Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwingimvua, hundi kifani ya dola milioni 309.65 (sh. bilioni 688.65), ambazo ni malipo ya awali (Advance Payment) kwa Mkandarasi Kampuni ya Misri, inayojenga Mradi wa kuzalisha umeme wa Maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, mkoani Pwani, Jijini Dar es Salaam. (Picha na Eva Valerian-Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Ni tukio la kihistoria ambapo
leo, Aprili 24, 2019, Serikali ya Tanzania, imetoa dola
za Marekani milioni 309.65, sawa na takriban shilingi bilioni 688.65, fedha
zake za ndani, kama malipo ya awali kwa Mkandarasi - Arab
Contractors ya Misri, wanaojenga mradi wa kuzalisha umeme unaotokana na
maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, mkoani Pwani.
"Haijapata kutokea katika
historia ya nchi hii Serikali kutoa fedha nyingi za malipo ya awali ya kiasi
kama hiki cha shilingi bilioni 688.65 katika mradi wa aina yoyote uliowahi
kutekelezwa hapa nchini isipokuwa huu" alisema Bw. Doto James, Katibu Mkuu Wizara
ya Fedha na Mipango.
Bw, Doto James, ambaye pia
ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali, alimkabidhi hundi kifani ya dola za
Marekani milioni 309.65, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua,
ambaye alimkabidhi hundi hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la
Ugavi wa Umeme nchini-TANESCO, Dkt. Alexender Kyaruzi, ambaye pia alimkabidhi
hundi hiyo Naibu Mkurugenzi wa Ujenzi wa mradi huo Mhandisi Mohamed
Hassan, kwa niaba ya kampuni za Arab Contractors (Osman A. Osman & Co na
Elsewedy Electric S.A.E (AC-EE JV).
Alisema kuwa kiasi
kilichotolewa cha shilingi bilioni 688.65 ni sawa na asilimia 70 ya zaidi ya
shilingi trilioni 1 ya malipo ya awali yanayotakiwa kutolewa ya asilimia
15 ya mradi huo ambao hadi kukamilika kwake ndani ya miaka mitatu
ijayo, unakadiriwa utagharimu zaidi ya shilingi trilioni 6.6.
Bw. James amezitaja baadhi ya
faida za mradi huo utakapo kamilika na kuzalisha megawati 2,115 za umeme kuwa
ni pamoja na nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika, kuongezeka kwa uwekezaji
katika sekta ya viwanda vitakavyo chochea uzalishaji wa
bidhaa, ajira pamoja na upatikanaji wa maji ya uhakika katika maeneo
yanayozunguka mradi na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
"Ninamtaka Mkandarasi
akamilishe mradi huu kwa wakati na kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba ili mradi
utakapo kamilika uwe kichocheo muhimu cha kuiwezesha Tanzania kufikia azma yake
ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025" alisisitiza Bw. Doto James
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati Dkt. Hamisi Mwinyimvua, alifafanua kuwa kwa mujibu
wa kifungu Na. 14.2 cha Mkataba, malipo ya awali ya Mkandarasi ni asilimia 15
ambazo zimegawanywa katika sehemu mbili ambapo asilimia 70 zinalipwa kwa
kutumia sarafu ya kigeni (dola za Marekani 309.645m) na asilimia 30 zitalipwa
kwa fedha za ndani ambazo zitalipwa baada ya Mkandarasi kukamilisha taratibu za
kimkataba zinazohusu malipo hayo.
"Ninao uhakika kwamba
malipo haya ya awali yatamwezesha Mkandarasi kukamilisha taratibu za kupeleka
vifaa katika eneo la mradi na kuanza ujenzi mara moja kwa mujibu wa Mkataba.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya TANESCO, Dkt. Alexender Kyaruzi, alisema uzalishaji wa umeme
hapa nchini umefikia megawati 1600 na kwamba kuongezeka kwa megawati nyingine
2,115 ni hatua kubwa na ya furaha na amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kutekeleza mradi huo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa
Mkandarasi wa mradi huo Mhandisi Mohamed Hassan ameishukuru Serikali na
wananchi kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata na amewahakikishia watanzania kwamba
mradi huo utatekelezwa kwa haraka na kwa viwango ili kutimiza matarajio ya nchi
ambayo ni maendeleo.
No comments:
Post a Comment