Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Sunday 24 May 2015

BAJETI YA WIZARA YA KILIMO NA CHAKULA YAPITISHWA NA WABUNGE 68



Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dodoma.  Ni wabunge 68 tu, wakiwamo mawaziri 10, waliokuwa ndani ya ukumbi wa Bunge wakati chombo hicho cha kutunga sheria kikipitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo na Chakula, lakini uongozi umesema “hakuna tatizo”.
Bunge la Jamhuri ya Muungano linatakiwa liwe na wabunge 357 iwapo kumetokea muujiza wakahudhuria wote.
Idadi hiyo ndogo ya wabunge kwenye kikao muhimu cha kupitisha bajeti imetia fora kwenye kikao cha 11 cha Bunge la 10 ambalo limetawaliwa na utoro katika mikutano yake ya mwisho kutokana na akili za watunga sheria hao kuwa majimboni.
Licha ya idadi hiyo ndogo, bajeti hiyo ilipitishwa kwa kutumia utaratibu wa “guillotine”, ambao wabunge hutakiwa na kiti cha Spika kutohoji jambo lolote katika vifungu mbalimbali vya bajeti husika anapoona havunji sheria.
Utaratibu huo hutumika wakati muda wa kawaida wa kikao husika au wa nyongeza unapomaliza huku utaratibu wa kupitisha vifungu ukiwa bado haujakamilika.
Akizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu ambaye aliongoza kikao cha jana asubuhi, alisema: “Bajeti za wizara zinaweza kupitishwa hata kama idadi ya wabunge ikiwa ndogo.  Katika bajeti kuu (wa wizara ya fedha) hapo ni lazima wabunge wote wawepo, akidi lazima izingatiwe.”
Kanuni ya 77 ya Bunge inayozungumzia akidi ya wabunge inayohitajika katika kikao cha Bunge kwa ajili ya kupitisha maamuzi, inaeleza kuwa lazima wawe zaidi ya nusu ya wabunge wote.
Hata hivyo, iwapo mbunge atasimama na kuomba muongozo wa Spika kama ataona ikidi ni ndogo, kiti cha spika kinaweza kutoa uamuzi wa wabunge wote kuhesabiwa na kisha kuwahoji wabunge kama wataridhia bajeti kupitishwa na idadi hiyo ama la. Jambo hilo halikutokea jana kwa sababu hakuna mbunge aliyehoji.
Pia, kanuni ya 146 ya bunge inaeleza kuwa mbunge atakwama kuwa mbunge iwapo hatahudhuria vikao vitatu mfululizo bila kutoa taarifa rasmi kwa Spika wa Bunge.
Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda alisema kuwa jambo hilo si sawa na kinachofanyika ni “kufunika kombe mwanaharamu apite”.
“Ninachokiona ni mambo ya kuburuzwa tu. Yaani ili mradi tu bajeti imepita. Idadi inatakiwa kuwa nusu au kuzidi,” alisema mbunge huyo wa zamani wa CCM.
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja alisema kuwa kanuni za bunge zinaruhusu jambo hilo.
“Bajeti hizi za wizara siyo mwisho. Kinachozingatiwa zaidi ni bajeti kuu ya Serikali. Wakati wa kupitisha bajeti hiyo ni lazima akidi izingatiwe,” alisema Ngeleja ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Jana wakati Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo, kulikuwa na wabunge 39 tu ndani ya ukumbi wa Bunge, baadaye wakaongezeka hadi 47.
Wakati Wasira na Naibu wake, Godfrey Zambi wakianza kujibu hoja za wabunge, ukumbi ulikuwa na wabunge 51 na baadaye waliongezeka wanane.
Mpaka Bunge linakaa kama kamati saa 7:05 mchana kupitisha bajeti hiyo, wabunge walikuwa wamefika 68.
Mawaziri waliokuwepo bungeni wakati huo ni Wasira, Zambi, George Mkuchika (Ofisi ya Rais- Utawala Bora), Samuel Sitta (Afrika Mashariki) na Hawa Ghasia (Ofisi ya Rais-Tamisemi).
Wengine ni Gaudencia Kabaka (Kazi na Ajira), Mary Nagu (Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu), Profesa Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais-Kazi maalum), Adam Malima (Naibu Waziri- Fedha) na Charles Mwijage (Naibu Waziri-Nishati na Madini).
Kati ya wabunge 68, wa upinzani walikuwa 15 na wa CCM walikuwa 53.
 Kutokana na kufika saa 7:48 mchana huku Bunge likiwa halijamaliza kupitisha bajeti hiyo, Zungu alilazimika kutumia utaratibu wa ‘guillotine’ wakati wabunge wakihoji baadhi ya mambo kwenye bajeti hiyo.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment