Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 8 May 2015

MWAKA WA TAABU, DAR GHARIKA WATANO WATHIBITIKA KUFA MAJI!!

Wananchi wakipita kwa shida katika Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani jana baada ya kufurika maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha Dar es Salaam. Picha na Said Khamis 
Maji yakiwa yamefurika katika nyumba zilizopo eneo la Jangwani jana kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam. Picha na Salim Shao 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Hali ya jiji la Dar es Salaam jana ilizidi kuwa mbaya kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuwaweka wakazi kwenye hali ngumu zaidi baada ya kukumbwa na matukio mengine makubwa yaliyoathiri jiji na sehemu nyingine kote nchini tangu kuanza kwa mwaka.
Mvua hizo kubwa zinazolingana na zile zilizonyesha miaka mitatu iliyopita na kusababisha usumbufu mkubwa, jana zilisababisha nyumba kadhaa kuanguka, madaraja kukatika, barabara kufungwa, ikiwapo ya Morogoro, usafiri kuwa mgumu kutokana na misururu mirefu ya magari na Jeshi la Polisi kulazimika kutoa tamko la kushauri wananchi kutoka mapema maofisini ili kuwahi majumbani.
Matukio hayo yametokea siku chache baada ya kusitishwa kwa mgomo wa pili wa madereva uliosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri karibu nchi nzima. Madereva waliamua kufanya mgomo huo kupinga masharti mapya ya kupata leseni yaliyotolewa na Serikali ikiwa ni mkakati uliobuniwa kukabiliana na ajali ambazo tangu Januari mwaka huu zimeua zaidi ya watu 900.
Mwaka 2015 pia umeanza kwa mgomo wa nchi nzima wa wafanyabiashara, kuibuka upya kwa mauaji ya albino, tishio la ugaidi lililoambatana na mauaji ya polisi na kugundulika kwa vituo vya mafunzo ya kigaidi kwa watoto wadogo, kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya shilingi, kuvurugika kwa mchakato wa katiba na mvua ya mawe iliyoua watu kadhaa mkoani Shinyanga.
Kwa muda wa siku mbili, mvua zimenyesha mfululizo na kusababisha mafuriko kwenye sehemu kadhaa za Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha biashara na shughuli za Serikali, likiwa na takriban watu milioni 4.4 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Pamoja na mvua hizo kunyesha kwa wingi jijini Dar es Salaam, athari zake zinategemewa kugusa mikoa mingine yote kutokana na umuhimu wa jiji kiuchumi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa daraja la Mwanamtoti lililopo eneo la Mbagala Kuu limeng’olewa na mafuriko hayo.
Kamanda Kova alisema Barabara ya Morogoro imefungwa eneo la kati ya Magomeni na Fire kutokana na Mto Msimbazi kufurika na kusababisha maji kupita juu ya daraja.
Alisema nyumba za watu wanaoishi Magomeni Mikumi zimejaa maji na hivyo Jeshi la Polisi limetoa amri kwa watu wote kuondoka eneo hilo.
Kova alisema barabara nyingine iliyofungwa ni ya Kinyerezi ambako maji yalikuwa yakiongezeka na kutishia kulisomba daraja linalounganisha Kinyerezi na Majumba Sita.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Temeke, Andrew Satta alisema daraja lililopo eneo la Mwanamtoti eneo la Mbagala Kuu limeng’olewa na mafuriko na kusababisha kukatika kwa mawasiliano.
“Nimewaagiza vijana wangu watembelee sehemu mbalimbali ili kuangalia maeneo ambayo yameathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam,” alisema Satta.
Wakati huohuo, meya wa Manispaa ya Temeke, Maabad Hoja alisema Barabara za  Kimbiji, Mpemba Mnazi zimekatika kutokana na mvua hizo na kuvuruga mawasiliano.
Hoja alisema halmashauri hiyo italazimika kuchukua hatua za haraka hivyo itaundwa kamati ili kuangalia  jinsi gani ya kutatua tatizo hilo.
“Hatua ya kwanza, tunawaagiza watendaji wa kata watuletee taarifa zilizopo kwenye maeneo yao kuhusu mvua zinazoendelea kunyesha,” alisema Hoja.
Hadi sasa tathmini halisi ya hasara iliyopatikana haijawekwa bayana, lakini wakazi wa jijini hapa waliozungumza na gazeti hili wameeleza jinsi walivyoathirika na mvua hizo za siku mbili pamoja na mgomo wa madereva uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Jumatatu.
“Hata leo, tulikuwa na kipindi lakini kutokana na mvua zinazoendelea, mhadhiri ametutangazia kusitisha darasa baada ya wanafunzi wengi kueleza kuwa huko waliko foleni ni ndefu tofauti na siku za kawaida,” alisema Athile Mputa, mwanafunzi wa shahada ya pili wa  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye pia alikosa vipindi wiki hii kutokana na mgomo wa madereva.
“Hali inaniongezea mzigo wa masomo ambayo nitalazimika kuyatafutia muda mwingine ili kukamilisha mtalaa,” aliongeza Mputa ambaye ana anahudhuria masomo ya jioni UDSM.
