Pages

Pages

Pages

Thursday 3 September 2015

MAKOMANDOO WATIA FORA HAFLA YA KUMUAGA JK

Makomandoo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wakionyesha umahiri wao wa kuvunja tofali katika mwili wa mmoja wao wakati wa hafla ya  kumuaga Amiri Jeshi Mkuu, Rais jakaya Kikwete kwenye Uwanja wa Uhuru jana.  Picha na Omar Fungo 

Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jana walikuwa kivutio katika hafla ya kumuaga Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo iliyohusisha vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama, makomandoo hao walitia fora kwa kuonyesha mbinu mbalimbali za kujihami na ukakamavu.

Makomandoo hao kama ilivyo desturi yao, walionyesha jinsi ya kupambana na maadui, kukunja nondo ya milimita 16 kwa kutumia mikono, kuvunja matofali ya inchi tano kwa ngumi, kulala juu ya misumali kifua wazi na kupigwa na mbao mgongoni na kifuani.

Kwa upande wa Polisi, walionyesha namna farasi na mbwa wanavyotumika wakati wa kupambana na wahalifu, ikiwa ni pamoja na kusaidia kuwahisha kutoa taarifa.

Askari wa Magereza, kwa upande wao  walikuwa kivutio walipoonyesha namna wanavyopambana na mahabusu wakorofi wanapokuwa magerezani.

Katika shughuli hiyo, Amiri Jeshi Mkuu anayemaliza muda wake mwishoni mwa mwaka, alipigiwa mizinga 21.

Ilivyokuwa

Katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini hapa jana, Amiri Jeshi Mkuu aliingia uwanjani hapo saa 4:16 asubuhi akiwa kwenye gari la wazi akiambatana na Mkuu wa Majeshi nchini Jenerali,  Davis Mwamunyange na alikagua gwaride maalumu na kupokea heshima kutoka kwa ndege za kijeshi zaidi ya 20, zilizopita juu ya uwanja huo.

Hafla hiyo pia, ilihudhuliwa na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, maofisa na makamanda mbalimbali wa jeshi na wananchi.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alitunuku nishani kwa askari wa majeshi ya ulinzi na usalama nchini katika sherehe iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Kikwete alitunuku nishani ya utumishi uliotukuka Tanzania kwa askari 12 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza.

Nishani hiyo hutunukiwa kwa maofisa walioko kwenye utumishi wa JWTZ wa cheo cha Meja na kwenda juu na kwa maofisa walioko katika utumishi wa Jeshi la Polisi ama Magereza, kuanzia cheo cha Mrakibu au wa juu ya cheo cha hicho na kwa maofisa waandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao wametimiza siyo chini ya miaka 20 mfululizo kwenye ofisa.

Rais Kikwete pia alitunuku nishani ya utumishi wa muda mrefu Tanzania kwa maofisa tisa wa majeshi hayo ya ulinzi na usalama.

Nishani hiyo ya utumishi wa muda mrefu Tanzania hutunukiwa kwa maofisa walioko kwenye utumishi hai wenye kamisheni katika JWTZ ama kwa maofisa ambao wametangazwa gazetini wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao wametimiza miaka 15 mfululizo wakiwa maofisa wenye tabia njema ya kuweza kusifiwa.

Rais Kikwete pia alitunuku nishani ya utumishi wa muda mrefu na tabia njema kwa watunukiwa tisa, ambayo hutunukiwa kwa maofisa wasiokuwa na kamisheni katika JWTZ na kwa wakaguzi, wakaguzi wasaidizi, stesheni sajini,sajini na koplo katika majeshi ya Polisi na Magereza.

CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment