Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 7 November 2014

KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AANZA NA MUHIMBILI

Rais Jakaya Kikwete akipeana mkono na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando baada ya kumwapisha Ikulu, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu 
Dar es Salaam. Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando ameutaka uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kupitia upya uamuzi wa kupandisha bei za baadhi ya huduma zao ili kuangalia namna ya kupunguza adha kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete Ikulu jana, Dk Mmbando alisema baada ya kupitia uamuzi huo, atauita uongozi huo wizarani kujadiliana njia za kupunguza bei na pia zitakazoifanya hospitali hiyo kuendeleza utoaji huduma kwa ufanisi.
Hivi karibuni, MNH ilipandisha bei ya kulaza wagonjwa kwa kitanda kuwa Sh5,000 kwa siku na Sh2,000 kwa ajili ya chakula. Bei hizo ni tofauti na za awali ambazo mgonjwa alitakiwa kulipa Sh20,000 kwa ajili ya huduma hizo mara anapoingia hospitalini hapo hadi anaporuhusiwa.
Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Dk Marina Njelekela alisema hatua hiyo ililenga kukabiliana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na kupunguza deni la Sh8 bilioni ambalo taasisi yake inadaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Alipoulizwa jitihada zake za kutatua tatizo la uhaba wa dawa katika vituo vya afya nchini, Dk Mmbando ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali alisema kwa sasa bajeti ya Serikali imeshapita ila wataweka mkazo katika ununuzi wa dawa katika mwaka wa fedha ujao ili kuzuia hali kama hii isitokee tena.
Dk Mmbando ni miongoni mwa makatibu wakuu, mabalozi na makatibu wa mikoa wapya walioapishwa jana na Rais Kikwete.
Makatibu Wakuu wengine walioapishwa ni Dk Yohana Budeba (Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Mhandisi Mbogo Futakamba (Wizara ya Maji) na Dk Adelhelm Meru anayekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kabla ya uteuzi wao, Dk Budeba na Futakamba walikuwa Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara walizoteuliwa kuziongoza wakati Dk Meru alikuwa ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Pia mabalozi Jack Zoka anayekwenda Canada na Samuel Shelukindo anayekuwa Msaidizi wa Rais Masuala ya Diplomasia waliapishwa. Shelukindo alikuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.
Pia aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Charles Pallangyo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa Geita na Addo Mapunda aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji Manispaa ya Bukoba amekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Arusha.
Wakuu wa mikoa
Pia waliapishwa wakuu wa mikoa wanne wapya ambao ni Dk Ibrahim Msengi (Katavi), Amina Masenza (Iringa), Halima Dendego (Mtwara) na John Mongella anayekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Juzi, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa mikoa na kuwahamisha sita huku wengine watatu kuwapangiwa kazi nyingine.
Waliokuwa wakuu wa mikoa ya Iringa, Dk Christine Ishengoma, na Kanali Fabian Massawe (Kagera) watapangiwa majukumu mengine. Kanali Joseph Simbakalia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ameteuliwa kujaza nafasi ya Dk Meru, EPZA.
Dk Msengi alishukuru kwa kuaminiwa na kupatiwa nafasi hiyo huku akibainisha kuwa changamoto namba moja ni kukamilisha mradi wa maabara katika shule za kata.
“Bado sijafika nikazisikie changamoto nyingine lakini kitu cha kwanza ni kukaa na wenzangu tuone walipofikia na kutafuta njia za kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kabla ya Desemba kama Rais alivyoagiza,” alisema Dk Msengi.
Masenza aliomba ushirikiano akisema hana majibu ya moja kwa moja juu ya mikakati ya maendeleo kwa kuwa ndiyo kwanza anakwenda kuanza kazi.
“Sina majibu binafsi kwa sasa ila nimedhamiria kuifanya kikamilifu kazi hii kwa ushirikiano na wenzangu. Ila cha msingi ni kuhakikisha mahitaji yote ya kitaifa ya maendeleo yanatimizwa,” alisema Masenza.
Kabla ya kuteuliwa juzi, Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mwanza; Dk Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kilimanjaro na Mongela alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.
“Nashukuru kwa Mheshimiwa Rais Kikwete kuniamini na kunipatia nafasi hii cha msingi ni kuhakikisha naongeza pato la wakazi wa Mtwara,” alisema Dendego.
Alipoulizwa juu ya mikakati ya kuimarisha amani katika mkoa huo uliokuwa umetawaliwa na vurugu za gesi, Dendego alisema: “Nashukuru kwamba tayari kumeshatulia na kuna amani tofauti na awali.”
Mongella aliyewahi kufanya kazi katika Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), alisema baadhi ya vipaumbele vyake ni ulinzi na usalama, maendeleo na utii wa sheria.
“Sina miujiza. Kila mmoja anajua majukumu yake hivyo ushirikiano wa kina na watumishi wenzangu utatufanya tufikie malengo,” alisema Mongella huku akibainisha ushirikiano pia na wananchi wataongeza ulinzi na usalama katika mkoa huo wa mipakani na nchi jirani.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Balozi Zoka alisema amepokea kwa furaha uteuzi huo na kuongeza kuwa changamoto kubwa ni namna ya kuiwakilisha nchi kikamilifu huko Canada.
“Canada wameendelea sana na wamewekeza hapa nchini katika sekta ya gesi hivyo kama balozi naimarisha uhusiano baina ya nchi hizi kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchi hiyo,” alisema Zoka.
Uhamisho mwingine
Katika mabadiliko hayo ya wakuu wa mikoa wengine wamehamishwa vituo vya kazi. Magesa Mulongo anayetoka Arusha kwenda Mwanza, Dk Rehema Nchimbi anakwenda Njombe kutoka Dodoma, Ludovick Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kapteni Aseri Msangi anayekwenda Mara kutoka Njombe na Everist Ndikilo anakwenda Arusha kutoka Mwanza.
Wengine ni Chiku Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dk Rajab Rutengwe anayekwenda Tanga kutoka Katavi, Fatma Mwasa anakwenda Geita kutoka Tabora na Magalula S. Magalula anayehamishiwa Lindi akitokea Geita.
Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.
CREDIT: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment