Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Monday, 17 August 2015

BARAZA LA MAWAZIRI LA CCM OKTOBA: KIGODA WAZIRI MKUU, MWIGULU NCHEMBA WAZIRI WA FEDHA!

Dk. Abdallah Omar Kigoda - kuwa Waziri Mkuu
Mwigulu Lameck Madelu Nchemba - kuwa Waziri wa Fedha 

 Celina Ompeshi Kombani - Mazingira
 Jenista Joachim Mhagama - Utumishi

 Na Daniel Mbega

WAKATI siku 64 za mtifuano wa kampeni zinatarajiwa kuanza Agosti 22 kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), watakaounda Baraza la Mawaziri la Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 wamekwishaanza kutajwa, imefahamika. 
Duru za siasa kutoka chama hicho kikongwe kabisa barani Afrika zinasema, licha ya vuguvugu kubwa la mageuzi lililopo nchini, lakini wana uhakika wa kukamata tena dola na sasa wanapanga mikakati madhubuti ya kutetea majimbo yao na kuyarejesha yaliyotwaliwa na upinzani.
Baraza hilo linaelezwa kuwa na uwiano sawa wa jinsia katika harakati za CCM kutimiza malengo ya “nusu-kwa-nusu” katika uongozi, kama alivyofanya mgombea urais Dk. John Magufuli alipomteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza.
Kwa mujibu wa duru hizo, wakati tayari mgombea urais na mwenza wake wamejulikana, hivi sasa wanaangalia ni nani kati ya makada wake ambaye anaweza kuwa waziri mkuu baada ya chama hicho kurejea madarakani.
“Baada ya Oktoba Rais ni Dk. (John) Magufuli na makamu wake ni Samia (Suluhu Hassan), sasa tunaangazia nani atakayeweza kuwa mtendaji mkuu wa serikali ingawa tayari tumemuona,” kinasema chanzo kimoja ndani ya CCM.
Ingawa chanzo hicho kimegoma kumtaja mtu wanayedhani atakuwa waziri mkuu, lakini taarifa zinasema, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Omar Kigoda, ndiye anayelengwa kushika wadhifa huo.
“Huyu jamaa ndiye waziri mkongwe kuliko wote, ameshika wizara nyingi na anaweza kusimamia vyema utendaji wa serikali,” kilieleza chanzo kingine.
Mbali ya Dk. Kigoda, mwingine anayetajwa kukabidhiwa wizara nyeti ya fedha ni Mwigulu Lameck Madelu Nchemba, ambaye kwa sasa anatetea kiti chake katika Jimbo la Iramba Magharibi.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Nchemba, ambaye ni naibu waziri wa fedha anayeshughulikia uchumi, anafaa kupewa nafasi hiyo kwani katika kipindi cha wiki mbili tu baada ya kuteuliwa aliweza kukusanya kodi zaidi ya Shs. 3 bilioni kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wanatajwa kwamba wamekuwa wakwepaji sugu wa kodi.
“Huyu jamaa ndiye hasa anayestahili kukaa kwenye ofisi ile, amewahi kufanya kazi Benki Kuu na zaidi ni mtendaji, ukiangalia utendaji wake katika kipindi cha tangu Januari 2014 hadi sasa unaweza kuamini kwamba ndiye hasa anayefaa,” kilisema chanzo kingine.
Hata hivyo, licha ya baraza hilo kuwa na uwiano sawa wa jinsia, lakini taarifa zinasema litakuwa na sura nyingi ngeni na wachache wa zamani.
Ifuatayo ni orodha pendekezwa ya baadhi ya wizara za sasa:
Waziri katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora): George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi).
Waziri Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma): Jenista Mhagama.
Waziri katika Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu): Profesa Jumanne Maghembe ambaye kwa sasa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge): Steven Masatu Wasira ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi): Aggrey Mwanri, Mbunge wa Siha mkoani Kilimanjaro ambaye kwa sasa ni naibu waziri katika wizara hiyo na utendaji wake umekuwa ukimfunika hata waziri mwenyewe.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira): Celina Ompeshi Kombani, ambaye amekuwa kwenye baraza la mawaziri kwamuda mrefu.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano): Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ambaye pia amewahi kuongoza wizara kadhaa za Muungano zikiwemo Ulinzi na JKT pamoja na Mambo ya Ndani.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji): Saada Mkuya, ambaye alikuwa waziri wa fedha.
Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango: Mwigulu Lameck Madelu Nchemba, naibu waziri kwenye wizara hiyo anayeshughulikia uchumi.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi: Dk. Shukuru Kawambwa anatajwa kwamba anaweza kurejea kwenye wizara hiyo aliyoiongoza kwa muda mrefu.
Waziri wa Maliasili na Utalii: Mahmoud Mgimwa, naibu waziri wa sasa katika wizara hiyo ambaye anatetea kiti chake katika Jimbo la Mufindi Kaskazini.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi: William Vangimembe Lukuvi, ambaye tangu alipoteuliwa kwenye nafasi hiyo ameweza kusaidia kutatua migogoro mingi ya ardhi mikoani huku mwenyewe akisimamia kupokea malalamiko ya wananchi hao.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto: Ummy Mwalimu, alipata kuwa naibu waziri katika wizara hiyo pia.
Wizara ya Katiba na Sheria: Angela Kairuki ambaye kwa sasa ni naibu waziri katika wizara hiyo.
Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko: Mary Michael Nagu, anayewania Jimbo la Hanang’ mkoani Manyara.
Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu: January Yussuf Makamba, Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga na naibu waziri katika wizara hiyo.
Wizara ya Kazi na Ajira: Anne Kilango Malecela, ambaye licha ya kuwa naibu waziri kwa sasa, lakini suala la ajira amekuwa akilipigia kelele muda mrefu. Anafaa kuiongoza wizara hiyo.
Wizara ya Habari, Michezo, Utamaduni na Vijana: Dk. Fenella Mukangara ambaye anawania ubunge katika Jimbo la Kibamba mkoani Dar es Salaam.
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa: Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi, ambaye anawania ubunge katika Jimbo la Kwahani, Zanzibar. Ndiye anayeiongoza wizara hiyo.
Wizara ya Mambo ya Ndani: Adadi Rajabu, Mkurugenzi wa zamani wa Makosa ya Jinai ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Wizara ya Nishati na Madini: George Simbachawene, waziri wa sasa katika wizara hiyo.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii: Dk. Stephen Kebwe, ambaye kwa sasa ndiye Naibu Waziri.
Wizara ya Ujenzi: Dk. Harrison George Mwakyembe, ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wizara ya Uchukuzi: Job Yustino Ndugai, ambaye amekuwa naibu spika kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika: Dk. Mathayo David Mathayo ambaye aliwahi kuiongoza wizara hiyo.
Wizara ya Maji na Umwagiliaji: Dk. Christine Ishengoma, amekuwa mbunge na mkuu wa mkoa kwamuda sasa na ni mhadhili wa zamani katika Chuo Kikuu cha Kilimocha Sokoine.
Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki: Balozi Khamis Kagasheki, japokuwa alijiuzulu katika Wizara ya Maliasili na Utalii kufuatia kashfa ya Operesheni Tokomeza, lakini bado anatajwa kama kiongozi makini anayeweza kuiongoza wizara hiyo.
Wiziri ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi: Dk. Titus Kamani, ambaye ndiye alikuwa akiiongoza wizara hiyo. Ingawa ameshindwa na Dk. Raphael Chegeni kwenye kura za maoni Jimbo la Busega, lakini bado anaweza kuteuliwa kupitia kwenye 'kapu'.
Wengine wanaotajwa kuwemo kwenye baraza la mawaziri wakiwa naibu mawaziri na wizara husika kwenye mabano ni Kassim Majaliwa (Tamisemi), Margaret Mkanga (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Namelock Sokoine (Maendeleo ya Mifugo), Mariam Reuben Kasembe (Elimu), Dk. Charles Tizeba (Uchukuzi), Dk. Suzan Kolimba (Wizara ya Afya), Lucy Mayenga (Ardhi), Daniel Mtuka (Mambo ya Ndani), Prudensia Kikwembe (Tamisemi) na Godfrey Zambi (Kilimo).


 IMECHAPWA MARA YA KWANZA NA GAZETI LA WAJIBIKA AGOSTI 17, 2015

No comments:

Post a Comment