwenyewe kujipima unapokuwa
nyumbani”.
Kwa upande wa kina mama wajawazito
aliwasihi kuhudhuria kliniki mapema ili kama kuna tatizo
litagundulika mapema na kupelekwa katika Hospitali kubwa na hivyo
kujifungua salama pia watapewa dawa za kumeza ambazo mama mjamzito
anatakiwa kuzitumia.
Aidha MNEC huyo aliwasisitiza
wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi
katika uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu
mwakani ili waweze kufika ngazi ya maamuzi na kuweza kuwatetea wanawake
na watoto ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.
Akizungumzia kuhusu malezi ya
watoto Mama Kikwete aliwataka wazazi na walezi kuwalea watoto wao
katika misingi mizuri ya dini na kuwapeleka shule wakapate elimu ambayo
itawasaidia katika maisha yao pia msiwafiche watoto wenye tatizo la
ugonjwa wa mdomo sungura ambao unatibika kwa njia ya upasuaji.
Wakati huohuo Mama Kikwete akiwa
katika matawi hayo alipata muda wa kuwapa nasaha watoto waliofika
kumsalimia kwa kuwahimiza umuhimu wa kusoma kwa bidii kwani elimu ndiyo
kitu pekee kitakachowasaidia kujikwamua kiuchumi katika maisha yao ya
baadaye.
“Wazazi wenu wanapowaamsha asubuhi
ili muende shule kwa sasa baadhi yenu mnaona kama wanawasumbua
vumilieni hii tabu mnayoipata sasa , mtakuja kufaidi matunda yake hapo
baadaye pale mtakuwa mmemaliza masomo yenu na kupata kazi”, alisisitiza
Mama Kikwete.
MNEC huyo ambaye alikuwa wilayani
humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na
kufanya vikao vya ndani na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya mwaka 2010 akiwa katika tawi la Mbuyuni B aliwakabidhi kadi
wanachama wapya wa CCM tisa na Umoja wa Wanawake (UWT) watatu.
No comments:
Post a Comment