Dk. John Pombe Magufuli (kulia), akigonga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakati wa mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma Julai 12, 2015 uliompitisha kuwa mgombea urais.
Na Daniel
Mbega wa www.brotherdanny.com
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeyavunja makundi na
kuweka mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 hasa baada ya kuona
upinzani umepata nguvu kubwa tangu Edward Lowassa alipokimbilia Ukawa baada ya
kutemwa Dodoma.
Na katika kudhihirisha kwamba CCM wameungana, Halmashauri
Kuu ya chama hicho iliyokutana jijini Dar es Salaam katika kikao cha siku moja
Agosti 17, 2015 imeunda Kamati ya Kampeni itakayomnadi mgombea wake Dk. John
Pombe Joseph Magufuli.
Ndani ya kamati hiyo yenye wajumbe 32, wamo makada
tisa ambao waligombea urais pamoja na Dk. Magufuli na wakashindwa pamoja na
Lowassa.
NEC, iliyokuwa chini ya mwenyekiti wake Dk. Jakaya
Kikwete, iwateua Bernad Membe, January Makamba na Dk. Asha-Rose Mtengeti Migiro
ambao walipenya kwenye tano bora pamoja na Dk. Magufuli huku Dk. Migiro akifika
fainali.
Wengine waliowania urais ambao sasa wamekabidhiwa
jukumu la kumnadi Dk. Magufuli ni Waziri wa Uchukuzi Samwel Sitta, Naibu Waziri
wa Fedha Mwigulu Nchemba, Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu, Waziri
wa Afrika Mashariki Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika
Steven Wasira na Mbunge wa Afrika Mashariki Charles Makongoro Nyerere.
Wajumbe
wengine kwenye kamati hiyo muhimu ni Abdulrahman Kinana (Mwenyekiti), Rajab
Luhwavi (Makamu Mwenyekiti – Bara), Vuai Ali Vuai (Makamu
Mwenyekiti - Z’bar), Sofia Simba, Mohamed Seif Khatib, Nape Nnauye, Amina
Makillagi, Christopher Ole Sendeka, Abdallah Majura Bulembo, Hadija Aboud, Mohamed
Aboud, Issa Haji Ussi, Waride Bakari Jabu na Mahmoud Thabit Kombo.
Wengine ni Shamsi Vuai Nahodha, Maua Daftari, Stephen
Masele, Pindi Chana, Shaka Shaka, Sadifa Juma Khamis, Antony Diallo, Livingston
Lusinde na Ummy Mwalimu.
Kwa
namna mchakato wa kuwania uteuzi wa kugombea urais ulivyokuwa na figisu figisu,
kuteuliwa kwa wajumbe hao tisa, ambao nao walikuwa na kambi zilizokuwa
zinasigana, kunamaanisha kwamba makundi hayo yamezikwa rasmi na sasa wote
wamekuwa chama kimoja kuhakikisha kwamba wanasaidia ili kiendelee kutawala.
Kuondoka
kwa Lowassa pamoja na makada wengi na wanachama kuelekea Chadema, kwa kiasi
kikubwa kumeifumbua macho CCM na kuona kwamba kama itaendelea na msuguano
inaweza kujikuta katika wakati mgumu, hasa kutokana na vuguvugu kubwa la
mageuzi lililopo upande wa pili.
Ingawa
haijajulikana majukumu ya kamati hiyo, lakini ni wazi kwamba ndiyo
itakayohusika na uratibu na utekelezaji wa shughuli zote za kampeni za urais
pamoja na kuweka mikakati thabiti ya kushinda viti vingi vya udiwani na ubunge,
ambavyo vinatishiwa na ujio wa Lowassa ndani ya Ukawa.
Wagombea
urais wengine ambao ni wazi pia watakuwa wameungana licha ya kutoteuliwa kwenye
kamati hiyo walikuwa Dk. Titus Kamani ambaye ameshindwa kwenye kura za
maoni Busega, Profesa Sospeter Muhongo, Balozi Amina Salum, Profesa Mark
Mwandosya, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa sasa Mizengo
Pinda, William Ngeleja, Peter Nyalali, Dk. Khamis Kigwangalla, Luhaga Mpina
ambaye amekosa mpinzani ndani ya CCM katika Jimbo la Kisesa.
Wengine walikuwa Dk. Augustine Mahiga, Dk. Mwele Malecela, Elidephonce
Bihole, Dk. Hassy Kitine, Joseph Chagama, Balozi Ali Karume, Maliki Malupu, Dk.
Mohamed Ghalib Bilal, Amos Siyantemi, Jaji Augustino Ramadhani, Dk. Mussa
Kalokola, Ritta Ngowi, Monica Mbega, Nicholas Mulenda, Banda Sonoko, Helen
Elinawinga, Mathias Chikawe, Antony Chalamila, Veronica Kazimoto na Peter
Nyalali.
(Imeandaliwa
na www.brotherdanny.com)

No comments:
Post a Comment