Gavrilo Princip, muuaji wa Mfalme Franz Ferdinand
Mfalme Franz Ferdinand
Na Daniel MbegaVITA Kuu ya Kwanza ya Dunia (WWI), ilianzia na kuhusisha mataifa ya Ulaya lakini ikasambaa ulimwenguni kote. Vita hii ilianza Julai 28, 1914 na kufikia tamati Novemba 11, 1918. Tangu kuanza kwa vita hiyo hadi kuibuka tena kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1939, ilikuwa inafahamika tu kama Vita Kuu. Zaidi ya wanajeshi milioni 9 waliuawa. Huo ulikuwa mgogoro wa tano mkubwa zaidi katika historia ya dunia, na kufungua mlango wa mabadiliko makubwa ya kisiasa, yakiwemo mapinduzi katika mataifa mengi yaliyohusika.
Vita hivi vilihusisha mataifa yote yaliyokuwa na nguvu za kiuchumi duniani, ambayo yalikuwa katika pande mbili zinazopingana kulingana na uchumi wao: Majeshi ya Washirika (yaliyotokana na Mkutano wa Utatu wa Uingereza, Ufaransa na Dola ya Russia) na Majeshi ya Kati (Central Powers) yaliyoundwa na Ujerumani na Austria-Hungaria. Ingawa Italia ilikuwa mjumbe wa Muungano wa Majeshi ya Kati pamoja na Ujerumani na Austria-Hungaria, haikuweza kuungana nayo kwani Austria-Hungaria ilikuwa imekiuka masharti ya umoja huo.
Majeshi hayo ya pande mbili yalikuwa yameundwa na kutanuka kadiri mataifa mengi yalivyoingia kwenye vita hivyo: Italia, Japan na Marekani wakajiunga na Majeshi ya Washirika (Allies), na Dola ya Ottoman na Bulgaria wakajiunga na Majeshi ya Kati. Maofisa milioni 70 wa kijeshi, wakiwemo milioni 60 kutoka Ulaya, wakajipanga katika mojawapo ya vita vikubwa kabisa katika historia ya dunia.
KUUAWA KWA MFALME FRANZ FERDINAND
Daraja mjini Sarajevo ambapo Mfalme Ferdinand na mkewe Sophie waliuawa Juni 28, 1914
Japokuwa kuibuka kwa ubepari kulikuwa
sababu ya msingi ya vita hivyo, lakini chanzo kikubwa kilikuwa ni tukio
la Juni 28, 1914 la kuuawa kwa Archiduke Franz Ferdinand wa Austria,
mrithi wa taji la ufalme la Austira-Hungaria. Ferdinand aliuawa mjini
Sarajevo, Yugoslavia na manafunzi mwanaharakati Gavrilo Princip. Hii
ilileta mgogoro wa kidiplomasia wakati Austria-Hungaria ilipopeleka
sharti (ultimatum) kwa Ufalme wa Serbia, na umoja wa kimataifa uliokuwa
umeundwa miongo kadhaa nyuma ukavunjika. Ndani ya wiki chache tu,
mataifa makubwa yalikuwa vitani na mgogoro ukasambaa haraka dunia nzima.Mnamo Juni 28, 1914, Mfalme Mkuu Franz Ferdinand wa Austria, ambaye alikuwa ndiye mrithi wa taji la ufalme la Austro-Hungaria, na mkewe Sophie, Duchess wa Hohenberg, waliuawa mjini Sarajevo na Gavrilo Princip, mmoja wa kundi la wauaji sita (watano Waserbia na mmoja Mwislamu wa Bosnia), mauaji yaliyoratibiwa na Danilo Ilic.
Madhumuni ya kisiasa ya mauaji hayo yalikuwa kuyavunja majimbo ya Slavia ya kusini katika himaya ya Austro-Hungaria ili yaungane na Serbia Kuu au Yugoslavia. Maofisa wa kijeshi wa Serbia walikuwa nyuma ya mauaji hayo yaliyoendeshwa katika harakati za Young Bosnia.
Mauaji hayo yalisababisha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia wakati Austira-Hungaria ilipotoa sharti la mwisho dhidi ya Serbia, ambalo lilikataliwa. Austria-Hungaria ikatangaza vita, na ndipo vita hasa ilipoibuka.
Kati ya maofisa wa jeshi la Serbia waliokuwa nyuma ya mpango huo walikuwemo Mkuu wa Ujasusi wa Kijeshi wa Serbia Dragutin Dimitrivajec, msaidizi wake wa karibu Meja Vojislav Tankosic, na Jasusi mkuu Rade Malobabić. Meja Tankosić aliwapatia wauaji mabomu na bastola na kuwapa mafunzo. Wauaji hao walipewa fursa kuingia katika mtandao maalum na kutumia nyumba za siri na mawakala wa usalama ambao Rade Malobabić aliwatumia wakati akipenyeza silaha na shughuli zake ndani ya Austria-Hungaria.
Wauaji hao, wafuasi wa mtandao ya kijasusi, na maofisa wa jeshi la Serbia waliohusika ambao walikuwa hai bado, walikamatwa, wakashtakiwa, wakakutwa na makosa na kudhibiwa. Waliokamatwa Bosnia walishtakiwa Sarajevu Oktoba 1914. Wengine walishtakiwa kwenye mahakama ya kangaroo ya Kiserbia katika eneo la Salonika Front lililokuwa linamilikiwa na Ufaransa kati ya mwaka 1916-1917 kwa mashtaka ya uongo yalisiyohusiana na mauaji hayo; Serbia iliwanyonga maofisa watatu wa jeshi.
Itaendelea kesho...
http://www.mjengwablog.com/habari-za-kijamii/item/10354-miaka-100-ya-ww1-mwanafunzi-alivyosababisha-vita-kuu-ya-kwanza-ya-dunia.html
No comments:
Post a Comment