Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba.
Dodoma. Mambo yamebadilika. Ukimya ulitawala jana katika Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, baada ya wabunge zaidi ya 200 ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vya Bunge hilo.
Ilikuwa ni saa 10:31 jioni baada ya Mjumbe wa Bunge hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alipohitimisha uchangiaji wake akisema: “Ukawa hatuwezi kuendelea kushiriki dhuluma dhidi ya wananchi kwa kupitisha Katiba ambayo ni kinyume cha matakwa yao.”
Baada ya kauli hiyo aliondoka akifuatiwa na Mwenyekiti wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na wajumbe wao kutoka nje ya Bunge.
Ukimya ulitawala takriban dakika mbili hivi na baada ya wajumbe hao kutoka, Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samia SuluhuHassan aliwaelekeza makatibu kuhesabu wajumbe ili kuona kama akidi imetimia ili waendelee na kikao.
Baadaye aliliambia Bunge kuwa makatibu wamemweleza hawahitaji akidi kwa kuwa kikao kilikuwa kinaendelea wakati Ukawa walipotoka nje ya ukumbi.
Hotuba ya Lipumba
Profesa Lipumba alianza kwa kunukuu Gazeti la Mwananchi la Aprili 14, mwaka huu katika sehemu inayosema; “Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge) ameanza kampeni kanisani kwa kuwataka wananchi kupinga serikali tatuzilizopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, vinginevyo nchi itatawaliwa na jeshi kwa kuwa serikali ya muungano itashindwa kuwalipa mishahara wanajeshi.”
Alisema yeye ni muumini wa dini ya Mwenyezi Mungu lakini anaafiki mapendekezo yaliyoletwa bungeni hapo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoundwa na Rais.
“Hii ni kauli ya Waziri Lukuvi ndani ya Kanisa la Methodist wakati wa sherehe ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu na Waziri Lukuvi alikuwa anamwakilisha Waziri Mkuu.”
Alisema inasikitisha kwa sababu kauli hiyo inafanana na ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati akihutubia Bunge Maalumu.
Alisema kauli za Lukuvi zinatisha baada ya kusema Wazanzibari ambao wanataka kuwa na nchi yao hawawezi kujitegemea, bali wanataka wapate nafasi ya kujitangazia kuwa ni nchi ya Kiislamu.
“Waziri anaweza kusema hivyo ndani ya kanisa? Kawahamasisha mpaka yule kiongozi wa kanisa akasema ili kudumisha Muungano bora Katiba ya Zanzibar ifutwe ili iwepo moja ya nchi moja ambayo inadumisha Muungano,” alisema.
Alisema Lukuvi alikuwa akiwaaminisha kuwa mfumo wa serikali tatu ukipita kutakuwa na mapinduzi na nchi haitatawalika na hivyo watu watashindwa kwenda kusali makanisani.
“Kama ndugu zetu wa Zanzibar wangekuwa wanahitaji serikali moja tungekuwa na utaratibu mzuri tu, lakini siyo wanachama wa CUF, siyo wa CCM, Wazanzibari wote hawataki muungano wa serikali moja,” alisema.
Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa mapendekezo ya serikali tatu kutokana na ukweli huo. “Hoja zilizoletwa hapa ni hoja za serikali moja, si hoja za serikali mbili lakini wenzetu moja hawataki, kwa hiyo tunahitaji Muungano ambao tutakuwa na maridhiano ya pande zote mbili,”
“Wengi wamenukuu makala niliyoitoa katika kituo cha TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania), ambayo iliunda Baraza la Katiba na mimi nilichambua mapendekezo ya Tume nikasema kwa mapendekezo yaliyomo ndani ya Rasimu ya Katiba hayatakidhi mapato ya shirikisho.”
Alisema wajumbe wanaomnukuu wanaishia hapo bila kwenda katika mapendekezo aliyoyatoa.
“Wamenisifu sana ni mchumi mahiri, basi waendeleze sifa hizo kwa mapendekezo niliyoyatoa ya mapato ya kukidhi uendeshaji wa serikali ya shirikisho.
“Nimeeleza katika hali halisi kuwa utaratibu mzuri ni mapato ya kila serikali kuchangia katika shirikisho na mambo haya yaandikwe katika Katiba. Katiba inaweza ikasema wazi asilimia 20 ya mapato yote yanayokusanywa Zanzibar au Tanganyika yataenda kwenye shirikisho.”
Alitaka pia kuwekwa kwa misingi mizuri ya kukusanya kodi na kutumia fedha za wananchi ndani ya katiba ya muungano ambayo ndiyo katibamama.
“Lakini ndugu zangu mjadala wetu unavyokwenda utadhani kuwa Rasimu ya Katiba iliyoletwa imeletwa na CUF au na Chadema au na NCCR-Mageuzi, au Wapemba,” alisema.
Alisema ukurasa wa kwanza wa Rasimu ya Katiba unaeleza kuwa toleo hili la Rasimu ya Katiba lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kwa mujibu wa Kifungu cha 20(2) ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83.
Alisema hiyo ni rasimu ya Tume ya Rais na si rasimu ya Wapemba.
Hata hivyo, alisema mjadala unaoendelea bungeni umekuwa na utaratibu wa ubaguzi... “Watu wamebaguliwa humu na viongozi wakubwa wanapiga makofi, Bunge hili limekuwa kama Bunge la Intarahamwe. Hii ni hatari kwa nchi yetu. Wapemba, Waarabu, Wahindi, Wakongo,” alisema.
“Hii hatuhitaji, tunahitaji katiba ambayo itahakikisha kila mwananchi anapata haki yake wote tuwe sawa bila kujali rangi zetu, jinsia zetu, makabila yetu, huu ndiyo msingi aliotuachia Mwalimu Nyerere tuenzi msingi huo.”
Alilalamikia kile alichokiita kuwa ni ubaguzi ndani ya Bunge na kwamba kama Serikali haikutaka Katiba Mpya kwa nini imepeleka wabunge Dodoma? Pia alihoji ni kwa nini ilitumia Sh70 bilioni katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa nini mmetufikisha hapa? Jengo hili nimeambiwa limekarabatiwa kwa Sh8.2 bilioni hali hamuamini Rasimu ya Katiba ama ilikuwa ni utaratibu wa kupata hizo asilimia 10, ndiyo maana mmekarabati kwa gharama kubwa?” alisema.
“Tunataka CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali), akague matumizi ya fedha zilizotumika. Utatumiaje fedha nyingi wakati hiyo katiba iliyowasilishwa kumbe huitaki kabisa.
“Hakuna utaratibu wowote wa kupiga kura na kufanya maamuzi kuhusu sura hizi mbili. Tumechoka kusikiliza matusi. Tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi, hatuwezi kuwa sehemu ya kundi linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania hili hatukubali,” alisema.
No comments:
Post a Comment