Msimamizi msaidizi wa mradi wa maji wenye
thamani ya Shs. 152 milioni, Baltazar Mtenga (kushoto) kutoka kampuni ya Ifango
General Enterprises, akielezea changamoto za kukwama kwa mradi huo mbele ya
Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mbagala Charambe Machinjioni, Shaibu Omari Naputa
(kulia) na Mwenyekiti wa Mtaa wa Machinjioni A, Mkonge Hassan Katani (wa pili
kulia) wakati Halmashauri Kuu ya tawi hilo ilipofanya ziara kukagua miradi ya
maendeleo mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu
HALMASHAURI ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tawi la Charambe Machinjioni
katika Jimbo la Mbagala mkoani Dar es Salaam imeonyesha kukerwa na
ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi miwili ya maji yenye thamani ya zaidi ya
Shs. 170 milioni.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika ziara ya kukagua miradi
ya maendeleo iliyoko katika Mtaa wa Machinjioni A, Mwenyekiti wa CCM wa tawi
hilo, Shaibu Omari Naputa, alisema kutokamilika kwa miradi hiyo muhimu kunaitia
doa Serikali ya CCM, ambayo imedhamiria kuwaletea wananchi maendeleo.
Miradi hiyo ya maji, mmoja ukitekelezwa na Halmashauri ya
Wilaya na mwingine ukiwa umefadhiliwa na Ofisi ya Jimbo, ingeweza kuwahudumia
wakazi zaidi ya 30,000 jimboni humo, ambao kwa sasa wanapata shida kubwa ya
kupata huduma hiyo.
“Miradi hii ilikuwa ikamilike zaidi ya mwaka mmoja ulipita,
lakini mpaka sasa ujenzi unasuasua huku mradi unaofadhiliwa na Ofisi ya Jimbo
ukiwa umekwama na vifaa kung’olewa,” alisema Naputa.
Katika mradi wa kwanza ambao ulikuwa chini ya taasisi ya
CHADEA kabla ya Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuuchukua, ulitengewa
takriban Shs. 152 milioni ili kuupanua kwa kujenga tenki kubwa na vituo vitano
vya kusambazia maji pamoja na pampu, lakini badala ya kukamilika Mei mwaka
2018, mpaka sasa hata ujenzi wa tenki haujakamilika.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Mkonge Hassan Katani
ambaye aliongoza ziara hiyo, alisema kwamba, kwa vile wasimamizi wakubwa ni
Halmashauri ya Manispaa yeye hana mamlaka ya moja kwa moja ya kuwahimiza
wakandarasi wamalize haraka ujenzi, kwani licha ya mradi huo kuwepo mtaani
kwake, hajui hata mikataba yao ikoje.
“Nimekuwa nikiwaulizia tu wakandarasi, lakini wanatoa sababu
kwamba hawajapatiwa fedha kutoka halmashauri, sasa kwa sababu halmashauri
wenyewe ndio wasimamizi, inakuwa vigumu kwangu kuwahimiza," alisema.
Msimamizi msaidizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Ifango
General Enterprises, Baltazar Mtenga, alisema kinachokwamisha ni fungu la fedha
kuchelewa kutoka halmashauri.
Alikiri kwamba, mradi huo ulikuwa ukamilike tangu Mei 2018,
lakini mkandarasi akaomba kuongezewa muda kutokana na sababu mbalimbali,
ikiwemo kuchelewa kupewa fedha na halmashauri.
“Fedha zinatolewa kwa awamu, kila tunapojenga lazima waje
wakague halafu waidhinishe fungu jingine, lakini kuna kipindi tulisubiri kwa
karibu miezi mitatu bila kupata fedha, jambo ambalo linakwamisha utekelezaji.
“Tukipata fedha tunaweza kukamilisha ujenzi ndani ya mwezi
mmoja,” alisema Mtenga wakati ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kujaza lita 45,000
za maji ukiendelea.
Kwa upande wake, Naputa amemuagiza mkandarasi kuhakikisha
anakamilisha mradi huo ndani ya mwezi mmoja kwani mpaka sasa ni mwaka mzima
tangu mradi huo ulipokuwa ukamilike.
Aidha, amemuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa
kuhakikisha anaidhinisha fedha kwa wakati ili wananchi wasiendelee kuteseka
kutafuta huduma ya maji.
Kuhusu mradi wa maji uliokuwa utekelezwe na Ofisi ya Jimbo,
Mwenyekiti wa Mtaa Bw. Katani alisema kwamba, ulitumia kiasi cha Shs. 24
milioni, lakini tangu kisima kilipochimbwa miaka mitatu iliyopita hakikuweza
kutumika hadi Mei 2018 walipofunga pampu.
“Pampu ilipofungwa ikaanza kuvuta tope badala ya maji,
kwahiyo hapa maji hayajatoka ingawa miundombinu yote ilikuwa imekamilika
ikiwemo tenki na kituo cha kutolea maji.
“Baada ya kuona hivyo, Mbunge wa Jimbo la Mbagala, Ally
Mangungu, aliamua kuja kung’oa pampu na nyaya za umeme kwa kuhofia zingeweza
kuibiwa, lakini mpaka sasa sijui vifaa hivyo vilivyong’olewa viko wapi japokuwa
alisema angeibadilisha pampu,” alisema Katani.
Kwa upande wake, Naputa alisema kwamba, anaamini fedha hizo
za Mfuko wa Jimbo hazijawasaidia wananchi wa Mbagala, akaitaka Ofisi ya Jimbo
iwajibike kwa sababu hasara iliyotokea imetokana na uzembe.
Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na ujenzi wa Ofisi ya
Serikali ya Mtaa na Barabara ya Charambe-Buza ambao haujaanza licha ya kwamba
tayari wakazi wote wamekwishalipwa fidia kupisha barabara hiyo.
Katani alisema, ikiwa barabara hiyo yenye urefu wa takriban
kilometa 3 itakamilika basi itakuwa mkombozi kwa wananchi wengi na kupunguza
msongamano, kwani magari, hasa yanayokwenda Tandika, Buza na Uwanja wa Ndege
hayatalazimika kuzungukia Temeke.
Kuhusu ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa, wana-CCM hao
wameonyesha mashaka ya matumizi ya Shs. 8 milioni zilizotolewa na Halmashauri
ya Manispaa na kusimamiwa na Ofisi ya Kata, kwani gharama zilizotumika
zinaonekana kuwa ndogo kuliko fedha zilizotolewa.
Naputa amesema watamwandikia barua Katibu wa CCM wa Kata ili
kumtaka Ofisa Mtendaji wa Kata aeleze mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo kwa
kuwa wanahisi kuna ufisadi mahali.
Mwenyekiti wa Mtaa, Bw. Katani, alisema mpaka kuezekwa jengo
la ofisi hiyo zimetumika Shs. 13 milioni na kwamba kuna upungufu wa Shs. 7
milioni ili ofisi hiyo ikamilike pamoja na miundombinu yake.
Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mbagala
Charambe Machinjioni, Shaibu Omari Naputa (katikati) na Mwenyekiti wa Mtaa wa
Machinjioni A, Mkonge Hassan Katani (kushoto) wakiwa katika kituo cha kutolea
maji katika mradi wa maji uliofadhiliwa na Mfuko wa Jimbo la Mbagala ambao
umekwama.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya tawi
la Charambe Machinjioni katika Jimbo la Mbagala wakiwa katika Ofisi wa Serikali
ya Mtaa wa Mmachinjioni A ambayo haijakamilika.
No comments:
Post a Comment