Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema mambo yanayotokea sasa nchini, kama viongozi kuwa na akaunti nje ya nchi na kudai ni ‘vijisenti’, Serikali kuingia mikataba yenye utata isiyohojiwa popote ni matokeo ya nchi kuwa na Katiba yenye maswali mengi kuliko majibu.
Akizungumza katika mdahalo wa Katiba uliokuwa na mvuto wa aina yake kwa watu kushangilia kila mjumbe aliyakuwa anazungumza ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba huku akitumia zaidi mifano alisema mambo hayo yanaweza kuendelea kwa sababu hata Katiba Inayopendekezwa pia ‘imeyabariki’.
Katika mdahalo huo Jaji Warioba aligusia ufisadi wa Sh306 bilioni za Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa ajili ya kuhifadhi fedha zilizokuwa zikilipwa na Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) kwa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, kuwa ni matokeo ya kuwa na Katiba isiyo na majibu.
Huku akijinadi kuwa yeye ni mwanachama hai wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jaji Warioba alisema kuna ‘CCM imara’ na ‘CCM maslahi’ na kwamba tabia yake ya kutoa changamoto ya masuala mbalimbali imetokana na kujengwa na Mwalimu Julius Nyerere.
Alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na mmoja wa washiriki wa mdahalo huo kutoka Umoja wa Vijana wa CCM, Senga Abubakar aliyetaka kujua kama Jaji Warioba ataiunga mkono Katiba Inayopendekezwa, iwapo itapitishwa katika kura ya maoni.
Mdahalo huo ni wa tatu kufanywa na taasisi hiyo, baada ya ule wa pili uliofanyika katika Hoteli ya Blue Pearl Novemba 2 mwaka huu na kuvunjika kutokana na kuibuka vurugu, huku Jaji Warioba akishambuliwa alipokuwa akihitimisha hotuba yake kwa kuhoji watu wanaotumia vibaya jina la Mwalimu Julius Nyerere kupitisha hoja zao katika misingi isiyokubalika.
Tofauti na mdahalo wa pili, mdahalo wa jana ulikuwa na ulinzi mkali wa polisi na mamia ya washiriki walikaguliwa kabla ya kuingia ukumbini na kutakiwa kuandika majina ili idadi yao iweze kutambuliwa.
Katika mdahalo huo, Jaji Warioba aliambatana na waliokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole, Profesa Mwesiga Baregu, Joseph Butiku na Mohammed Yusufu Mshamba.
Huku akishangiliwa na mamia ya washiriki wa mdahalo huo, Jaji Warioba alisema, “Tume ya Katiba ilipendekeza miiko na kanuni za uongozi lakini Bunge Maalumu la Katiba limeyaondoa na kuyaweka katika msingi wa utawala bora.
“Hivi huwezi kuwa mzalendo na mwadilifu mpaka uwe kiongozi? Hii si misingi ya utawala bora ni misingi ya kitaifa na inamhusu kila mmoja wetu.”
Alisema lengo la kuweka suala hilo ni kutaka zawadi wanazopewa viongozi ziwe za taifa, “Maana yake kama umepewa zawadi inakuwa ya taifa siyo ya kwako. Yaani kama umepewa dhamana ya uongozi na unapata ‘vijisenti’ viwe vya taifa.”
Alisema kutokana na maoni waliyokusanya kutoka kwa wananchi na utafiti uliofanywa na Tume walibaini kuwa masuala hayo yakiwekwa katika sheria badala ya Katiba, sheria husika haitakuwa na nguvu.
“Ukiweka jambo hili katika Katiba kama walivyofanya Afrika Kusini na Namibia inasaidia. Maana yake ikijulikana kiongozi una Akaunti nje ya nchi, hakutakuwa na haja ya Takukuru kumchunguza mhusika,” alisema.
Alisema Mwalimu Nyerere alishauriwa kufungua akaunti nje ya nchi lakini alikataa na kuhoji iweje viongozi wa Tanzania sasa kubariki suala hilo la kuweka fedha nje ya nchi na kusaidia nchi nyingine.
“Unapoweka suala hilo katika sheria badala ya Katiba maana yake umeruhusu watu wafungue akaunti nje ya nchi na unawawekea utaratibu wa jinsi ya kufanya. Nchi ina matatizo ya rushwa, ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka lakini tunaogopa kuyatia katika Katiba kuonyesha dhamira ya kupambana nayo,” alisema.
Akizungumzia mgawanyo wa madaraka na jinsi mihimili ya Serikali na Bunge inavyoingiliana katika utendaji, Jaji Warioba alitoa mfano wa hivi karibuni jinsi Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilivyonyimwa na Serikali kupewa mikataba 26 ya gesi na kuchukua jukumu lisilo lake la kuwakamata watendaji wa Serikali.
“Haya mambo ndiyo yanatokea sasa. Katika rasimu ya Tume tulipendekeza Bunge kuridhia mikataba ya kimataifa na rasilimali za taifa kama mafuta, madini na ardhi. Jambo hilo limekataliwa na hivi karibuni limeibuka katika Kamati ya Bunge na kamati kuidhinisha watendaji wa Serikali wakamatwe,” alisema.
Akijibu swali la Abubakar, Jaji Warioba alisema, “Tunachofanya sasa ni kutaka kuwa na Katiba bora. Tuitazame Katiba Inayopendekezwa vizuri na tusiichukulie kama ni ilani ya uchaguzi. Tukifanya hivyo tutajuta baadaye.”