Mvua zinazoendelea zimewaathiri wafanyakazi ambao ofisi zao zipo katikati ya mji. Hali hiyo ilithibitishwa na Elibariki Mushi anayefanyakazi katika tawi la benki moja lilipo katikati ya mji.
“Jana (juzi) nilitoka ofisini saa 1:30 jioni lakini nilifika nyumbani kwangu (Tabata-Segerea) saa 7:00 usiku. Nilikuwa nimechoka hata hivyo sikupata muda wa kulala vya kutosha kwani niliwahi kuamka na kwenda ofisini saa 12:00 alfajiri. Hata hivyo, nilifika saa 6:00 mchana. Hata kazi nashindwa kufanya, hasa nikifikiria foleni ya kurudi tena nyumbani… sijui nitoke saa ngapi ili niwahi,” alisema.
Licha ya hao, wafanyabiashara pia wamepoteza kipato na kuyumba kiuchumi kwa muda. Wengine wamelazimika kukopa ili kuendesha familia baada ya kutofanya mauzo yoyote kwa wiki nzima.
Jackline Champanda, ambaye anafanya biashara ya maji maeneo ya Mbagala, anasema kuwa hali hii ni mbaya kwake tangu aanze biashara hiyo kwani amepoteza mapato kiasi cha kushindwa kuihudumia familia yake.
“Sikujua kama kutakuwa na mgomo wa madereva hivyo nilipoteza Sh20,000 nauli ya kwenda na kurudi kwa Jumatatu pekee. Hata siku iliyofuata, asubuhi ilikuwa hivyo. Lakini pamoja na hilo bado biashara siyo nzuri hata kidogo… watu hawanunui maji wala juisi kama inavyokuwa siku zote,” alisema.
Jackline anayeishi Ubungo, alifafanua kuwa hali hiyo imemkuta ikiwa ni siku chache baada ya kununua mzigo mkubwa kwa ajili ya duka lake hivyo hali inayoendelea kuwa janga kwake.
Wapo wanafunzi waliokosa masomo pia kutokana na mvua zinazoendelea. Chacha Marigo, mkazi wa Chanika, alisema kuwa watoto wake hawakwenda shule jana baada ya kukosa usafiri.
“Niliondoka nyumbani saa 12:00 alfajiri na niliwaacha wanangu wawili kituoni ambako basi la shule huwapitia kila siku. Lakini nilipopiga simu shuleni baadaye ili kujua kinachoendelea mkuu wa usafiri alinijulisha kuwa gari halikupita katika mzunguko leo (jana). Watoto walirudi nyumbani,” alisema Marigo.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Loyola, Pontain Kashangashi aliliambia Mwananchi kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha shule imelazimika ‘kulegeza’ baadhi ya masharti ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo.
Kashangashi alisema kuwa siku mbili mfululizo baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakifika shuleni bila ya sare za shule huku wengine wakichelewa kufika kutokana na mvua hizo ambazo pia zimesababisha kukosekana na kwa usafiri hasa wa kuingia katikati ya jiji.
Alieleza kuwa ratiba ya shule inawataka wanafunzi kufika shuleni saa 12:30 asubuhi lakini kutokana na mvua wengi wamekuwa wakichelewa wakiwamo baadhi ya walimu. “Wanatembea kwenye mvua kwa muda mrefu, wanakuja nguo zimeloana hasa viatu ndio vinaharibika sana. Tumeamua hata masomo ya jioni tuyaondoe ili wanafunzi waondoke mapema,” alisema Kashangashi.
Victoria Kishimbo, mkazi wa Kijichi, alisema kuwa tangu mgomo wa mara ya pili wa madereva na mvua zinazoendelea kunyesha zimemuathiri kwa kiasi kikubwa kwa kuwa amekuwa akichelewa kwenda hospitali kumpelekea chakula dada yake aliyelazwa katika Hospitali ya Temeke.
“Ule mgomo ulinichelewesha kupeleka chakula kwa mgonjwa, yaani nilikaa kituoni hadi muda wa kuona wagonjwa ukaisha. Nilipofika hospitali nilimkuta amesubiri hadi amechoka, kibaya zaidi chakula chenyewe kilikuwa kimepoa,” alisema Victoria.
Alisema baada ya kusikia mgomo umekwisha alijua hali ingekuwa nzuri, lakini kinyume chake usafiri wa daladala umekosekana kutokana na mvua zinazoendelea Dar es Salaam. “Mvua zinaanza kunyesha tangu saa 11:00 asubuhi, ukienda kituoni hakuna usafiri magari mengi yamekwama kwenye foleni. Sijui hali hii nayo itaisha lini,” alisema.
Wakati wakazi hao wa jijini Dar es Salaam wakitafakari matukio hayo makubwa yaliyotokea wiki hii, hali haijawa nzuri nchini tangu mwaka 2015 uanze kutokana na matukio mengi kulikumba Taifa, baadhi yakiwa yanatishia amani na usalama wa nchi.
Katika hatua nyingine, Mvua kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo tangu juzi imesababisha vifo vya watu watano huku mamia wakikosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.
Mvua hiyo iliyofikia kipimo cha milimita 132.5 kwa mujibu wa vipimo vilivyofanywa katika kituo cha Shule ya Msingi ya Maktaba, ilisababisha barabara kujaa maji na nyingine kuharibika na madaraja kadhaa kukatika.
Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa, Dk Agnes Kijazi alisema jana kwamba kipimo hicho cha mvua ni cha juu mno kulinganisha na kile cha wastani ambacho ni kati ya milimita 16 na 30.
“Kwa takwimu za mwezi Mei, kiwango hiki hakijawahi kufikiwa kwa miaka 10 iliyopita.” Alipotakiwa kufafanua miezi mingine, Dk Kijazi alisema hakuwa na takwimu kwa kuwa alikuwa nje ya ofisi.
Awali, Dk Kijazi alitoa taarifa ikisema mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuwa “hali ya mvua inatarajiwa kuendelea katika baadhi ya siku hadi Mei 20, mwaka huu”.
“Mamlaka inaendelea kushauri wakazi wa maeneo hatarishi pamoja na watumiaji wa bahari kuchukua tahadhari,” alisema Dk Kijazi.
Watano wafa
Kutokana na mafuriko hayo, watu watano wakiwamo watoto wawili, walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema waliopoteza maisha ni watoto wawili na mzee mmoja ambao majina yao hayajafahamika.
“Mtoto mmoja (2) alisombwa na mafuriko katika eneo Machimbo ya Makangarawe na mzee mmoja alifariki jana baada ya mvua kunyesha na kujaa ndani ya nyumba yake. Mtoto mwingine ambaye bado hajapatikana alisombwa na mafuriko pia,” alisema Sadick.
Hata hivyo, habari zilizopatikana wakati tunakwenda mitamboni zilisema kuwa waliopoteza maisha ni watu watano.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaja mtu aliyefariki dunia kuwa ni Shabani Idd (73) mkazi wa Manzese.
Maeneo mengine
Katika eneo la Mbezi Luis, Mto Mbezi ulifurika, hali iliyosababisha nyumba zilizojengwa kandokando ya daraja hilo kufunikwa na maji.
Mkazi wa eneo hilo, John David alisema hali ilikuwa mbaya zaidi jana asubuhi kwani maji yalifurika na kujaa barabarani na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji.
Alisema wakazi walio karibu na mto huo walichukua tahadhari tangu juzi na kuhama makazi yao.
“Haikuwa rahisi kwa wao kuendelea kukaa hapa wakati wanafahamu hali kama hii ingetokea. Tangu jana jioni familia zinazoishi huko ziliondoka, lakini vitu vyao vimesombwa na maji na nyumba moja imesombwa pia,” alisema David.
Maeneo ya Boko Basihaya, zaidi ya nyumba 20 zilikuwa zimezingirwa na maji huku familia kadhaa zikilazimika kukimbia nyumba zao na kutafuta makazi ya muda kuanzia juzi usiku hadi jana.
Timu ya waandishi wa Mwananchi ilifika katika eneo hilo na kushuhudia maji yakiwa yamejaa kwenye nyumba zilizojengwa kandokando ya bwawa linalotiririsha maji kuelekea baharini.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Dionise Swai alisema baada ya maji kujaa nyumbani kwake, alilazimika kuyanyonya kwa kutumia pampu ili kunusuru mali zake.
“Niliyawahi kwa hiyo hayakuingia. Wanafamilia wengine wameondoka nimebaki mwenyewe,” alisema.
Mkazi wa mwingine eneo hilo, Frank Shuma alizitupia lawama mamlaka kwa kushindwa kujenga mifereji ya kutiririsha maji kwenda baharini.
Hali kama hiyo pia ilitokea eneo la Kinondoni Hananasif ambako maji yalijaa na kufunika baadhi ya nyumba.
Katika daraja la Kawe, wananchi walikuwa kwenye harakati za kuokoa mali zao zilizosombwa na maji, yakiwamo magodoro, vyombo na nguo.
Maji yalijaa kwenye barabara na kusababisha vyombo vya moto na watembea kwa miguu kupita kwa shida huku magari mengine yakilazimika kusimama pembeni.
Barabara ya Haile Selassie, upande wa baharini karibu na Hoteli ya Sea Cliff, eneo hilo lilifunikwa na maji na kusababisha usumbufu kwa vyombo vya moto na madereva kulazimika kuendesha kwa mwendo wa taratibu na kusababisha foleni.
Watumiaji wa barabara ya Mwai Kibaki walikuwa na wakati mgumu kupita, wengi walionekana wakiwa wamevua viatu au kutafuta njia mbadala kukwepa maji yaliyokuwa yamejaa barabarani.
Mkazi wa Ubungo Kibangu, Julieth Kibakaya alisema hofu imetanda kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na athari zinazosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha hasa mafuriko.
“Huku kwetu hali ni mbaya. Mafuriko yamebomoa nyumba mbili hadi sasa. Hivi sasa wanafamilia hao hawana makazi tena imebidi wapewe hifadhi ya muda na majirani zao na hali ikiendelea hivi tunahofia wakazi wengi wa eneo hili watapoteza nyumba zao,” alisema Kibakaya.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment