Na Daniel Mbega
MCHAKATO wa kutafuta Katiba Mpya utaendelea
endapo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) utatwaa Dola Oktoba mwaka huu,
imefahamika.
Taarifa kutoka ndani ya Ukawa zinaeleza
kwamba, umoja huo utaipitisha Rasimu ya Pili ya Katiba iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ambayo inapendekeza muundo wa Muungano wa Serikali Tatu.
Rasimu hiyo ya Tume ya Warioba ilipendekeza
muundo wa Serikali Tatu, ambapo ile ya Muungano itakuwa ya mkataba badala ya
mfumo wa sasa ulivyo.
Hali hiyo inatasfiriwa kwamba, ushindi wa
Ukawa ndio utakuwa mwisho wa Katiba Pendekezwa ambayo ilikuwa ipigiwe kura ya
maoni mwaka huu kabla ya kuahirishwa.
“Chanzo cha Ukawa ni kutetea ‘Katiba ya
Wananchi’ ambapo wapinzani tuliungana pamoja kuiafiki Rasimu ya Pili ya Katiba
kama ilivyowasilishwa na Jaji Joseph Sinde Warioba aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo tukitwaa Dola, lazima tuwatendee haki Watanzania
kwa kuwapa kile wanachokitaka,” alisema mbunge mmoja wa Chadema ambaye aliomba
hifadhi ya jina lake kwa kuwa siyo msemaji.
Mbunge huyo amesema sababu ya wao kususia
vikao vya Bunge Maalum la Katiba tangu Aprili 2014 ni kupinga hila za Chama cha
Mapinduzi za kuichakachua Rasimu ya Pili ya Katiba kwa kuwa ilikuwa inawabana
viongozi wa Serikali ya chama hicho.
Mnamo Jumatatu Machi 17, 2014 wabunge wa
upinzani walianza kupinga mchezo mchafu uliofanyika baada ya Mwenyekiti wa
Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, kumruhusu Jaji Joseph Sinde Warioba
(Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba), awasilishe Rasimu ya Katiba hiyo
Bungeni kabla ya
Rais Jakaya Kikwete kulihutubia Bunge hilo.
Hali hiyo iliwalazimu wabunge waliokuwa
wanaunda Ukawa kutoka vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, DP, Chausta,
Chauma,NRA, NLD na CCK pamoja na wajumbe walioteuliwa kutokana na makundi
yaliyotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kutoka
nje.
Hata hivyo, wabunge wa vyama vya Chadema,
CUF, NCCR-Mageuzi na NLD waiamua kususa moja kwa moja vikao baada ya kutoka nje
ya Bunge hilo mnamo Jumanne Aprili 15, 2014 na tangu hapo hawakuhudhuria tena.
Baada ya hapo wabunge wote wa Ukawa
wakaanza ziara ya nchi nzima na kufanya mikutano ya hadhara kueleza namna CCM
ilivyokuwa inaichakachua Rasimu hiyo, mikutano ambayo baadaye ikazaa
makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja wa urais.
Tume ya Katiba
Ikiwa Ukawa wataingia madarakani na kurejea
Rasimu ya Pili, watakuwa wamenusuru takriban Shs. 60 bilioni zilizotumiwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika michakato mbalimbali, ikiwemo posho za
wajumbe.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikuwa na
wajumbe 34 na iliundwa chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura 83, Toleo
la 2012, Vifungu 5, 6 na 7 ambapo Mwenyekiti wake alikuwa Jaji Warioba na
Makamu Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhan.
Wajumbe waliokuwa wanaonda Tumehiyo kutoka
Tanzania Bara walikuwa Profesa Mwesiga Baregu, Riziki Shahari Mngwali, Dk.
Edmund Sengodo Mvungi (sasa marehemu), Richard Shadrack Lyimo, John Nkolo,
Alhaj Said El-Maamry, Jesca Sydney Mkuchu, Prof. Palamagamba Kabudi, Humphrey
Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Malingumu Kashonda, Aly-Shymaa
John Kwegyir (MB), Mwantumu Jasmine Malale na Joseph Warioba Butiku.
Wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa Dk. Salim
Ahmed Salim, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali
Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Hamis Mohammed, Simai Mohammed
Said, Muhammed Yussuf Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama
Kombo Ahmed, Abubakar Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh.
Aidha, Uongozi wa Sekretarieti ya Tume hiyo
ulikuwa na Assaa Ahmad Rashid (Katibu) na Casmir Sumba Kyuki (Naibu Katibu).
Bunge la Bajeti liliwahi kuidhinisha Sh.