Aliwataka Watanzania kutodanganywa na kuhakikisha wanapiga kura kupitisha Katiba Inayopendekezwa kwa masilahi ya nchi.
“Wanasema nijiunge na Ukawa. Hapana, nitabaki kuwa Mtanzania. Rasimu iliyotolewa na Tume ilikuwa na upungufu. Watu walitoa maoni mengi hivyo ni lazima tuhakikishe yanafanyiwa kazi ili kuondoa matatizo yanayotukabili. Hata hili la escrow ni dalili ya matatizo tuliyonayo,” alisema.
Alisema sasa wabunge wanapeleka mamilioni majimboni lakini hakuna wa kuwahoji na akisisitiza kuwa bila maridhiano kati ya pande zinazovutana pamoja na Tanzania Bara na Zanzibar ni vigumu Katiba Inayopendekezwa kutekelezeka.
Katika hotuba yake, Jaji Warioba alieleza kushangazwa kwake na kauli za baadhi ya mawaziri na wabunge kukiri kwamba walimkejeli katika vikao vya Bunge Maalum la Katiba kama mbinu za kupata ushindi.
“Tusitumie matusi, kejeli, kubeza kama njia ya kupata ushindi. Siyo kitu kizuri kwa viongozi kutafuta ushindi kwa kutukana na kukejeli,” alisema.
Akiwajibu wanaodai kuwa yeye na wenzake (waliokuwa wajumbe wa Tume) kuwa wanamsaliti Mwalimu Nyerere, alisema hilo siyo kweli kwa sababu Mwalimu Nyerere angeweza kujitajirisha lakini alipoona dalili za ufisadi, alipitisha Azimio la Arusha akijua kuwa litaanzia kwake.
“Mwaka 1984 Mwalimu Nyerere alikazana kuweka ukomo wa urais wakati akiwa rais kwa sababu alijua utaanzia kwake. Siku hizi kuna marais wanataka kuendelea tu na wako tayari kubadili Katiba,” alisema.
Alisema wanaosema kuwa Mwalimu Nyerere alitaka Serikali mbili ndiyo wameondoa mambo ya Muungano yaliyowekwa na mwasisi huyo pamoja na mwenzake, Abeid Aman Karume.
Pia, Jaji Warioba aligusia tofauti kati ya Katiba Inayopoendekezwa na Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kugusia suala la maadili ya viongozi, madaraka ya rais, mgombea binafsi, tunu za taifa, mgawanyo wa madaraka, dira, haki mbalimbali, idadi ya wabunge, mgombea binafsi na Muungano.
Huku akishangiliwa, Jaji Warioba pia alisema kuwa suala la Katiba Inayopendekezwa, isitumike kama ajenda ya Uchaguzi Mkuu mwakani, zaidi ya kusisitiza wananchi kuisoma na kuielewa na kuitolea uamuzi.
Kwa upande wake, Polepole akizungumzia sakata la Escrow alisema kuwa hayo ni matokeo ya nchi kuwa na msingi wa katiba ambayo haijashonwa vizuri huku akiwataka viongozi kuwa na tabia ya kuwajibika yanapotokea makosa.
“Kuna makosa makubwa yakutisha yametokea lakini watu wanaendelea kufunga tai. Kujenga Tanzania ya kesho ni gharama, tukisema tuweke haya mambo kwenye sheria hawataweka ni bora yakawekwa kwenye katiba, “alisema.
Kuhusu kasoro zilizopo kwenye Katiba Inayopendekezwa, alisema ingawa baraza la vijana limetajwa, lakini ni kosa kudhani kuwa ajira za vijana zinaweza kuletwa na mabaraza.
Akizungumzia kuhusu muundo wa serikali tatu, Polepole alisema baadhi ya marais wastaafu na mawaziri wakuu wastaafu walitaka serikali tatu.
Pia, alizungumzia kile alichokitaja kuwa ni ‘kuchakachuliwa’ kwa haki za watu wenye ulemavu, wanawake, nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi kupitishwa na Bunge na mbunge kung’olewa na wapiga kura wake.
Pia, alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipendekeza kuundwa kwa Tume ya maboresho ya jeshi la polisi ili kuwawezesha kupata maslahi mazuri zaidi lakini Bunge Maalumu halikupitisha kifungu hicho.
Kwa upande wake Profesa Baregu alisema kilichotokea kwenye mchakato wa Katiba ni kuburuzwa na kushinikiza mambo huku baadhi ya wananchi wakibaguliwa.
Alisema katika hali ya kawaida hakutegemea kuona watu wakifanya sherehe ya kuipata Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa ilipatikana kwa namna ya mvutano.
“Nilishangaa kuona wabunge, marais wote wawili kwenda kusherehekea kushindwa kufikia malengo tuliyojiwekea.. Waliokuwa wanasheherekea walisema wengi wape, lakini siyo katika katiba, waliokuwa wengi watakuwa wachache wa kesho,” alisema Baregu.
Pia Baregu alisema kuwa muungano hauna mwenyewe kwa kuwa hakuna mtu yeyote kutoka Zanzibar au Bara anayeweza kusimama na kutetea masilahi ya muungano.
“Muungano hauna mwenyewe, ni yatima. Tulipendekeza ianzishwe mamlaka ya muungano, ni katiba iliyokuwa inaondoa uyatima. Uwezekano wa Muungano kuvunjika utakuwa karibu kuliko tulivyodhani,” alisema.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Hussein Issa na Goodluck Eliona
CREDIT: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment