Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira (kushoto), akihutubia katika uzinduzi wa kampeni ya chama hizo uliofanyika viwanja vya Zakhem Mbagala jijini Dar es Salaam leo. (Picha zote na Dotto Mwaibale wa habarizajamii.com).
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto akihutubia katika uzinduzi huo.
Mshauri wa Chama cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo akihutubia kwenye uzinduzi huo.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto (kushoto), akiteta jambo na Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira.
Viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiimba wimbo wa taifa.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, akiwatambulisha wagombea ubunge wa majimbo yote ya Dar es Salaam.
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, akigawa ilani ya chama hicho kwa mgombea urais na mwenza wake.
Mgombea Mwenza, Hamad Mussa Yusuph akihutubia kwenye uzinduzi huo.
Mwana muziki Bwana misosi, akitoa burudani katika uzinduzi wa kampeni wa Chama cha ACT-Wazalendo uliofanyika viwanja vya Zakhem Mbagala Dar es Salaam leo.
Umati wa Wananchi ukiwa katika uzinduzi wa kampeni wa Chama cha ACT-Wazalendo uliofanyika viwanja vya Zakhem Magala Dar es Salaam leo.
Na Daniel Mbega
CHAMA cha ACT-Wazalendo leo kimezindua rasmi kampeni zake kitaifa huku mgombea urais wa chama hicho, Bi. Anna Elisha Mghwira, akisema wataunda serikali makini ambapo Zitto Kabwe atakuwa Waziri Mkuu.
Akizungumza katika mkutano huo kwenye Viwanja vya Mbagala-Zakhem jijini Dar es Salaam, Bi. Mghwira aliwataka Watanzania kukipa dhamana chama hicho kwa kuwa sera zake zitarejesha misingi imara iliyoasisiwa na wazee walioipigania hadi ikapata uhuru.
"ACT-Wazalendo tutarudisha misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa hili na ndiyo maana kauli mbiu yetu ni Uhuru, Uzalendo na Uadilifu, vitu ambavyo vimepotea," alisema mgombea huyo wakati akinadi sera zake akirejea Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Chama hicho, ambacho leo kimezoa wanachama 150 kutoka CUF, kimeweka rekodi ya pekee kwa kusimamisha wagombea ubunge 219 kati ya viti 265 vilivyopo, kikiwa chama cha pili katika uchaguzi wa mwaka huu kilichosimamisha wagombea wengi baada ya CCM.
Bi. Mghwira alisema, chama chake kina watu makini na kwamba Zitto Kabwe, ambaye ndiye kiongozi mkuu wa chama hicho, anastahili kuwa waziri mkuu kwani juhudi zake zimeonekana katika kipindi cha miaka 10 aliyokaa bungeni.
Awali, Zitto akimkaribisha mgombea huyo pamoja na mgombea mwenza Hamad Mussa Yusuph, alisema sera za chama hicho zinatekelezeka na kwamba watahakikisha Watanzania hawapewi mzigo wa kodi unaochangia ugumu wa maisha, kwani siri wanayo.
"Serikali haikusanyi kodi kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, wapo wafanyabiashara wanaokwepa kodi kwa kuingiza bidhaa ambazo wanadai zinapelekwa nchi za jirani wakati zinabaki hapa hapa bila kulipiwa kodi," alisema.
Alisema, ukwepaji huo wa kodi unaikosesha serikali mapato ya Shs. 900 bilioni kila mwaka, hivyo wao wakiingia madarakani watahakikisha kazi ya kwanza ni kukusanya kodi hizo ili zitumike kujenga hospitali na huduma nyingine za jamii.
Zitto alisema kwamba, ufisadi umezidi katika serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo wiki mbili zilizopita kampuni moja ya Uswisi imepewa mkataba wa kuingiza mafuta kwa mkupuo (bulk petrol) wakati zabuni hiyo haikutangazwa.
"Katika mkataba huo inaonyesha kwamba pipa moja la mafuta linauzwa kwa senti za Dola 60 wakati kwenye soko la dunia pipa linauzwa senti za Dola 40, hii maana yake ni kwamba watu waliopiga dili watavuna bila jasho kiasi cha Shs. 20 bilioni huku wanaoumia wakiwa ni Watanzania wenyewe kwa kuwa bei ya mafuta haiwezi kushuka," alisema.
Naye mshauri wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo, aliwataka Watanzania kuichagua ACT-Wazalendo kwa kuwa sera zake zitairudisha heshima na taifa pamoja na misingi yake imara.
"Kuna wengine wanafuata mbwembwe za wanasiasa walaghai, hapa sisi tunanadi sera, kwa sababu taifa hili limepoteza misingi yake ikiwa ni pamoja na miiko ya viongozi," alisema.
Aidha, aliibeza kauli ya Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye kwamba rais wa nchi ni meneja tu.
Sumaye aliitoa kauli hiyo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni za Ukawa kwenye Viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kazi ya urais siyo kubeba zege.
"Inashangaza mtu aliyekaa ndani ya serikali kwa miaka mingi anathubutu kusema kwamba kazi ya urais ni umeneja, mtu wa namna hiyo akija mkataeni mwambieni hatutaki meneja wa miradi.
"Miaka 50 baada ya uhuru tumesomesha mameneja wengi, wahandisi wengi na kadhalika ambao wanaweza kuifanya kazi hiyo, Rais anatakiwa awe mbunifu, siyo mtu wa kusahau alichokisema jana. Tunataka mtu anayetoa kauli inayofanana juzi, jana, leo na kesho wala si mtu wa kukariri," alisema Profesa Mkumbo.
Aidha, aliongeza kwamba rais mbali ya kuwa mbunifu, asiwe mwenye papara katika kutoa maamuzi na alinde umoja na muungano pamoja na tunu zake.
No comments:
Post a Comment