Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 2 August 2015

LOWASSA VS CHADEMA, NANI ATAMBADILI MWENZAKE?

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiteta jambo la Edward Lowassa

Na Daniel Mbega
KIMBUNGA cha kisiasa kinatarajiwa kuanza kuonekana wiki hii Ukawa watakaporihia kwamba Edward Lowassa ndiye awe mgombea pekee wa urais kutoka umoja huo, akipitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Na kimbunga hicho kitakuwa kikubwa zaidi wakati Lowassa atakapochukua rasmi fomu ya kugombea urais katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hali ambayo italeta mafuriko makubwa.
Natabiri kwamba mafuriko hayo yanaweza kugeuka kuwa gharika pindi Lowassa atakapoanza kutambulishwa nchi nzima, kabla ya kuanza rasmi kwa kampeni za uchaguzi.
Sina uhakika kama Chama cha Mapinduzi (CCM) kina Mkakati B wa kukabiliana na gharika hiyo ingawa Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape Moses Nnauye, alitamba mjini Dodoma kwamba walifanikiwa kuzuia mafuriko kwa mikono.
Siku kadhaa zilizopita, CCM ilitaja sababu tano zilizokilazimu kuengua jina la Lowassa kati ya wagombea 38 wa urais huku chama hicho kikisisitiza kwamba taratibu zote zilifuatwa, ingawa Lowassa mwenyewe amekuwa akizungumza nje ya chama kwamba hakutendewa haki ndiyo maana ameamua kuhama.
Sababu zinazotajwa ni pamoja na; 1. Kukiuka taratibu za chama kwaani alionekana kufanya kampeni badala ya kutafuta wadhamini; 2. Kutoa rushwa kwa wanachama mbalimbali hivyo kukigawa chama na kama angepishwa kuwa mgombea CCM ilikuwa katika hatari ya kuwekewa pingamizi mahakamani lakini pia angeweka watu wake kwenye utawala kuwalipa fadhira; 3. Edward Lowasa aliwahonga wajumbe katika uchaguzi wa wajumbe NEC uliofanyika miaka iliyopita ili kupata watu wake ndani ya NEC; 4. Kuanza kampeni kabla ya wakati, alikuwa akisafirisha watu mbalimbali na kuwalipa fedha nyingi kisha kutoa taarifa kuwa walikuwa wakimtaka kugombea Urais, hii ni hadaa na hatari kwa chama; na 5. Kuwa na kashfa nyingi za ufisadi.
“Msemea sikioni siyo majinuni”, yawezekana kabisa CCM wanajua wanachokisema na ndiyo maana wao leo ndio wanaosema ‘Lowassa ni fisadi’ wakati Chadema alikokimbilia wanasema ‘Lowassa siyo fisadi’ japokuwa ni Chadema hao hao waliomwanika hadharani kwamba ni miongoni mwa mafisadi 11 wanaoiangamiza Tanzania katika ile ‘Orodha ya Aibu’ (List of Shame) pale Mwembeyanga Jumamosi ya Septemba 15, 2007.
Chadema, ambao siku zote walidai kwamba wana ushahidi na wakaitaka Serikali imfikishe Lowassa mahakamani, leo hii wamegeuka, wamebadilika na kusema kwamba mwanasiasa huyo ‘ni msafi’.
Kama tuhuma za kwamba wamepewa Shs. 10 bilioni ili kumkaribisha mwanasiasa huyo zitakuwa na ukweli wowote, basi nachelea kusema kwamba hakuna Mtanzania mwenye ujasiri wa kukemea ufisadi na kilichopo ni mazingaombwe tu ya watu wachache kutumia hoja za ufisadi ili waende Ikulu ya Magogoni.
Nakubaliana na maneno ya Mwalimu Ndimara Tegambwage aliyoyabandika wiki iliyopita kwenye mtandao wa kijamii wa facebook kwamba “Siasa haijawahi kuwa mchezo mchafu… Bali kuna watu wachafu kwenye siasa – na vyamavya siasa.”
Naam. Fedha inaweza kununua kila kitu: inaweza kununua nafasi katika Ukawa na mwenye tuhuma za ufisadi akateuliwa kugombea nafasi yoyote bila hata kufuata utaratibu.
Nataka kushawishika na maelezo ya mwanasiasa machachari mdogo wangu Zitto Zuberi Kabwe aliyoyatoa Januari 5, 2014 kuhusu tuhuma dhidi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akijibu mapigo ya Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu aliyeanza kumtuhumu yeye kwamba alihongwa magari mawili na Wakili Nimrod Mkono.
Zitto alisema, kama Mkono ndiye aliyemweleza Lissu kwamba alimhonga yeye Zitto magari, basi atakuwa alimweleza pia kwamba mwaka 2005 Mkono huyo huyo alimpa Freeman Aikaeli Mbowe Shs. 40 milioni ili Mbowe asifanye kampeni Musoma Vijijini; Atakuwa pia alimwambia kwamba mwaka 2008 (baada ya orodha ya mafisadi kutangazwa 2007) Mkono alimpa Mbowe Shs. 20 milioni za uchaguzi wa Tarime ambazo Mbowe alisema kwenye chama ametoa mkopo na akalipwa.
