Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Wednesday 5 November 2014

IPTL KAA LA MOTO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi

Sakata la madai ya kuchotwa zaidi ya Sh. bilioni 200 kutoka katika akaunti ya Escrow limechukua sura mpya, baada ya wabunge kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza suala hilo.


Akaunti ya Escrow ilifunguliwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuhifadhi fedha za Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Supply Tanzania Limited (IPTL) kutokana na mgogoro uliozuka baina wabia wa IPTL ambao walikuwa wanaliuzia umeme Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Kampuni hizo ni VIP na Pan African Power Limited (PAP).

Inadaiwa kuwa fedha hizo baadaye zilichotwa na PAP na kuzitumia kama sehemu ya malipo ya kuinunua IPTL mwishoni mwa mwaka 2010, hatua inayopingwa na wabunge kadhaa.

Wabunge hao wamefikia hatua hiyo jana bungeni baada ya kudai kuwa serikali inachelewa kukabidhi bungeni ripoti ya uchunguzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

LUKUVI
Tafrani hiyo iliibuka baada ya ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kuliambia Bunge kuwa suala hilo haliwezi kujadiliwa kwa sasa kwa kuwa  bado ripoti hizo mbili hazijakabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mzozo huo ulizuka mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali  na majibu jana, huku Wabunge kadhaa wakisimama na kuomba miongozo kwa Naibu Spika, Job Ndugai, kwa masuala mbalimbali kuhusiana na suala la fedha za Escrow.

KAFULILAMbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR- Mageuzi), alimwomba Naibu Spika kuiamuru serikali kuwasilisha ripoti hiyo ili ijadiliwe, akisema Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hosea, amekaririwa akisema tayari ameikabidhi ripoti hiyo kwa Waziri Mkuu.

“Mheshimiwa Naibu Spika, nasimama kwa mujibu wa kanuni namba 47 kuhusiana na taarifa ambayo imetolewa jana (juzi). Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Takukuru kwamba kazi ya uchunguzi wa tuhuma za ufisadi kwenye akaunti ya Escrow amekwishamaliza na kwamba ameshamkabidhi Waziri Mkuu, Pinda na kwa hiyo hana cha kujibu zaidi ya hapo?” alihoji.

“Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii iliibuka katika Bunge lililopita la Bajeti na Mheshimiwa Waziri Mkuu akaahidi kwamba uchunguzi ukikamilika italetwa ndani ya Bunge,” alisema na kuongeza:

“Kwa kuwa hadi sasa nchi inaumia kufuatia suala hili hasa baada ya nchi wahisani kukata misaada yote ya kibajeti…miradi ya maendeleo imekwama huko majimboni kwetu na serikali imekuwa ikisuasua, haitaki kuleta taarifa kumbe taarifa inayo.”

Aidha, alisema kutokana na unyeti wa jambo hilo linalogusa maisha ya watu milioni 44, analiomba Bunge lijadili suala hilo kwa sababu wabunge ndiyo wenye kazi ya kuisimamia serikali.

“Kwa kuwa serikali inaonyesha mizengwe katika jambo hili, naomba kutoa hoja kuwa Bunge ilijadili jambo hili ili tufikie mwisho na wachache waliohusika kwenye jambo hili waweze kuchukuliwa hatua na nchi ibaki salama na Watanzania waweze kuishi kama kawaida…naomba kutoa hoja,” alisema.

Maelezo hayo yalimfanya Lukuvi kusimama na kutoa maelezo ya serikali akisema ripoti zote mbili yaani ya CAG na ile ya Takukuru bado hazijakabidhiwa kwa Waziri Mkuu, ingawa alisema zipo katika hatua ya mwisho ya kukamilika.

“Mheshimiwa Naibu Spika, si kweli kwamba tayari ripoti hizo zimekabidhiwa kwa Waziri Mkuu. Taarifa nilinazo mimi ni kuwa CAG amemtaarifu Waziri Mkuu kwamba yupo katika hatua za mwisho za kukamilika kwa ripoti yake.

 “Hata hiyo, taarifa ya Takukuru bado haijakabidhiwa kwa Waziri Mkuu. Tunachosubiri ni kwa taarifa hizo kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu ili zote kwa pamoja ziletwe kwa Mheshimiwa Spika ili zijadiliwe. Kama alivyoahidi Waziri Mkuu mwenyewe wakati alipoviagiza vyombo hivi viwili vifanye uchunguzi ambapo kimsingi, Takukuru wanachunguza jinai na CAG anachunguza mahesabu,” alisema Lukuvi.

Aidha, Lukuvi alisema suala la kuchukuliwa kwa fedha kutoka akaunti ya Escrow si suala la dharura la kulifanya Bunge kuwa na uharaka wa kulijadili na hivyo kuwaomba Wabunge kusubiri hadi ripoti hizo zitakapokabidhiwa kwa Waziri Mkuu na baadaye kuwasilishwa bungeni.

MOSES MACHALIHata hivyo, kauli hiyo ya Lukuvi ilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wabunge wengine akiwamo Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), ambaye aliomba mwongozo na kusema: “Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kwa mujibu wa kanuni namba 68(1) kuhusu utaratibu.”

“Na nitaomba nijielekeze kwenye kanuni namba 64(1)(a) ambayo inasema kwamba mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli,” alisema na kuongeza:
“Mheshimiwa Naibu Spika, mzungumzaji aliyekaa chini (Lukuvi) amezungumza kwamba anaitazama hoja hii kana kwamba siyo jambo la dharura, leo hii nchi wahisani wamegoma kutoa fedha kwa sababu ya sakata hili la fedha za Escrow…wananchi hawana dawa, na hata ukija kwenye kamati za Bunge, tumeshuhudia Wabunge wakipata shida wakiwa Dar es Salaam kwa sababu hawakulipwa posho zao…leo Waziri anasimama anasema jambo hili siyo la dharura. Muhimbili pale watu wapo hoi dawa hakuna, deni la MSD (Bohari Kuu ya Dawa) ni kubwa, mtu mmoja anazungumza siyo ya dharura,” alisema Machali.

Alisema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni chombo ambacho kina dhamana ya kuishauri na kuisimamia Serikali na iwapo CAG amechelewa kuwasilisha taarifa yake  ni wakati wa Bunge hilo kuonyesha makali yake badala ya kuendelea ya kusubiri.

“Mheshimiwa Naibu Spika, huu ni wakati wa kuonyesha meno ya Bunge lako, Waziri Lukuvi anasema suala la kuchotwa kwa mabilioni haya ya fedha kuwa si suala la dharura wakati hapa leo tumeambiwa kuwa hospitali hazina dawa, watu wanakufa, wafadhili wamesitisha kutupa misaada kwa suala hili na miradi majimboni mwetu inakwama kwa kukosa fedha.”

“Huu ni wakati ya Bunge kuonyesha meno yake ni si kuendelea kukalia na kusubiri  blablaa za Serikali kama ambavyo zinatolewan na akina Mheshimiwa Lukuvi, haiwezekani Bunge hili liendelee kukubali kwamba mamlaka iliyokabidhiwa kwa mujibu wa Ibara ya 53, basi lisiwe na mamlaka ya kuiagiza serikali kufanya lolote lile…haya mamlaka yanaporwa,” alisema.

 “Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Bunge lako litumie mamlaka iliyopewa…sasa kama taarifa ya CAG imekamilika kwa nini wasituletee?” alihoji.Hata hivyo, kutokana na kauli ya Machali, Lukuvi alisimama na kusema kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka ya kuisema serikali na si vinginevyo.

 “Kwa hiyo ninaposimama hapa na kuisemea serikali halafu mheshimiwa mmoja anasema kuwa ni blaablaa, mie sielewi labda tunatofautiana katika kuelewa,” alisema.

PETER SERUKAMBAMbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM),  alisimama akitaka Naibu Spika kuruhusu kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge ili kuchunguza suala hilo kwa maelezo kwamba serikali inachelewa kuliwasilisha bungeni.

“Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lako inatakiwa lifike mahali lifanye maamuzi…mimi nakubali serikali bado inafanya uchunguzi, inawezekana serikali isimalize uchunguzi na Bunge hili likaisha, na Bunge lijalo wakasema hawajamaliza…wakati huo wanaendelea na uchunguzi wa Serikali, mimi nilitaka niliombe Bunge lako liunde tume teule kwa ajili ya kushughulikia jambo hili kama Bunge,” alisema Serukamba.

NAIBU SPIKAAkijibu hoja hizo, Ndugai alisema kwa vile Kamati ya Uongozi ya Bunge ilitarajiwa kukutana jana jioni, suala hilo litajadiliwa kwa kina ikiwamo hoja ya Serukamba ya kutaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge, lakini pia kuangalia namna nzuri ya  Bunge kutoa maelekezo kwa Serikali kuhusiana na suala hilo.

HOSEAH: MAJIBU ESCOW YANAKUJA Mkurugenzi Mkuu waTakukuru, Dk. Edward Hoseah, alisema jana kuwa  uchunguzi ya akaunti ya Escrow majibu yake yatatolewa hivi karibuni.

Akizungumza na NIPASHE jana jijini Mwanza, Dk. Hoseah alisema suala la uchunguzi wa akaunti hiyo unafanywa na taasisi yake baada ya kupewa miezi sita na Bunge.

“Tunaendelea na uchunguzi baada ya kupewa miezi sita kufanya hivyo na Bunge huku CAG akipewa miezi miwili, uchunguzi wetu unakamilika mwezi ujao, lakini tunaamini majibu yatawasilishwa mapema kabla ya muda huo,” alisema Dk. Hoseah.

Alisema bado hawajawasilisha taarifa ya uchunguzi serikalini kwani muda waliopewa bado haujafikia tamati, hivyo muda ukifika Watanzania watapata taarifa rasmi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment