Mwalimu Nyerere
(Inaendelea kutoka jana)
MSIMAMO WA CHAMA
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi haiwezi kuepuka lawama. Lakini kuilaumu Kamati Kuu ni kukiri kwamba sasa Chama Cha Mapinduzi kina kansa ya uongozi ambayo isipotibiwa itakiua Chama kizima. Pengine kwa nchi yetu hii lisingekuwa jambo la kutisha kama tungekuwa tumeanza kuona chama kizuri cha upinzani ambacho kinaweza kuiongoza nchi hii badaIa ya CCM. Hakijaonekana bado.
Chama Cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa watu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa vyama vya upinzani, kinaweza kuendelea kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama chochote, ili mradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa nchi yetu unataka yasemwe.
Viongozi wakuu wa CCM walimshauri Rais suala la OIC lisizungumzwe na Chama. Sijui lingezungumzwa msimamo wa Kamati Kuu ungekuwaje. Lakini viongozi wahusika walihisi kuwa angalau baadhi ya idadi ya wapinzani itakuwa kubwa zaidi likifikishwa katika HaImashauri Kuu ya Taifa. Lakini suala la utaratibu wa kuchagua Makamu wa Rais lilifikishwa katika Kamati Kuu; Kamati Kuu ikakubali msimamo wa 'Wazanzibari", maana ulikuwa "nyeti"; na ikapendekeza kuwa Halmashauri Kuu nayo ikubali msimamo huo; kwa sababu "nyeti" hizo ambazo hazina maelezo. Mjadala ulipokuwa mgumu, viongozi wakafanya hila suala likahamishwa kutoka katika HaImashauri Kuu bila uamuzi, likapelekwa bungeni kwenda kuombewa muda wa miaka miwili. Chombo kilichotumiwa na viongozi hao ni Kamati Kuu.
Suala la utaratibu wa kuchagua makamu Iilikuwa geni, na sijui ni Wajumbe wangapi wa Kamati Kuu walikuwa wamesoma mapendekezo ya Kamati ya Bomani. Pengine ilikuwa ni rahisi kwa viongozi wetu wakuu kutumia lugha "nyeti", na kuwababaisha Wajumbe wengine wa Kamati Kuu ambao hawajui unyeti wa mambo. Lakini suala la Serikali Mbili ina umri ule ule kama Tanzania yenyewe. Sababu za kupinga Serikali Tatu zinajulikana. Kwa hiyo tume ya Jaji Nyalali ilipopendekeza Shirikisho la SerikaIi Tatu, pendekezo hilo lilipingwa na Kamati Kuu, lilipingwa na HaImashauri Kuu, lilipingwa na Mkutano Mkuu wa CCM, na lilipingwa na Serikali ya Muungano katika Bunge la Muungano. Hoja ya Serikali Tatu iIipozushwa na wabunge, Kamati Kuu, kwa niaba ya HaImashauri Kuu ya Taifa, na chama kizima, iliwaagiza viongozi wetu wakaipinge; mwezi Agosti, 1993.
Kamati Kuu hiyo hiyo, katika kikao chake cha Dodoma, cha mwezi wa Novemba, 1993, ikapendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa, kwamba hoja waliyokuwa wamewaagiza viongozi wetu wakaipinge, sasa ikubaliwe; maana viongozi wetu badala ya kuipinga walipata ndoto nzuri zaidi wakasarenda.
Mapendekezo ya Kamati Kuu yanayoiomba Halmashauri Kuu ikubaIi SerikaIi Tatu, hayasemi mahali popole, kwamba mwezi Agosti, Kamati Kuu hiyo hiyo ilikuwa imeagiza Serikali kuipinga hoja hiyo. Wala sijui kama wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya Taifa wanafahamu hivyo. Viongozi wetu wakubwa walipokwisha kusarenda na wakawaandalia wajumbe wa HaImashauri Kuu nao hati yao ya kusarenda.
Hali hii haishangazi; lakini haipendezi. Haishangazi kwa sababu mwenyekiti wa chama, makamu wake wawili, na katibu mkuu wa chama, ndio viongozi wakuu wa chama na wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa. Katika kikao cha wajumbe wachache kama Kamati Kuu, viongozi hawa wakishakuwa na msimamo mmoja, hasa katika jambo zito au suala la msingi, viongozi wa chini yao na wanachama kwa jumla watayumba. Na chama chochote kinapenda umoja; kwa hiyo kinapenda mshikamano wa viongozi wake wakuu katika masuala yote muhimu. Na kama viongozi wanao msimamo huo kuwapinga tu kwa ajili ya kupinga ni jambo la kipumbavu.
Lakini haIi ya sasa haipendezi kwa sababu vyama makini huundwa kwa sababu na shabaha makini. Umoja wa chama ni umoja wa shabaha, si umoja wa nasaba. Ni mbinu au nyenzo ya kufikia shabaha fulani. Tukitekeleza shabaha yenyewe iIiyotufanya tukaunda umoja ili tuitekeleze, umoja au mshikamano mtupu utakuwa hauna maana. Hatuwezi kuheshimu mbinu au nyenzo zaidi kuliko shabaha yenyewe. Au hatuwezi kufanya mshikamano wa viongozi ukawa ndio shabaha na mambo mengine yote yakawa ni nyenzo tu za kufikia na kulinda shabaha hiyo.
Hatuwezi kusema kuwa madhali viongozi wetu wote wanalitaka jambo hili hatuna budi tuwaunge mkono, hata kama tuliwaunga mkono katika jambo ambaIo ni kinyume kabisa cha hili wanalotuomba leo. Na hasa hasa hatuwezi kuwaunga mkono tukijua kuwa jambo wanalotuomba tukubali si haIaIi, na ni kinyume cha msimamo na uamuzi wa chama chetu. Viongozi wetu wakuu hawawezi kukiuka Uamuzi na msimamo wa Chama kizima, halafu wadai kuungwa mkono na viongozi wa chini yao au na wanachama kwa jumla. Kwa kweli tunatazamia kuwa viongozi hao watapingwa kwa nguvu kabisa, na kama hapana budi kufukuzwa. Huko ndiko kuwajibika. Bila hivyo viongozi wetu watafanya wapendavyo bila kuwa na wasiwasi. Watapinda, watapuuza, watavunja maamuzi na msimamo wa chama bila kuwa na hofu yoyote. Wenye hofu watakuwa ni viongozi wa chini na wanachama wa kawaida watakaofanya ujasiri wa kuwapinga viongozi wakuu. Maana hao wataonekana kuwa ni wakorofi na wachochezi, na watachukuliwa hatua za nidhamu!
Kwa kweli hapo ndipo tupo sasa. Tume ya Jaji Nyalali imependekeza Shirikisho la Serikali Tatu. Kamati Kuu imepinga; Halmashauri Kuu ya Taifa imepinga; Waziri Mkuu amesimamia uamuzi huo na kuutetea Bungeni, tarehe 30 Aprili, 1992. Mkutano mkuu wa CCM huko Chimwaga umepinga pendekezo hilo na kusisitiza tena sera ya Chama ya tangu 1964, ya Muungano wa Serikali Mbili. Mwezi Agosti, 1993, wabunge fulani wamefufua suala hili tena kuleta hoja ya kudai Serikali Tatu.
Tarehe 10.8.1993 Kamati Kuu imekutana na kusisitiza tena msimamo wa Chama, na kuiagiza Serikali ikaipinge hoja hiyo. Tarehe 14.8.1993 Rais wa Jamhuri ya Muungano anakwenda Bungeni na kupinga Hoja ya Serikali Tatu. Hapo ni kabla viongozi wetu wakuu hawajapata ndoto nzuri zaidi.
Itaendelea kesho...
No comments:
Post a Comment