Zitto akaendelea kusema kwamba, kama Mkono alimwambia Lissu kuhusu kumhonga yeye magari, pia atakuwa alimwambia kwamba mwaka 2010 Mkono huyo huyo alimpa Mbowe Shs. 200 milioni za kampeni ya Dk. Slaa na hakusahau kumwambia kuwa Rostam Aziz (fisadi) pia alimpa Mbowe Shs. 100 milioni za kampeni bila kusahau kwamba gazeti la Tanzania Daima lilianzishwa na fedha kutoka chama cha Conservative cha Uingereza.
Akamtaka Lissu amuulize Mbowe aliingia deal (mkataba) gani na (Abdulrahman) Kinana na (Frederick) Sumaye mwaka 2005 kufuatia deni lake NSSF bila kusahau kuweka wazi mkataba kati yake na NHC kuhusu nyumba ya umma ilipo Club Bilicanas.
Naam. Hizo ndizo siasa na hiyo ndiyo michezo inayoendelea ndani yake. Sishangai kuona leo Chadema wamemuona yule yule waliyemwita fisadi, amekuwa muadilifu wa kutupwa.
Kinachonishangaza tu ni kitu kimoja, nani kati ya Lowassa na Chadema atakayeweza kumbadilisha mwenzake? Kama wamemwita ‘mtakatifu’ aliyekuwa ‘mwenye dhambi’, watawezaje kumbadilisha atakapokuwa madarakani hasa ikizingatiwa kwamba hata alipokuwa madarakani, Lowassa hajawahi kupinga hadharani vitendo vya rushwa na ufisadi na mafisadi wenyewe, ambao karibu wote waliotajwa na Chadema ni maswahiba zake?
Kimsingi, Chadema haitakuwa na jeuri wala uwezo wa kumbadili Lowassa kwa sababu tayari amekwishasema mapema kabisa kwamba yeye ‘anachukia umaskinina hawachukii matajiri’ ambao Chadema imewatangaza miaka mingi kwamba ni mafisadi. Kwa hili, kamwe Chadema haitaweza.
Lakini Lowassa yeye ameweza kuibadilisha Chadema vile atakavyo. Nguvu zake kisiasa na kifedha zimebadili mambo mengi ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani kwa sasa.
Kwanza; Lowassa kafanikiwa kubadili ratiba ya uchaguzi ya Chadema. Wakati ambapo tarehe ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea urais kupitia chama hicho ilikuwa saa 10 jioni Jumamosi, Julai 25, 2015, Chadema iliamua kusogeza mbele ratiba kutokana na kuendelea vikao vya siri vya kumshawishi Lowassa akiunge nacho.
Pili; Lowassa amefanikiwa kumbadili mgombea kipenzi wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, ambaye tangu kutua kwa Lowassa ndani ya chama hicho, kumekuwepo na hadithi nyingi kwamba huenda daktari huyo wa theolojia amejiengua ndani ya chama na siasa kwa ujumla. Chadema walijipimana kuona hakuna mtu ndani yao wala ndani ya Ukawa ambaye alikuwa na ubavu wa kukabiliana na mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, isipokuwa Lowassa.
Tatu; Lowassa ameibadilisha bajeti ya uchaguzi ya Chadema. Kwa fedha alizonazo, ni dhahiri kwamba bajeti ya kampeni za uchaguzi wa chama itapaa sana, japokuwa wanapaswa kuwa makini na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.
Nne; Lowassa amebadilisha kauli zao za ufisadi dhidi yake. Kama nilivyosema hapo juu, viongozi wengi, kama si wote, wa Chadema na hata Ukawa, wanaamini Lowassa ‘siyo fisadi tena’ kwa kutumia fomula ya namba hasi ikitoka kushoto kwenda upande wa kulia wa alama ya sawa sawa lazima itakuwa namba chanya! Watamnadi kwa kumtakasa kwa nguvu zote na ole wake atokee mtu akasema Lowassa fisadi, watapambana naye kila kona!
Tano; Lowassa kabadilisha Ilani ya Uchaguzi ya Chadema. Hivi sasa wataalam wachama hicho wamejichimbia kubadili vipengele mbalimbali vya ilani hiyo, hasa kwa kuzingatia kwamba sera za Lowassa ni kutowatupa matajiri ambao chama hicho kinawaita ni mafisadi. Nguvu zaidi ya kumkaribisha Lowassa inatajwa kutoka kwa Mbowe, ambaye huenda anajua maslahi yaliyo nyuma ya ujio wa Lowassa.
Kwa misingi hiyo basi, siyo rahisi Chadema – chama chenye haiba ya kupinga ufisadi nchini – kikambadili Lowassa kirahisi rahisi hivyo kama wengi wanavyodhani, bali ni wimbi jingine la ‘ufiadi’ ambalo litaingia Ikulu ikiwa Lowassa atashinda Oktoba 25, 2015.
Na endapo Ukawa itashindwa uchaguzi, hili ndilo litakalokuwa ‘anguko kuu’ la upinzani nchini.
Haya ndiyo niyaonayo.
0656-331974



No comments:

Post a Comment