Pages

Pages

Pages

Thursday 3 September 2015

ADC YAJA NA VIPAUMBELE VITANO URAIS 2015

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha Alliance For Democratic Change (ADC, Hamadi Rashid (kulia), mgombea urais wa chama hicho Tanzania, Chief Yemba na mgombea mwenza, Said Miraji Abdullah wakitambulishwa wakati wa mkutano wa ufunguzi uliofanyika katika Uwanja wa Tangamano mijni Tanga jana. Picha na Salim Mohammed 

Na Burhani Yakub
Tanga. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Chief Yemba ametaja vipaumbele vitano ambavyo atavitekeleza kama atachaguliwa kuwa rais.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za chama hicho jana, Yemba alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni elimu, afya, ajira na uwajibikaji, haki sawa katika utawala na ufufuaji wa miundombinu iliyokufa.

Alisema tangu dunia iumbwe, kipaumbele cha kwanza kilikuwa elimu na ndiyo maana hata mitume waliwahimiza watu wasome ili kuongeza maarifa.

Alisema atabadilisha mfumo wa elimu ili wanaomaliza vyuo vikuu waweze kuajirika tofauti na hali ilivyo sasa ambapo mfumo hauwapi wahitimu hao fursa ya kukubalika kwenye ajira.

Pia, Yemba alisema atawawezesha watoaji wa huduma kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitali kufanya kazi kwa saa 24 na kuvipatia vifaa tiba vya kisasa. Alisema atahakikisha kila mfanyakazi anazalisha ajira ya watu wawili zaidi kwa sababu wafanyakazi wote watafanya kazi kwa saa 24 wakibadilishana kwa zamu.

Alitaja kipaumbele kingine kuwa ni utawala kwa haki sawa kwa wote hasa kwenye eneo la sheria ambako atahakikisha uamuzi unatolewa bila kuwagawa watu kwa makundi.

“Darfur hakuna sheria ya ugaidi, lakini Tanzania kwenye utulivu kuna sheria ya ugaidi. Unapoweka sheria kama hiyo unatoa nafasi kwa baadhi ya makundi kugandamizwa. Hili kwa ADC halitakuwapo, ni lazima tutawale kwa kufuata haki na ucha Mungu” alisema.

Katika sekta ya uchumi, alisema atahakikisha miundombinu, ikiwamo bandari na reli, inafufuliwa ili kuongeza ajira kwa wananchi, hasa vijana ambao sasa idadi yao ni kubwa na hawana ajira.

Mgombea urais Zanzibar
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed alisema tofauti ya ADC na vyama vingine ni kwamba chama hicho kiliundwa kwa ajili ya kuwakumbusha wananchi kutambua uwapo wa Mwenyezi Mungu.

Alisema chama hicho kina sera ya vitendo kwa asilimia 70 na maneno asilimia 30, hivyo kikipata nafasi ya kuongoza, nchi itakuwa na kazi moja tu, kuwaletea wananchi maendeleo kupitia shughuli za uzalishaji mali na viwanda.

Alisema Tanga ina bahati ya kuwa na bandari, lakini haina msaada kiuchumi kwa sababu imekufa, hivyo mpango wa ADC ni kuifufua ili iweze kushindana na Bandari ya Mombasa.

Hamad alisema ADC inakusudia kuwajengea wakazi wa Tanga mashine ya kukaushia karafuu kama itakavyofanya kwa Zanzibar na kwamba hakuna chama kilicho na sera ya namna hiyo.

Kuhusu elimu, alisema ADC itahakikisha inawalea wananchi kitaaluma na kimaadili kuanzia watoto wa miaka mitatu hadi vyuo vikuu ili kukuza kizazi chenye heshima na kinachofanya kazi vizuri.

Tutaheshimu matokeo
Hamad alisema wagombea wa ADC wakishindwa katika Uchaguzi Mkuu, wataheshimu matokeo na kuwaunga mkono watakaopita kwa kura nyingi.

“Nikishindwa nitakubali matokeo na nitamuunga mkono atakayeshinda bila kuleta vurugu wala chokochoko kwa sababu tunataka Tanzania yenye kudumisha amani iliyopo,” alisema.

Mgombea mwenza
Kwa upande wake, mgombea mwenza, Said Miraj aliwahimiza watu waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili wakachague viongozi wanaowataka.

“Kwa hivyo unatakiwa kutumia nafasi hiyo adhimu kuchagua Serikali. Nakuomba kwa heshima kubwa tumia kura yako kumchagua Chief Yemba kwani atakuwa kiongozi mcha Mungu,” alisema Miraji na kuongeza:

“Mwenyezi Mungu amekupa akili, maarifa na bahati ya kujiandikisha. Kwa hiyo unatakiwa kutumia fursa hiyo kwa kufanya uamuzi utakaoleta hatima njema kwa taifa.”

Katibu Mkuu wa ADC, Lydia Bendera aliwaomba wanawake kumchagua Yemba ili alete mabadiliko katika uongozi wa Tanzania. Aliwataka wanawake kuwapa kura wagombea wa ADC akisema ni chama pekee kati ya vinane ambacho kina sera madhubuti katika ukombozi wa mwanamke.

Naibu Katibu Mkuu, Doyo Hassan alisema sababu za chama hicho kuzindua kampeni zake kitaifa Tanga ni kuwapa fursa wananchi walio nje ya Dar es Salaam kuwajua wagombea makini.

“Hatuigi mambo ya vyama vingine, tumeamua kuzindua kampeni kitaifa Tanga badala ya Dar es Salaam, lakini pia hatukodi magari kuwaleta watu wala hatuwatumii wasanii kama kivutio cha kuja mkutanoni, sisi tunahitaji wanaokuja kusikiliza sera zetu,” alisema Doyo.

Sababu nyingine ni alisema ADC imepiga marufuku kwa wagombea wake kuwataja wagombea wa vyama vingine wakati wa kufanya kampeni kwa kutambua kwamba huko ni kujenga uhasama badala ya upendo na umoja.

“Hivi ADC itapata kura ngapi kwa kumsakama mgombea wa urais, ubunge au udiwani wa chama kingine? Hilo halipo kwetu tunataka upendo miongoni mwa Watanzania,” alisema.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment