
Waziri Kiongozi mstaafu wa Awamu ya Sita, Shamsi Vuai Nahodha.PICHA|MAKTABA YA MWANANCHI
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar. Waziri Kiongozi mstaafu wa Awamu ya Sita, Shamsi Vuai Nahodha amesema tatizo la kuingia mikataba mibovu nchini litaisha kwa kuanzishwa utaratibu wa mikataba yote kuidhinishwa na Bunge, baada ya kuipitia na kuona kama ina tija kwa taifa.
Nahodha anaeleza hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika nyumbani kwake huko Chukwani na kueleza kuwa hatua hiyo ikifikiwa itajenga na kutanua uwazi, kuaminiana, kuongozwa na nguvu ya uzalendo.
Alisema mbali ya uwazi kutapunguza kutuhumiana na kunyoosheana vidole visivyo na ushahidi hata pale mhusika anapofanya kwa kujali masilahi ya Taifa.
Nahodha alisema Serikali lazima iweke rasilimali fedha za kutosha na wataalamu wa mambo ya uchunguzi ili Tume ya Maadili iweze kufanya kazi zake za kuchunguza watendaji na viongozi wanaovunja na kukiuka miiko ya uongozi na kuhakikisha lengo la kuimarisha misingi ya utawala bora inafikiwa na kutekelezeka.
Alisema kulingana na ukubwa wa nchi, Tume inashindwa kuwafuatilia kwa undani na kutaka Tume hiyo ipewe uzito kulingana na umuhimu wa kazi zake na kueleza tatizo la rushwa na uhujumu uchumi haliwezi kuondoka bila ya kuwa na nia au utashi wa kupambana na mambo hayo kwa vitendo.
“Rushwa si jambo jepesi, unapotaka kupambana na jambo hilo uwe tayari kuongeza maadui na wakati mwingine kuanguka kwa maadili na malezi katika familia kumechangia sana kukithiri kwa vitendo vya rushwa, iweje mtoto katika familia anajenga nyumba nne za ghorofa kwa muda mfupi, familia yake badala ya kumchunguza huonekana kama shujaa na mitaani kuogopwa,” anasema Nahodha.
Alisema kwamba tatizo la rushwa na ufisadi lazima liwekewe mikakati mikubwa ikiwemo kuimarisha misingi ya utawala bora kwa kuvipatia rasilimali fedha na wataalamu wa vyombo vya kusimamia sheria.
Nahodha alisema kuwa nchi kama Ghana imeweka masharti katika Katiba Miradi kuanzia Dola40 milioni lazima ziidhinishwe na Bunge kwa nini Tanzania tunashindwa wakati tayari mikataba imeanza kuleta matatizo makubwa na kuathiri maendeleo ya Taifa.
Alisema kwamba kama utaratibu wa Bunge kupitia mikataba kabla ya kufikiwa Serikali utafanyika kwa kiwango kikubwa tatizo la mikataba mibovu litadhibitiwa badala ya mikataba kuendelea kufungwa chini ya meza bila kuwapo uwazi.
“Nchi zote duniani zinazosimamia misingi ya utawala bora kwa vitendo suala la uwazi ni muhimu na wakati umefika mikataba kupelekwa bungeni kupitishwa kabla ya kufikiwa na Serikali kwa manufaa ya Taifa,” alisisitiza Nahodha.
Vilevile, alisema kilio cha wabunge kutaka mikataba yenye utata kupelekwa mbele ya Bunge kisingelikuwepo kama mikataba ingelikuwa inapitishwa bungeni kabla ya kufungwa na Serikali.
Hata hivyo, alisema utaratibu wa mikataba kupitiwa kabla ya kufungwa na Serikali unatakiwa pia kuwapo Zanzibar kwa Baraza la Wawakilishi (BLW), hasa wakati huu Zanzibar ikielekea katika mambo ya Utafiti na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia visiwani humo.
Alisema kwamba nishati ya mafuta na gesi zina faida na hasara yake na kutaka Zanzibar kujifunza kupitia mataifa mengine ambayo yameingia migogoro mikubwa na kuteteresha amani ikiwamo Sudan, Nigeria Libya na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati.
Alikumbusha kwamba pamoja na Zanzibar kufanikiwa kuliondoa suala la mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano kupitia rasimu mpya ya Katiba Inayopendekezwa lazima suala la utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi kufanyika kwa umakini mkubwa katika ufungaji wa mikataba yake na Baraza la Wawakilishi lipewe nafasi ya kupitia kabla ya Serikali kufikiria kufunga mkataba kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
“Upande wa Zanzibar unajiandaa vipi na suala la utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi, jambo hilo lina ushawishi mkubwa wa rushwa na mikataba yake muhimu ipitiwe na Baraza la Wawakilishi kabla ya kufikiwa na Serikali,” alisema Nahodha.
Kuhusu Mamlaka ya Kupambana na Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar kutokuwa na kesi hata moja mahakamani tangu kuundwa kwa chombo hicho miaka mitatu, Nahodha alisema kinachoonekana ni kukosekana kwa rasilimali-fedha na wataalamu wa fani mbalimbali katika mamlaka hiyo.
Alisema kwamba chombo hicho kina umuhimu mkubwa katika kujenga misingi ya utawala bora kwa kuhakikisha rushwa inadhibitiwa katika sekta muhimu za huduma za jamii visiwani Zanzibar.
Vilevile alisema kazi ya kupambana na rushwa inahitaji kujitoa mhanga kwa kukubali kuchukiwa na wachache na kuwafariji waliokuwa wengi kwa manufaa ya Taifa na wananchi wake.
Hata hivyo, alisema Zanzibar ina watu 1.5 milioni kama chombo hicho kitajengewa uwezo wa rasilimali-fedha na wataalamu tatizo la rushwa Zanzibar litabakia hadithi.
Alionya kwamba chombo hicho hakiwezi kuleta mafanikio kwa njia ya mkato lazima kipate ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi ikiwamo kufichua wanaotoa na kupokea rushwa bila ya kujali nyadhifa zao kwa manufaa ya umma.
Alieleza kama Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) litachukua hatua mbalimbali za kuendelea kuhoji utekelezaji wa maagizo yake kwa Serikali kupitia ripoti za kamati teule za kuchunguza ubadhirifu na ufisadi lengo la kuimarisha misingi ya utawala bora litafikiwa kwa wakati mwafaka Zanzibar.
Kamati za uchunguzi za BLW zinafanya kazi nzuri lakini bado zinakabiliwa na jukumu la kufuatilia utekelezaji wa ripoti zake kwa maagizo wanayotoa kwa Serikali kama tunavyoona katika Bunge,” alisema Nahodha.
Alisema kwamba matatizo ya rushwa na ubadhirifu yapo Zanzibar na kuathiri sekta za huduma na njia ya pekee ya kuondoa matatizo, kwanza wananchi kupewa elimu kuhusu madhara ya rushwa na mamlaka ya kupambana na rushwa kujengewa uwezo wa kifedha na wataalamu.
“Hatuwezi kujenga nchi yenye uchumi imara kama kuna watu wanaendelea kufanya ufisadi na ubadhirifu wa kutisha,” alisema Nahodha.
Akijibu swali la kujiuzulu kwake katika nafasi ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alisema aliwajibika kwa lengo la kuheshimu utendaji wa pamoja baada ya waliokuwa chini yake kukabiliwa na shutuma ambazo zilikuwa chini ya usimamizi wake ingawaje hakuwa mhusika na mshiriki wa jambo lililodaiwa kufanyika.
“Kama wizara ikifanya mambo mazuri sifa huwa ni za waziri, yanapofanyika mambo ambayo si mazuri unalazimika pia kukubali mambo hayakuwa mazuri, kuondoka kwako kwa aina hiyo kunatoa nafasi ya wenzako na vyombo vingine kukuchunguza na kujiridhisha, unapobaki unaweza kuwatia shaka wenzako wasikupekue na kujiridhisha,” alisema Nahodha.
Akizungumzia wagombea waliojitokeza kutaka kurithi nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, alisema Taifa la Tanzania linaongozwa na binadamu siyo malaika kwa msingi huo hakuna mtu asiyekuwa na kasoro katika maisha.
“Hakuna binadamu msafi kama karatasi nyeupe, wagombea 12 waliotangaza nia kila mmoja ana sifa na kasoro zake muhimu kuangalia nani mwenye kasoro chache na kuuzika kwake kwa wapiga kura,” alisema Nahodha ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya CCM na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Alisema kwamba chama hicho kimeweka sifa na vigezo 13 kabla ya mwanachama wake kuchaguliwa na chama kugombea wadhifa huo, lakini pia muhimu awe anakubalika na pande mbili za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Nahodha mbali ya kuwa Waziri Kiongozi mstaafu, Mwakilishi wa Jimbo la Mwanakwerekwe na Mbunge wa kuteuliwa pia amewahi kushika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kabla ya kujiuzulu mwaka huu.
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment