(Inaendelea kutoka jana)
DODOMA 12.11:1993
Nadhani
uamuzi wa kuitisha kikao cha mchanganyiko ulifanywa na viongozi wetu katika
kikao cha Dodoma II. Nimesema awali kwamba Waziri Mkuu alipohisi kuwa baadhi ya
mawaziri wenzake walikuwa wanaunga mkono hoja ya Utanganyika, na yeye kwa
wakati huo alikuwa hajui aiunge mkono au aipinge, alipendekeza ifanyike semina
ya viongozi wote ili jambo hili lizungumzwe na lipingwe nje ya Bunge.
Viongozi
ambao wangehudhuria katika semina hiyo ndio walioalikwa kuja katika kikao cha
mchanganyiko cha Dodoma. Lakini shabaha ya kuwakutanisha ilikuwa imebadilika.
Kama semina ya awali ingefanyika, shabaha yake ilikuwa ni kupinga hoja ya
Wabunge, na mimi niliombwa niende nisaidie. Kamati Kuu ya CCM ikaamua kuwa
hapakuwa na haja ya kufanya semina hiyo. Lakini baada ya kuona msimamo wa
Halmashauri Kuu ya Taifa na ugumu wa kushawishi wajumbe wake wakubali hoja ya
Serikali Tatu, viongozi wetu walifufua tena wazo la semina.
Huenda
waliona wanahitaji msaada, na kwa kuwa sasa hoja ni ya wabuge wote, walihisi
kuwa itafaa itafutwe njia ya kuikutanisha Halmashauri Kuu ya Taifa pamoja na
wabunge wote. Na kwa kuwa isingetoa sura nzuri kuita wabunge peke yao,
ikapendekezwa kuwa Serikali ya Mapinduzi na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
nao waitwe!
Mazungumzo
na maamuzi ya kikao hicho cha mchanganyiko yanafahamika vizuri zaidi, na hayana
haja ya kuelezwa sana. Inatosha kusema kuwa wote walikubaliana, na baada ya
mjadala wa wazi wazi, kwamba sera ya Serikali Mbili ni sera ya Chama Cha
Mapinduzi. Wakapendekeza kuwa suala hili lizungumzwe na wanachama wa CCM ili
tupate maoni yao. Ni aina ya referendamu, lakini badala ya kutafuta maoni ya
wananchi wote, waulizwe wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kama wanataka,
(i) Tubaki
na Sera ya Serikali Mbili;
(ii)
Tuibadili na kuwa na sera ya Serikali Tatu; au
(iii)
Tuibadili na kuwa na sera ya Serikali Moja
Jambo hili
yafaa lisisitizwe.
Viongozi
wetu, kama kawaida yao, walipachika maneno "haja ya kuwa na Serikali ya
Tanganyika," katika mapendekezo ya kikao cha pamoja. Hizo ni hila;
maelewano sivyo yalivyokuwa. Mapendekezo ni kwamba sera ya Serikali Mbili,
izungumzwe ndani ya Chama ili kuona kama pana haja ya kuibadili.
Kikao kile
hakikusema kuwa endapo wanachama wetu wataamua kubadili sera ya Serikali Mbili,
basi wazingatie hoja na haja ya kuwa na Serikali Tatu. Kwa bahati njema maswali
waliyoulizwa wanachama wa CCM yanazingatia na kuheshimu uhuru wao, bila kujali
hila hizi za viongozi.
Hapo ndipo
tulipo hivi sasa. Mimi nitashangaa kabisa ikiwa wanachama wa CCM watasema kuwa
wanataka Serikali ya Tanganyika. Iwafanyie kazi gani ambayo haiwezi kufanyika
hivi sasa? Na kuvunja Muungano kutawafaa nini, wao na raia wenzao? Na wana
uhasama gani na Wazanzibari, au wamewafanyia nini hata waseme wamechoka nao?
III HAJA YA KUWAJIBIKA
Kabla ya
kuondoka Dodoma kwenda Dar es salaam ambako nilionana na watangazaji wa habari
baadaye, nilipata nafasi ya kuzungumza na Rais kuhusu matokeo ya mkutano wa
pamoja, na nini la kufanya. Nilimweleza maoni yangu. Kwa kuwa mazungumzo haya
yanayotakiwa yafanywe na wanachama wa CCM ni ya kusukumizwa, na hayana maelezo,
si busara kufanya haraka. Ilikuwa imetangazwa kuwa Rais atateua kamati ya
kuratibu maoni ya wananchi. Nilitazamia kuwa badala yake atateua kamati ya
kusimamia utaratibu wa kupata maoni ya wanachama. Nilishauri ateue kamati ya
watu makini; iongozwe na mtu mwenye busara, iandae maelezo yatakayokuwa
mwongozo wa mazungumzo yatakayofanywa na wanachama wa CCM. Wanachama hawana
budi waelezwe kwa nini tunataka wazungumze muundo wa Muungano. Lazima tueleze
tena asili ya muundo wa Serikali Mbili. Tuwasaidie wanachama, na wananchi kwa
jumla, kuelewa sababu za muundo huo; uzuri wake na upungufu wake.
Lazima
tueleze ni upungufu gani tunadhani unatokana na muundo wenyewe, na ni upungufu
gani unaotokana na utekelezaji tu. Lazima tuchambue namna mbali mbali za
kuendesha Muungano; jinsi ya kurekebisha muundo wa Serikali Mbili, na jinsi ya
kuondoa upungufu unaotokana na utekelezaji. Kamati hiyo ingeweza kusaidiwa na
kazi ambayo imeanzwa na kamati mbali mbali za Chama na Serikali.
Kama
itaonekana kuwa muundo wa Serikali Mbili lazima uachwe, hatuna budi tuchambue
na kueleza faida na hasara za miundo mbali mbali: muundo wa Serikali Moja, na
muundo wa SerikaIi Tatu. Tunaweza, tukipenda, kuchambua na kueleza pia faida na
hasara za kuwa na muundo wa Serikali zaidi ya Tatu.
Kinachopendekezwa
na washabiki wa Serikali Tatu ni Muundo wa Shirikisho. Wako watu wanaoamini
kwamba ni rahisi zaidi kuwa na Shirikisho la Zanzibar yenye Serikali Moja na
Tanganyika yenye Serikali zaidi ya moja, kuliko kuwa na Shirikisho la Zanzibar
yenye Serikali Moja na Tanganyika yenye Serikali Moja.
Yote haya
yanatakiwa yachambuliwe na kuelezwa vizuri kabisa. Na wakati huo huo maelezo
hayo hayana budi yasisitize historia na mwelekeo wa nchi yetu, na Chama Cha
Mapinduzi. Historia yetu na mwelekeo wetu mpaka sasa umekuwa ni wa kuimarisha
Muungano.
Kama
tunaona kuwa inafaa kuacha muundo wa Serikali Mbili hatuna budi tuseme wazi
wazi katika Mwongozo huo kwamba kwa maoni ya uongozi wa Chama muundo unaoweza
kuendeleza historia na mwelekeo wa nchi yetu, ni muundo wa Muungano wa Serikali
Moja. Uongozi wa Chama hauwezi kusema kuwa hauna maoni yake, ila unasubiri
maoni ya wanachama! Kuongoza ni kuonyesha njia.
Baadaye
wanachama wa CCM walipoombwa watoe maoni yao kuhusu suala hili, hapakuwa na
maelezo wala mwongozo kama huo. Sababu zinazotolewa ni kwamba viongozi wetu
hawakutaka waonekane kama wanawashawishi au kuwalazimisha wanachama kufuata
msimamo fulani. Nadhani ukweli ni kwamba viongozi wetu walidhani kuwa sera ya
Chama isipokuwa na mtetezi wake, na uwanja ukaachwa wazi kwa washabiki wa
Serikali Tatu, basi wanachama wa CCM watakubali hoja ya Utanganyika. Lakini
hata bila maelezo hayo na mwongozo huo siamini hata kidogo kwamba wanachama wa
CCM watakubali hoja ya Serikali Tatu.
llikuwa ni
dhahiri kwamba kazi hii haiwezi kufanywa chini ya usimamizi wa viongozi
waliopo. Hawa sasa wanaona kuwa heshima yao na "nyuso" zao, na labda
baadaye zao, zinawadai watetee msimamo wa Serikali Tatu. Hawawezi kutetea sera
ya Chama ya Serikali Mbili, wala mwelekeo wa Chama wa Serikali Moja. Watatumia
uwezo walia nao kutokana na hadhi walizo nazo, kuvuruga sera ya Chama na
mwelekeo wake. Tutahitaji kiongozi mpya wa Serikali, na kiongozi mpya wa Chama.
MAANA YA MANENO:
Neno la
Kiingereza "resign", lina
maana mbili:-
(i) to give up or surrender (one's job or
property or claim etc.). Ni kuacha au kuachia; kama kuacha au kuachia,
(kazi, au mali au haki, au madai n.k.). Maana ya "give up"; to cease (doing something); to part with; to
surrender; to abandon hope; to declare a person to be incurable or a problem to
be too difficult for oneself to solve. Ni kuacha (kufanya jambo); kuachia
au kuachana na; kusalimu amri; kukata tamaa; kusema kuwa mtu hatibiki au tatizo
fulani linakushinda kutatua.
Maana ya "Surrender": (1) to hand over, to
give into another person's power or control, especially on demand or under
compulsion. Ni kutoa kwa, au kumwachia mwingine uwezo au mamlaka, hasa kwa
kudaiwa au kulazimishwa. (2) to give
oneself up, to accept an enemy's demand for submission. Ni kusalimu amri,
kukubali amri ya adui ya kujitolea. Hayo ndiyo maelezo ya maana ya kwanza ya
neno "resign," yaani
“jiuzulu".
(ii)Maana
ya pili: "Resign onself to": to
be ready to accept or endure, accept as inevitable. Ni kuwa tayari kukubali
na kustahimili; kukubali kuwa jambo fulani ni lazima liwe, halizuiliki. Ni
kukubali kuwa umeshindwa au utashindwa, na kuwa tayari kustahimili matokeo ya
kushindwa. Ni kukubali kusalimu amri ya adui au mpinzani wako na kuwa tayari
kustahimili matokeo yake. Ni kukubali kutekwa, na kuwa tayari kustahimili
matokeo ya kuwa mateka. Nikukubali kushindwa; ni kubwaga silaha. Mkazo katika
maana hii ya pili ni kule kukubali kustahirnili matokeo ya kukata tamaa na
kubwaga silaha.
Itaendelea
kesho…

No comments:
Post a Comment