Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 19 June 2016

HUU NDIO UCHAMBUZI WA ZITTO KABWE KUHUSU BAJETI YA SERIKALI 2016/17


Zitto Kabwe (Mb)
Kiongozi wa Chama
1.     Utangulizi
Serikali ya Awamu ya Tano imewasilisha Bungeni Bajeti yake ya kwanza tangu iingie madarakani. Bajeti hii inapaswa kutafsiri maono, malengo, shabaha na ahadi kadha wa kadha ambazo zimekuwa zikitolewa tangu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Katika uchambuzi wetu huu mfupi tutatazama kama Serikali, kupitia Bajeti yake ya kwanza, imeweza kuweka fedha kwenye maneno yake.
Serikali imependekeza kutumia jumla ya shilingi 29.5 trilioni ambapo kati ya hizo shilingi 17.7 ni za matumizi ya kawaida na shilingi 11.8 ni za matumizi ya Maendeleo. Hata hivyo uwezo wa Serikali kukusanya mapato yake ya ndani (Mapato ya kodi, mapato yasiyo ya kodi na mapato ya Halmashauri) na misaada kutoka nje ni shilingi 22.1 trilioni tu. Hivyo nakisi ya Bajeti ni shilingi 7.4 trilioni sawa na 4.5% ya Pato la Taifa. Nakisi hii ya Bajeti itazibwa kwa mikopo ya ndani na nje ya Nchi ambapo Serikali itakopa jumla ya shilingi 7.4 trilioni ili kuziba nakisi hiyo ya Bajeti.
Serikali imependekeza kufanya marekebisho kadhaa kwenye kodi mbalimbali ili kuweza kufikia malengo ya makusanyo ya kodi. Tutachambua baadhi ya mapendekezo hayo na kuonyesha kama yatakidhi haja na kuwezesha kufikia malengo husika.
Chama cha ACT Wazalendo kinafanya mapitio ya Bajeti ya Serikali kwa lengo la kuainisha maeneo ambayo tunaamini Serikali inafanya vizuri na maeneo ambayo yanahitaji kuangaliwa upya na tunatoa mapendekezo mbadala. Tumeanza utaratibu mwaka huu na utakuwa endelevu kila mwaka.

2.     Dhana na misingi ya Bajeti ya Serikali
Bajeti ya serikali ndiyo tafsiri ya matamko ya kisera yanayotolewa na viongozi wa serikali katika nyakati mbalimbali. Ni kupitia bajeti ambapo serikali hujaribu kutekeleza kwa vitendo ahadi zake mbalimbali. Aidha, bajeti ni nyenzo muhimu kwa chama kilichoshinda uchaguzi kutafsiri ilani yake kwa vitendo.
Bajeti hujengwa katika misingi mikuu mitatu. Mosi, bajeti ya serikali huanisha vyanzo vya mapato ya serikali, ikiwemo kodi inayokusanywa kutoka katika vyanzo mbalimbali. Pili, Bajeti ya serikali huanishi maeneo ambayo serikali inakwenda kutumia makusanyo ya fedha. Matumizi haya hugawanywa katika makundi mawili: matumizi maendeleo na matumizi ya kawaida. Tatu, Bajeti ya serikali hutoa dira ya maendeleo ya nchi kwa kipindi cha mwaka mmoja wa fedha na miaka mingi ijayo. Katika uchambuzi huu tunaangalia maeneo ambayo serikali inakwenda kukusanya na kutumia mapato yake na kwa kiasi gani maeneo haya yanajibu changamoto za nchi kwa sasa na muda mrefu ujao.



3.     Taswira halisi ya Bajeti ya Mwaka 2016/2017
Katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, Serikali ilipanga kukusanya na kutumia Shilingi 22.5 trilioni. Kama tulivyoona kwenye utangulizi, Serikali ya Awamu ya Tano imepanga kukusanya na kutumia shilingi 29.5 trilioni katika mwaka wake wa Kwanza. Ndiyo kusema Bajeti ya Mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 31 ukilinganisha na Bajeti ya Mwaka jana. Hata hivyo, tangu Bajeti ya mwaka jana thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani imeporomoka kwa takribani asilimia 10%. Kwa kuwa manunuzi yetu mengi hasa kwenye miradi ya Maendeleo (ununuzi wa ndege, ujenzi wa Reli, mikataba ya wakandarasi wa barabara nk ) hufanywa kwa fedha za kigeni hususan dola ya Marekani, thamani halisi ya Bajeti itakuwa imeongezeka kwa asilimia 21. Aidhd, mfumuko wa bei umeongezeka kwa takribani asilimia tano kutoka mwaka 2015/16. Ndiyo kusema uwezo wa kimanunuzi wa Bajeti ya mwaka huu ni pungufu wa uwezo wa Bajeti ya mwaka jana kwa asilimia tano. Hivyo basi ongezeko hali la Bajeti ya mwaka huu ni takribani asilmia 16. Hata hivyo tunaipongeza serikali kwa ongezeko hili, pamoja na kwamba, kama tutakavyoonyesha, na kama ambavyo wachumi mbalimbali wamekwishaoonyesha, utekelezaji wake unatia shaka.
.
4.     Bajeti inajibu Changamoto za Nchi?
Changamoto kubwa ya nchi yetu hivi sasa ni ukosefu wa Ajira kwa maelfu ya Vijana wanaomaliza masomo na kuingia kwenye soko la Ajira. Ili kujibu changamoto hii hatuna budi kutazama sera za kibajeti kwenye maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi na kuona kama maamuzi ya kibajeti yanapeleka rasilimali kwenye maeneo hayo.
Sekta yenye kuajiri Watanzania wengi kwa sasa ni sekta kubwa ya Uchumi wa Vijijini ( Kilimo, Mifugo na Uvuvi) ambapo kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2015 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango tarehe 8 Juni 2016, asilimia 65 ya Watanzania wanajihusisha na ajira vijijini. Ajira katika sekta rasmi ni 2.1 milioni chini ya 10% ya Watanzania wote wenye uwezo wa kufanya kazi 22.3 milioni. Katika ajira rasmi sekta inayoongoza ni Viwanda kwa kuchangia 20% y ajira zote rasmi ikifuatiwa na Elimu 17% na Ulinzi na Utawala 15%. Mchanganuo huu unaonyesha kuwa Watanzania wengi ( zaidi ya theluthi mbili) wanaishi nje ya mfumo rasmi na hivyo juhudi kubwa inapaswa kuwekwa kwenye Uchumi wa Vijijini ili kuboresha maisha yao na kuongeza ajira rasmi huko huko vijijini.
Bajeti ya mwaka 2016/17 inajibu changamoto hii? Ili kujibu swali hili kwa uhakika inabidi kutazama kwa ufupi hali ya sekta ya Kilimo ( inayojumuisha na Mazao, Misitu Ufugaji, Uvuvi nk) na kuona kama rasilimali za kutosha zimeelekezwa kuikwamua sekta hiyo.
Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kilimo umeporomoka mpaka 2.3% mwaka 2015. Sababu kubwa imeelezwa ni tija ndogo, teknolojia duni, ukosefu wa masoko na uhaba wa viwanda vya kusindika mazao ya kilimo. Kwa sisi wachumi tunatuambia kuwa ili kupunguza umasikini wa Tanzania kwa zaidi ya nusu ilihitajika sekta ya Kilimo kukua kwa kati ya 8% na 10% kwa mwaka. Kwa ukuaji huu maana yake itachukua miaka mingi sana Watanzania kuondoka kwenye dimbwi la umasikini. Baadhi ya Mazao yanayotarajia kuzalisha malighafi za viwanda uzalishaji wake umeporomoka kwa kiwango cha kutisha. Kwa mfano Zao la Pamba, uzalishaji na mauzo nje ya zao hili yameshuka kwa 45% kwa mujibu wa Taarifa ya hali ya Uchumi iliyosomwa na Serikali bungeni tarehe 8 Juni 2016.
Hata hivyo, katika Bajeti yote ya Maendeleo ya tshs 11.8 trilioni, ni shilingi 100 bilioni tu zimetengwa kwa ajili ya sekta ya Kilimo sawa na 1% ya Bajeti nzima ya Maendeleo. Ni dhahiri kwamba ili kujenga uchumi shirikishi ni muhimu kufanya jitihada za makusudi kuhakikisha kwamba kilimo kinaanza kuchangia vya kutosha katika kasi ya ukuaji wa Uchumi.
Kwa Uchumi wa Tanzania, ujenzi wa Sekta ya Viwanda hauwezi kufanikiwa bila kukua kwa sekta ya kilimo. Kilimo ndio sekta Kiongozi katika kutokomeza umasikini kwani inachangia theluthi moja ya Pato la Taifa na kuajiri theluthi mbili ya Watanzania wote. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano imeshindwa kufungamanisha Sekta ya Kilimo na ndoto ya maendeleo ya Viwanda. Ushahidi wa kisayansi unaotokana na Taarifa za Serikali yenyewe inaonyesha kuwa hakuna mahusiano kati ya mipango ya maendeleo ya viwanda na mipango ya maendeleo ya wananchi.
Maeneo mengine ambayo yanaweza kuzalisha ajira za kutosha ni Sekta ya Utalii ambayo kwa kiasi kikubwa inazalisha ajira kwenye sekta za usafirishaji, malazi na huduma za vyakula. Sekta ya Utalii ililiingizia Taifa Mapato ya kigeni ya Dola za Kimarekani 2.3 bilioni. Ikumbukwe kuwa kila Mtalii anayeingia nchini anatarajiwa kula, kulala na kusafiri na yote hayo ni huduma zinazotolewa na Watanzania wanaoajiriwa kwenye mahoteli na magari ya Watalii. Hata hivyo Serikali katika hotuba yake ya kwanza kabisa ya Bajeti imeamua kurudisha nyuma juhudi zote za kukuza Sekta ya Utalii kwa kuanzisha kodi ya VAT kwenye huduma zote za Utalii. Kodi hii itaifanya Tanzania kuwa ghali kuliko washindani wake kama Kenya ambayo imeifuta kodi hii na kuongeza Bajeti ya kutangaza Utalii. Utalii ndio sekta inayoongoza kwa kuingiza mapato mengi ya fedha za kigeni na kawaida inapaswa kuangaliwa kama sekta ya nje ( export sector ). Sekta za nje hazina kodi ya Ongezeko la Thamani yaani VAT lakini cha kushangaza ni kwamba Serikali imeweka kodi hii kwa sekta ya Utalii.
Vile vile maamuzi ya Serikali kubana matumizi kwa kufanya mikutano yake kwenye majengo ya Serikali yatapelekea mahoteli mengi nchini kufunga shughuli zao na kuachisha kazi mamia ya Watanzania wanaofanya kazi kwenye mahoteli hayo. Hatua hii itakosesha Serikali mapato yatonayo na Kodi na PAYE ambayo hulipwa na Wafanyakazi.
Kwa Ujumla Bajeti ya mwaka 2016/17 haitaweza kutatua kero ya ajira nchini na badala yake itapelekea Watanzania wengi zaidi kukosa ajira kwa waajiri kupunguza wafanyakazi ili kubana matumizi. Tumeanza kusikia waajiri mbalimbali wakipunguza wafanyakazi. Hali itakuwa mbaya zaidi kwa wenye mahoteli na miji kama Arusha itaumia zaidi kwani inategemea sana Biashara ya Utalii. Kuanguka kwa sekta ya Utalii ni kuanguka kwa uchumi wa nchi kwa ujumla.

5.      Viwanda Vitajengwa?
Kauli mbiu ya Bajeti ya mwaka 2016/17 ni kuongeza uzalishaji viwandani ili kupanua fursa za ajira. Kama tulivyoainisha hapo juu, Viwanda vinachangia 20% ya ajira zote rasmi nchini na kwamba thuluthi mbili ya Watanzania wameajirwa na sekta isiyo rasmi. Hivyo juhudi za kuongeza uzalishaji viwandani ni muhimu sana ili kuwaondoa Watanzania wengi kutoka sekta isiyo rasmi na kuwaingiza kwenye sekta rasmi. Ili kupima nia hii ya Serikali inabidi kutazama hatua mbalimbali za kisera kuwezesha sekta binafsi kufungua viwanda vingi zaidi nchini na kuajiri watu wengi.
Moja ni jambo la kupongeza sana kwamba Bajeti ya mwaka 2016/17 imelenga kuondoa changamoto ya miundombinu kwa kiwango kikubwa sana. Wenye Viwanda wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu kutokuwepo kwa umeme wa uhakika, gharama kubwa za usafirishaji wa malighafi na bidhaa na mawasiliano ya intaneti yasiyo na kasi ya kutosha. Katika Bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali imeelekeza rasilimali nyingi sana kujibu changamoto hizo. Kwa mfano, Bajeti za Miundombinu ya Usafirishaji na Umeme zimechukua 53% ya Bajeti yote ya Maendeleo. Jumla ya shilingi 6.2 trilioni ya Bajeti imetengwa kwa ajili ya miradi ya miundombinu na umeme. Huu ni mwelekeo mzuri katika kujibu changamoto hizo.
Hata hivyo inawezekana kabisa kuwa uwekezaji kwenye Viwanda ukakumbwa na changamoto ya soko maana katika Bajeti ya Mwaka huu Serikali imebana matumizi na hivyo watu hawatakuwa na fedha za kutumia bidhaa na huduma. Miundombinu inaweza kujengwa lakini ikawa haina watu wa kuitumia wala bidhaa za kusafirisha kwa sababu hakuna vivutio vya kuanzisha viwanda pia. Ikumbukwe kuwa Serikali haianzishi viwanda bali inajenga mazingira mazuri ya wawekezaji kuanzisha viwanda. Bajeti ya mwaka 2016/17 haijaweka hivyo vivutio vya kaunzisha viwanda na imeminya uwezo wa walaji kutumia kwa kudhibiti matumizi na pia kutoza kodi nyingi zinazopunguza uwezo wa kutumia bidhaa na huduma.
Ni vema kukumbusha kuwa kasi ya ukuaji wa shughuli za uzalishaji viwandani ni ndogo kwa kiwango cha 6.5% na mchango wake katika Pato la Taifa ni mdogo sana wa 5.2% tu. Serikali ilipaswa kuja na Sera mahususi za kufikisha 10% au zaidi ukuaji wa uzalishaji viwandani. Hii maana yake ni kwamba matamshi mengi kuhusu viwanda hayaendani na hali halisi ya viwanda nchini. Serikali haina budi kukaa na wenye viwanda na kupata mwafaka wa namna bora ya kuweka sera mahususi zitazopelekea uwekezaji mkubwa wa wenye mitaji katika viwanda na kuongeza uzalishaji. Vinginevyo, ahadi za Serikali hazitaweza kutekelezwa kwa wakati. Vile vile viwanda vitahitaji muda mpaka kuanza uzalishaji, hivyo juhudi kubwa ilipaswa kuwekwa kwenye uzalishaji wa malighafi za viwanda ili wakati viwanda vinaanza kazi vikutane na malighafi.
5.1Mapendekezo
Katika sekta hizi tatu nyeti kwa uchumi wa Tanzania, Chama cha ACT Wazalendo tunapendekeza hatua zifuatazo kuchukuliwa
        I.            Serikali itunge mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka (stable fiscal regime) kwa sekta ya kilimo ili kumwezesha mkulima kubakia na sehemu kubwa ya mapato yake na kuvutia wananchi wengi kujishughulisha na uzalishaji katika kilimo.
      II.            Serikali iharakishe kuanza kufanya kazi kwa soko la bidhaa ( commodities exchange ) ili kupuguza watu wa kati katika sekta ya Kilimo
   III.            Serikali ianzishe mfumo wa hifadhi ya jamii kwa wakulima kwa kuanzisha pia Fao la Bei ili kuhakikisha kuwa mkulima anarudisha gharama zake za uzalishaji pindi bei katika soko zinapoterereka.
   IV.            Serikali ifute kodi zote za mazao ( produce cess) na kuondoa vizuizi vya aina yeyote ile ili kuhakikisha mkulima anauza bidhaa zake anapotaka mwenyewe.
      V.            Serikali ifanye maamuzi ya kisera ili kuhakikisha kuwa Viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi vinapewa vivutio vya kikodi.
   VI.            Serikali iweke utaratibu kurahisisha taratibu za kufungua viwanda na kuweka mfumo wa kisheria wa kufidia baadhi ya gharama za uzalishaji kwa viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi wengi zaidi
 VII.            Serikali iondoe msururu wa kodi katika sekta ya Utalii ikiwemo kuondoa kabisa wazo la kuweka VAT kwenye huduma za Utalii katika Bajeti ya 2016/17
VIII.            Serikali itunge mfumo rahisi wa kikodi katika sekta ya utalii kwani ni sekta inayoweza kuajiri vijana wengi sana na kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la ajira nchini.

6.     Bajeti ina maana gani kwa Wananchi?
Tunapotazama maana ya Bajeti kwa wananchi hatuna budi kuangalia mambo ya msingi kama bei za bidhaa za huduma. Iwapo shilingi 1000 aliyonayo mwananchi leo itanunua bidhaa nyingi zaidi kuanzia Mwezi Julai mwaka 2016, tutasema hali ya maisha ya mwananchi imeboreka. Iwapo shilingi 1000 aliyonayo mwananchi leo itanunua bidhaa chache zaidi kuanzia mwaka mpya wa fedha tutasema hali ya wananchi imeporomoka.
-          Serikali imepandisha kodi mbalimbali kwenye bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na ushuru wa bidhaa mbalimbali. Hii itapelekea bei ya bidhaa na huduma kupanda na kusababisha mfumuko wa bei tofauti na malengo ya Serikali. Serikali inatarajia mfumuko wa bei kuwa katika tarakimu moja. Hata hivyo uchumi wetu unategemea sana uchumi wa dunia kwa sababu tunaagiza zaidi ya uwezo wetu wa kuuza nje. Bei ya Mafuta katika soko la dunia imeanza kupanda taratibu na sasa imefikia $50 kwa pipa moja kutoka chini ya $30. Uzalishaji wa kilimo umekuwa hauridhishi kwani chakula ni sehemu kubwa ya mfumuko wa bei ( huchangia takribani 52% ya kapu la bidhaa na huduma). Kuna mwelekeo mkubwa kwamba mfumuko wa bei utaongezeka mpaka kwenye taratimu mbili na hivyo kupelekea hali za wananchi kuwa mbaya. Kodi za miamala ya kutuma fedha kwenye mabenki au simu za mkononi inabidi zitazamwe upya ili kuhakikisha kuwa malengo ya Serikali ya kuwaingiza wananchi wengi katika mfumo wa kibenki yanafanikiwa.
-          Serikali imeamua kubana matumizi kwenye baadhi ya maeneo, jambo jema sana. Hata hivyo uamuzi huo utaendana na biashara nyingi kufungwa na watu wengi kupoteza ajira na kuingia mtaani. Hii inaweza kuongeza ugumu maisha kwa wananchi wengi wa kawaida. Serikali inabidi kuaianisha hatua inazochukua na madhara yake katika kuhakikisha jamii inabaki salama. Ni vizuri Serikali ikatazama ni maeneo gani ambayo matumizi yake yanachochea ukuaji wa sekta binafsi na kuyaachia badala ya kubana na kukumbatia fedha zote. Madhara yake ni kwamba uchumi hautapata ‘ multiplier effect’ na hivyo kuendelea kudumaa badala ya kukua mpaka kufikia tarakimu mbili.
Kwa ujumla, Bajeti ya mwaka 2016/17 itapelekea maisha ya mwananchi wa kawaida kuwa magumu zaidi kwa sababu gharama za maisha zitapanda na kipato kupungua. Sera za Bajeti zimeshindwa kutazama Bajeti kama Sera (policy instrument) na badala yake imekuwa nyenzo tu ya kukusanya mapato na kuyatumia.
7.     Mambo ya Kushangaza katika Bajeti 2016/17
Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya Tano imeshindwa kutoka na jambo kubwa la kisera ambalo lingeamsha ari ya wananchi ya kufanya kazi na kujenga Taifa lao. Jambo kubwa la kushangaza ni kwamba Bajeti hii ni ya kawaida mno na haina tofauti kubwa na Bajeti zilizopita. Tofauti na matamko makali makali ya Serikali kabla ya Bajeti, kimsingi Bajeti hii inathibitisha kauli kwamba watawala ni wale wale na ni inaonyesha kuwa Utawala wa Awamu ya 5 utachoka mapema sana kabla hata kazi haijaanza. Hii inathibitishwa na ukweli kwamba hakuna ubunifu katika kutafuta vyanzo vipya vya mapato. Yafuatayo ni mambo ambayo yanashangaza katika Bajeti ya mwaka 2016/17
         i.            Serikali imeamua kupandisha nakisi ya Bajeti mpaka 4.5% ya Pato la Taifa na kuziba nakisi hiyo kwa kukopa kutoka ndani na nje. Mwaka 2016/17 Serikali itakopa shilingi 7.5 trilioni ambapo kati ya hizo mikopo ya masharti ya kibiashara itakuwa shilingi 2.1 trilioni. Mikopo ya ndani itapelekea Serikali kugombania vyanzo hivyo na wafanyabishara wa ndani na kupelekea wafanyabiashara kupata tabu kubwa kupata fedha za kuendesha biashara ( crowd out effect). Mikopo ya nje nayo itaongeza gharama za kuhudumia Deni la Taifa ambapo hivi sasa nusu ya mapato yote ya Serikali itakwenda kulipa madeni ( Wakati Mapato yote ya Ndani ya Serikali ni shilingi 17.7 trilioni, mwaka Huu Serikali italipa madeni shilingi 8 trilioni). Hata hivyo, Serikali haina uhakika wa kupata mikopo hii kwa sababu inategemea na jamii ya kimataifa ya mabenki yao yanaonaje Serikali yetu. Mwaka 2015/16 Serikali ilipanga kukopa shilingi 2.1 trilioni na ikaambulia shilingi 1.1 trilioni tu. Kwa namna Serikali ya awamu ya tano inavyohusiana na mataifa ya nje na hatua mbalimbali za kuonekana kuvunja mikataba ya kibiashara na kampuni za uwekezaji za nje, inawezekana Serikali isipate hata theluthi ya mikopo hii kutoka nje.  Jambo la kushangaza ni kwamba matamko ya Viongozi wa Serikali yalionyesha kuwa Tanzania haitahitaji misaada kutoka nje lakini Bajeti kwa kiwango kikubwa inategemea  fedha kutoka nje ( Misaada na Mikopo shilingi 3.6 trilioni na mikopo ya kibishara kutoka nje shilingi 2.1 trilioni kufanya jumla ya shilingi 5.7 trilioni).
       ii.            Serikali inategemea kukusanya shilingi 17.8 trilioni kutokana na kodi na mapato yasiyo ya kikodi. Hata hivyo, Serikali inatarajia kutumia shilingi 8 trilioni kulipia deni la Taifa na shilingi 6.6 trilioni kulipia mishahara ya wafanyakazi. Jumla ya Matumizi haya shilingi 14.6 trilioni sawa na 82% ya mapato yote ya Serikali. Hii maana yake ni kwamba katika kila shilingi 100 ambayo Serikali inakusanya, shilingi 82 zinalipia deni na mishahara na hivyo Serikali kubakia na shilingi 18 tu kwa ajili ya matumizi mengineyo na matumizi ya maendeleo. Uamuzi wa Serikali kutenga shilingi 11.82 trilioni kwa ajili ya Maendeleo unategemea misaada ya wafadhili na mikopo ya ndani na nje jambo ambalo Serikali haijawaambia wananchi kwani inajua ni jambo gumu kutekelezeka. Kutenga 40% ya Bajeti kwenye maendeleo ni jambo jema lakini ni siasa zaidi kuliko uhalisia kwani hakuna fedha za uhakika kwenye Bajeti kuweza kulipia miradi hiyo ya maendeleo.
     iii.            Serikali imeamua kutoza kodi ya 5% kwenye Kiinua Mgongo cha Wabunge wanapomaliza miaka yao 5. Kwanza, ni jambo jema sana kuwa Serikali inataka kuwaweka wabunge sawa na wafanyakazi wengine wowote ambao kiinua mgongo hutozwa kodi. Hata hivyo jambo la kushangaza ni kwamba kodi hii haina nyongeza yeyote ya mapato katika mwaka wa fedha 2016/17. Chama cha ACT Wazalendo tulitarajia Serikali ama kufuta posho za vikao katika mfumo mzima wa utumishi wa umma au kutoza kodi posho hizi angalau kwa kiwango cha kodi zuio ya 10%. Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba Mapato ya Viongozi wakuu wa Serikali kama Rais, Makamu wa Rais nk hayapo wazi na hayatozwi kodi yeyote ile. Serikali ingeanza kwa kutoza kodi mishahara ya viongozi wakuu wa Serikali akiwemo Rais ili kuonyesha mfano wa uzalendo kwa wananchi.
     iv.            Serikali imeamua kushusha kiwango cha chini cha kodi ya mapato (PAYE) kutoka asilimia 11% mpaka asilimia 9%. Nafuu anayopata mfanyakazi ni tshs 3800 tu. Jambo la kushangaza ni kwamba Serikali imebakiza kiwango cha kutozwa kodi kuwa kile kile cha zaidi ya shilingi 170,000. Tulitaraji kuwa kipato cha chini ya shilingi 360,000 kisingetozwa kodi na kiwango cha juu kingeongezwa mpaka kufikia zaidi ya shilingi 15 milioni. Rais mara kwa mara amekuwa akizungumza kuhusu dhamira ya kupunguza malipo makubwa wanayopata watu (“wanaoishi kama malaika kuwashusha waishi kama mashetani”). Serikali inapaswa kurekebisha tofauti ya kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho kwa kupitia sera za kodi. Tulitarajia Serikali ingetumia Bajeti yake ya kwanza kurekebisha tofauti hizo. Chama cha ACT Wazalendo kinapendekeza mfumo mbadala wa kodi ya Mapato katika majumuisho ya mada hii.
       v.            Serikali haikugusia mabadiliko ya mfumo wa kodi kwa kampuni za kimataifa zinazowekeza nchini ( Multinational Corporations). Jambo la kushangaza ni kwamba Serikali imeshiriki katika mkutano wa kimataifa wa rushwa uliofanyika nchini Uingereza ambapo ajenda yake kubwa ilikuwa kuzuia makampuni makubwa kukwepa kodi katika nchi wanazozalisha faida. Serikali ya awamu ya tano imeshindwa kabisa kuja na sera za kibajeti kuzuia ukwepaji huu mkubwa wa kodi ambao kwa hapa Tanzania ni zaidi ya 5% ya Pato la Taifa ( yaani zaidi ya nakisi ya Bajeti ya mwaka huu).
6. ACT Wazalendo ingefanya nini katika mwaka wake wa Kwanza?
Chama cha ACT Wazalendo kinapendekeza mabadiliko makubwa ya mfumo wa kodi kufanyika ikiwemo kuwa na mtazamo kuwa Kodi sio tu ni sera ya mapato bali ni sera ya kuchochea ukuaji uchumi wa sekta teule. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya Tano haipelekei kujenga Tanzania ambayo hakuna unyonyaji wala kujenga Uchumi Imara, shirikishi na unaosimamiwa na Dola. Serikali ya awamu ya tano inaendeleza vikundi vya kinyonyaji ( cartels) ama kwa kuziimarisha cartel zilizopo au kujenga vi cartel vipya kwa faida za watawala. Kwa mfano, Serikali imeshindwa kuvunja vikundi maslahi kwenye sekta ya Sukari na bidhaa zingine zinazoagizwa kutoka nje ikiwemo mafuta ya kula na mchele licha ya kelele ambazo zimepelekea bei ya sukari kupanda maradufu na kuwapa wananchi ugumu wa maisha. Wakulima wa mpunga nchini hivi sasa wanapata ushindani mkubwa kutoka mchele unaotoka nje ya nchi kama Vietnam na Pakistani na hivyo kupelekea bei ya wakulima kuporomoka na kushindwa kulipa mikopo waliyochukua kuendesha kilimo.
Tunapendekeza Wabunge wazingatie masuala machache yafuatayo kwenye mjadala wa Bajeti na hatimaye kuweza kuifanya Serikali kuepuka madeni makubwa inayokwenda kuchukua na kuanza kujitegemea.
                     i.            Katika sheria ya Fedha ya mwaka 2016, kuwe na kifungu cha Sheria kinachoweka ukomo wa misamaha ya kodi mpaka 1% ya Pato la Taifa. Misamaha ikaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na misamaha yenyewe na taarifa ya ukaguzi viwekwe wazi kwa umma. Mfumo ambao Serikali imependekeza sasa unaweza kuwa na madhara makubwa sana kwa kuongeza urasimu na hasa ukizingatia kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania haina utamaduni wa kurudisha fedha ( tax refunds). Uamuzi wa kutunga sheria tunayopendekeza unaweza kuwezesha Serikali kukusanya shilingi trilioni 1.8 ya kodi.
                   ii.            Serikali irekebishe sheria ya Kodi ya Mapato na kuweka vifungu vinavyohakikisha kuwa kila Mtanzania anajaza Tax Returns kila mwaka. Hii itawezesha kila Mtanzania kuwa na wajibu wa kujaza fomu inayoonyesha kipato chake na TRA kutambua walipa kodi. Rais aongoze hili kwa kujaza Tax Returns kila mwaka na kuweka wazi. Fomu zaweza kutolewa kupitia mfumo wa Serikali za Mitaa kwa Watendaji wa Mitaa na Vijiji.
                 iii.            Serikali ifanye marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi zinazohusisha makampuni ya kimataifa ( MNCs) ili kuzuia kumomonyoa wigo wa kodi ( Base Erosion and Profit Shifting) kunakofanywa na kampuni hizi. Hili linawezekana kwa Serikali kuchukua hatua ya kupitia mikataba ya kikodi (double taxation treaties) ambayo Tanzania iliingia na nchi nyingine duniani. Tafiti mbalimbali katika eneo hili zinaonyesha kuwa Tanzania hupoteza 5% ya Pato la Taifa kutokana na vitendo vya kampuni kubwa kukwepa kodi kwa kutumia mbinu za kihasibu (tax planning measures). Iwapo Serikali ikichukua hatua kwenye eneo hili haitahitaji kukopa kabisa shilingi 7.5 trilioni inazopanga kukopa mwaka 2016/17 ama itakopa kidogo sana kwa sababu hatua hizi zitaingiza fedha nyingi kwa mara moja.
                 iv.            Kodi za Majengo ziendelee kukusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuziwezesha kuwa na mfumo wa elektroniki wa kukusanya kodi hizi kupitia kwa Watendaji wa Mitaa. Mamlaka ya Mapato Tanzania haina uwezo wala nyenzo za kukusanya kodi hii kwa ufanisi.
                   v.            Michango ya Hifadhi ya Jamii ishushwe mpaka 14% kwa Waajiri kuchangia 7% na Waajiriwa kuchangia 7% ya mishahara yao. Hii itasaidia kupunguza gharama za kuajiri kwa Waajiri. Tozo ya SDL ishushwe mpaka 3% pia. Eneo hili ni muhimu liangaliwe kwa muktadha wa kukuza ajira nchini hivyo ajira zinapoongezeka mapato kwenye maeneo haya yanaongezeka pia.
                 vi.            Msamaha wa kodi kwenye maduka ya Majeshi na Taasisi za Dini iendelee kama ilivyo sasa kwani misamaha hii ni chini ya asilimia 1 ya misamaha yote inayotolewa nchini. Taasisi za Dini zinatoa huduma nyingi kwa jamii hasa maeneo ambayo Serikali imeshindwa kutoa huduma kama vile Elimu, Afya nk. Kuwapa posho wanajeshi ili wanunue bidhaa kunaweza kuwaweka wanajeshi katika hatari ya kununua bidhaa zisizo na ubora na hata kuwaweka kwenye hatari ya kudhuriwa. Vikosi vyetu vya ulinzi na usalama havipewi misamaha kwa ajili ya mapato tu bali ni kwa ajili ya kuimarisha usalama na ustawi wao kijamii.
               vii.            Pendekezo la kodi ya VAT kwa huduma za utalii liondolewe ili Tanzania iendelee kuwa shindani kwenye sekta ya utalii.
             viii.            Pendekezo la kodi kwenye karatasi kutoka nje litazamwe upya kwani litaongeza gharama za uzalishaji wa vitabu nchini. Tanzania haina viwanda vya karatasi vya kulinda ukiachana na Mgololo ambacho karatasi zake hazitumiki hapa nchini kwa kiasi kikubwa.
                 ix.            Pendekezo la tozo kwenye miamala ya simu za mkononi na ile ya kibenki iondolewe ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kutumia mifumo ya kifedha ya nchi.
                   x.            Serikali itangaze kupiga marufuku kuuza malighafi nje ya nchi baada ya miaka mitatu ijayo ili kihakikisha bidhaa za kilimo zinaongezwa thamani hapa hapa nchini kuongeza ajira kwa Watanzania.

7.     Hitimisho
Tanzania isiyo na unyonyaji na yenye uchumi shirikishi unaozalisha ajira nyingi haitajengwa kwa Bajeti ya mwaka mmoja. Hata hivyo ni muhimu juhudi zianze kuonekana katika hatua za mwanzo kabisa. Serikali ya awamu ya Tano ina maono ya kujenga Tanzania ya Viwanda. Hata hivyo, Bajeti yake ya kwanza kabisa imeshindwa kuonyesha sera mahususi ambazo zinaweza kupelekea watu wenye mitaji kuleta mitaji yao Tanzania na kujenga viwanda. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya Tano imekosa ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na sera zitakazopelekea nchi yetu kusonga mbele kiuchumi. Maamuzi ya kibajeti yaliyotangazwa na Serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango hayana mvuto unaoonyesha nia ya kujenga uchumi wa viwanda. Chama cha ACT Wazalendo kimejaribu kuonyesha mapungufu kadhaa yaliyomo kwenye mfumo wa Bajeti ya mwaka 2016/17 na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha. Ni dhahiri kuwa mwaka unaoanzia Julai 2016 utakuwa ni mwaka mgumu sana kwa Watanzania wa kawaida kwani Bajeti haijawapa unafuu wa maisha na badala yake imeongeza machungu. Ni kweli kwamba ili kupata maendeleo ni lazima kuumia katika mchakato, lakini kuumia huko ni lazima kueleweke na umma. Hivi sasa Umma umebakia bumbuwazi bila kuelewa Bajeti na Serikali imekosa uwezo wa kuwasiliana na umma vizuri.
Chama cha ACT Wazalendo kinahimiza wananchi kufuatilia kwa kina utekelezaji wa Bajeti ya Serikali na kupaza sauti pale wanapoumia ili Serikali ipate kusikia na kurekebisha mapungufu. Tunaamini kuwa tunao uwezo wa kujenga Uchumi shirikishi na usio na unyonyaji wa kidola au sekta binafsi. Tuna uwezo wa kujenga Tanzania lenye Ujamaa wa Kidemokrasia yaani Taifa lisilo na unyonyaji na lenye uchumi unaowashirikisha wananchi wengi.

Ahsanteni kwa kunisikiliza na kunisoma!

No comments:

Post a Comment