33.944 bilioni mwaka 2012/2013na kiasi kama hicho kikaombana Wizara ya Sheria
na Katiba kwa mwaka 2013/2014 kwa ajili ya matumizi ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Kiasi cha Sh. 33.944 bilioni kilichoombwa
mwaka 2013/2014 kilihusisha Sh. 12.193 bilioni kwa ajili ya posho za vikao kwa
wajumbe wa Tume 34 na Sekretarieti 160; Sh. bilioni 1.728 za posho ya kujikimu
kwa ajili ya wajumbe na Sekretarieti wanaposafiri ndani ya nchi kikazi; na Sh.
bilioni 1.650 kwa ajili ya kulipa gharama za nyumba za wajumbe na Sekretarieti
wanaotoka nje ya Dar es Salaam.
Pia Sh. 18 milioni ziliombwa kwa ajili ya
kughariamia chakula kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti watakaokuwa wamepata
maambukizi ya Ukimwi; Sh. 60 milioni kwa ajili ya usafiri wa ndani; Sh. 50 milioni
kwa ajili ya gharama za malazi kwa wajumbe wa Tume na Sekretarieti
‘wanaposafiri kikazi’; Sh. 423 milioni kwa ajili ya ‘chai na vitafunwa’; na Sh.
50 milioni kwa ajili ya wahudumu wanaosaidia kazi za Tume wakiwa mikoani wakati
wa kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la upigaji kura ya maoni.
Aidha, kulikuwa na maombi ya Sh. 19.039
bilioni nyingine kwa ajili ya posho za aina mbalimbali na malipo mengine
yanayowahusu wajumbe na Sekretarieti ya Tume kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Wizara iliomba Bunge liidhinishe Sh. 60 milioni
kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za Tume; Sh. 30 milioni kwa ajili ya kulipia
gharama za usafiri wa basi na teksi kwa wajumbe na Sekretarieti watakaposafiri
ndani ya nchi kikazi; Sh. 103 milioni kwa ajili ya kulipia gharama za simu za
mikononi; na Sh. 604 milioni kwa ajili ya posho kwa wajumbe wa Tume na
Sekretarieti wakati wa Bunge Maalum la Katiba.
Wajumbe wa kawaida wa Tume kwa mujibu wa
mchanganuo wa bajeti, walikuwa wanalipwa Sh. 200,000 kama posho ya vikao kwa
siku. Maofisa waandamizi wa Tume hiyo walikuwa pia wanalipwa posho ya Sh.
200,000 kwa siku, maofisa wa kati walikuwa wanalipwa Sh. 150,000 kutwa na
maofisa wa ngazi za chini walikuwa wanalipwa Sh. 100,000 kwa siku kulingana na
taratibu za Serikali.
Bunge Maalum la Katiba
Bunge hilo lilikuwa na wajumbe 640
likijumuisha wabunge wote 357 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wajumbe 82 wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na 201 kutoka kwenye makundi mbalimbali.
Makundi hayo na idadi ya wajumbe kwenye
mabano ni Taasisi zisizo za Kiserikali (20), Taasisi za Dini (20), Vyama vya
Siasa (42), Taasisi za Elimu (20), Makundi ya Walemavu (20), Vyama vya
Wafanyakazi (19), Vyama vya Wafugaji (10), Vyama vya Wavuvi (10), Vyama vya
Wakulima (20) na Makundi yenye Malengo yanayofanana (20).
Bunge hilo, ambalo lilisusiwa na wapinzani
kwa uchakachuaji wa rasimu, lilianza Februari 18, 2014 likiwa limepangiwa
kufanyika kwa siku 90, na linatajwa kwamba lilitumia gharama kubwa kiasi cha
Shs. 192 bilioni kwa posho tu za wajumbe mbali ya gharama nyingine za
uendeshaji.
Ikiwa Ukawa wataamua kuirejea Rasimu ya
Pili kama ilivyo, gharama za Bunge Maalum la Katiba zitakuwa zimekwenda na maji
na kwamba fedha nyingine zaidi zitalazimika kutengwa ili kuitisha kikao kingine
cha Bunge Maalum kuijadili upya rasimu hiyo.
Vipo vikwazo vingi vilivyoleta mgongano
wakati wa mjadala wa rasimu hiyo ya pili, lakini kikubwa zaidi ni hoja ya
Muundo wa Muungano wa Serikali Tatu ambao CCM waliupinga kwa nguvu zote kwa
mtazamo kwamba ungeua muungano wa sasa.
Hoja nyingine ni vipengele vya kuwabana
viongozi wa kuchaguliwa, wakiwemo Rais na Wabunge, na kwamba Rais anaweza
kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye hata akiwa madarakani na pia anaweza
kushtakiwa.
Wananchi wengi walionekana kuunga mkono
rasimu hiyo ya pili wakiwanaimani kwamba wanaweza kuwawajibisha wawakilishi wao
na hivyo maendeleo kupatikana.
CHANZO: GAZETI LA WAJIBIKA, AGOSTI 17, 2015

No comments:
Post a Comment