Maxence Mello, Mkurugenzi wa kampuni ya Jamii Media wamiliki wa JamiiForums na Fikra Pevu, akifafanua madhara ya Sheria ya Makosa ya Mtandao kwa wahariri na waendhsa blogu (blogger) wakati wa warsha ya siku moja iliyofanyika kwenye Hoteli ya Kebbys, Mwenge jijini Dar es Salaam Agosti 27, 2015. (Picha na Daniel Mbega).
Maxence Mello akijibu maswali mbalimbali kutoka kwa washiriki (hawapo pichani).
James Marenga, mwanasheria kutoka Nola, akifafanua kuhusu Sheria ya Takwimu ambayo itaanza kutumika Septemba Mosi, 2015.
Washiriki wa warsha wakifuatilia.
Na Daniel Mbega
AGOSTI
27, 2015 Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika tawi la Tanzania (MISA-TAN)
iliwaita baadhi ya wahariri na waendesha blogu (bloggers) nchini kujadili ujio
wa sheria kadhaa zinazoonekana zitawabana, si waandishi tu, bali Watanzania
wote wanaotumia mitandao ya kijamii.
Sheria
ambazo zitawabana watumiaji wote wa mtandao wa internet ni ile ya Makosa ya
Mtandao na Sheria ya Takwimu, ambazo zote zimepitishwa mwaka 2015 na zinaanza
kazi rasmi Septemba Mosi, 2015 huku Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ikitangaza
kiama kwa wale wanaotumia vibaya na wahalifu wote wa mitandao nchini.
Wakati wa
warsha ya siku moja iliyoandaliwa na MISA-TAN, ilielezwa kwamba hakuna
atakayekuwa salama katika sheria hizo mbili, hali ambayo inaifanya Tanzania
kuingia kwenye orodha ya mataifa yenye sheria kali za utumiaji wa mtandao na
kuunyonga kabisa uhuru wa kupashana habari.
“Lengo la
Sheria ya Makosa ya Mitandao ni kuangalia makosa kama vile kutuma taarifa bila
ridhaa ya mtu, kusambaza picha za ngono na za utupu, udanganyifu unaohusiana na
kompyuta, kughushi kunakohusiana na masuala ya kompyuta na pia kusambaza picha
za utupu za watoto na hata marehemu,” alisema Maxence Mello, Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni ya Jamii Media inayoendesha jukwaa maarufu duniani la
JamiiForums pamoja na tovuti ya Fikra Pevu.
Maxence,
mhandisi wa ujenzi ambaye kwa sasa amezama kwenye habari hususan katika upande
wa uandishi wa mitandaoni, alisema ingawa Watanzania walio wengi hawafahamu
ujio wa Sheria hiyo na inawahusu kwa namna gani, lakini kwa lugha rahisi ni
kuwa itamuathiri mtu yeyote anatumia mtandao wa internet kwa kutimia kifaa
chochote - iwe kompyuta kubwa au vifaa vyenye uwezo wa kufanya kazi kama
kompyuta kama simu za mikononi, saa, televisheni na vifaa vingine vinavyoendana
na hivyo.
Malengo ya
Sheria hii ni kuainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta
na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kuweka utaratibu wa upelelezi,
ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki na masuala mengine
yanayohusiana na hayo.
Matumizi
ya mitandao yote mikubwa kama Twitter, Instagram, JamiiForums, Facebook, Barua
pepe, WhatsApp, blogu na data zote zilizo katika kifaa chochote cha
kielektroniki yanaathiriwa kwa kiwango kikubwa na Sheria hii.
Hiyo
inamaanisha kwamba, jitihada za kuufanya mtandao wa internet kuwa wazi ili kila
mtu awe na uhuru wa kuunganishwa, kuwasiliana, kuandika, kusoma, kutazama,
kuzungumza, kusikiliza, kujifunza, kuunda na kubuni nazo zinafikia kikomo.
Sheria hiyo haijaeleza kuhusu kulinda uhuru wa kugundua na kuunda bila kulazimika kuomba idhini, hatua ambayo itawafanya wanasayansi chipukizi kuogopa kufanya ugunduzi wowote kwa kuhofia kuingia matatani.
Sheria hiyo haijaeleza kuhusu kulinda uhuru wa kugundua na kuunda bila kulazimika kuomba idhini, hatua ambayo itawafanya wanasayansi chipukizi kuogopa kufanya ugunduzi wowote kwa kuhofia kuingia matatani.
Maxence
alisema hakuna anayepingana kuwepo kwa sheria ya mitandao ambayo kimsingi
itadhibiti baadhi ya mambo, lakini akasema tatizo kubwa lipo kwenye adhabu
zinazoendana na sheria hiyo.
“Sheria
ni muhimu iwepo ili kudhibiti, hata hivyo adhabu zake ni kubwa kiasi kwamba
hakuna Mtanzania wa kawaida, ambaye ndiye mtumiaji mkubwa wa mitandao hii,
atakayemudu kulipa faini tajwa, vinginevyo mamia kwa maelfu wataishi gerezani.
“Sheria
inapoeleza kwamba utalipa faini isiyopungua shilingi milioni tatu, au kifungo
kisichopungua miezi sita, tafsiri yake halisi ya kisheria ni kwamba unaweza ama
kuhukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni hamsini au ukatumikia kifungo cha
miaka 10 jela kwa sababu imeelezwa ‘isiyopungua’ na siyo ‘isiyozidi’,” alisema
Maxence.
TCRA
inasema Tanzania inaongoza kwa kuwa na watumiaji vibaya wengi wa mitandao ya
kijamii, jambo linalosababisha taarifa nyingi za mitandao kutoaminika hadi nje
ya nchi kutokana na kujaa uzushi, uongo, uchochezi na lugha na picha za matusi.
Mamlaka
hiyo inasema kwamba, pamoja na kufanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya
utumiaji sahihi wa mitandao hiyo, bado matumizi yake si mazuri hasa katika
kipindi hiki cha uchaguzi na kwa watu maarufu.
Kwa mujibu
wa sheria hiyo, mtu atakayepatikana na hatia ya kusambaza picha za ngono,
matusi, uasherati atalipa faini isiyopungua Shs. 30 milioni au kutumikia
kifungo kisichopungua miaka 10 au vyote.
James
Marenga, Mwanasheria kutoka taasisi ya kisheria ya Nola, akielezea Sheria ya
Takwimu, alisema nayo itawapeleka wengi gerezani hasa tunapoelekea kwenye
uchaguzi mkuu.
Marenga,
ambaye pia ni mwanahabari na wakili wa Mahakama Kuu, alisema kwa mujibu wa
sheria hiyo, hakuna takwimu ambazo zitatolewa bila idhini ya mamlaka husika, na
endapo mtu atatenda kosa hilo ataingia matatani.
“Kwa
mfano, tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, ile tabia iliyozoeleka ya kuandika
kwamba ‘fulani anaongoza’ inaminywa na sheria hii, hakuna mtu anayeruhusiwa
kutangaza matokeo – hata ya awali – isipokuwa msimamizi wa uchaguzi au Tume ya
Taifa ya Uchaguzi makao makuu,” alisema.
Ofisa wa
MISA-TAN, G.S. Gasirigwa, alisema ni vyema wanahabari wakawa makini katika ujio
wa sheria hizo, kwani tayari zimekwishapita na hakuna namna ya kuzikwepa.
“Hata tufanye
nini haiwezekani, sheria zimekwishapitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lazima tuziishi, hoja ni namna gani
tunaziishi,” alisema.
Imeandaliwa na www.brotherdanny.com. Simu:
0656-331974
No comments:
Post a Comment