Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 3 October 2014

RASIMU YAPITA, BADO ZAMU YA WANANCHI KURA YA MAONI!


Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakipongezana baada ya kupita wa Rasimu ya Katiba

Bunge Maalum la Katiba (BMK), jana lilimaliza uhai wake kwa kupitisha kwa mbinde Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kwa kupata theluthi mbili ya kura zote kutoka upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar.

Akitangaza matokeo ya kura zilizopigwa na kwa siku mbili na wajumbe wa BMK, Naibu Katibu wa Bunge Maalum, Dk. Thomas Kashilillah, alisema jumla ya wajumbe wote wa Bunge hilo kutoka Zanzibar walikuwa ni 219 na Tanzania Bara ilikuwa na wajumbe 411.



Alisema ili kukidhi matakwa ya kisheria ya kupatikana kwa theluthi mbili ya wajumbe wote, Zanzibar ilitakiwa kupata kura za ndiyo 146 na Tanzania Bara ilipaswa kupata kura za ndiyo 274.

Alisema hata hivyo, kwa upande wa Zanzibar ni wajumbe 154 ndiyo waliopiga kura na wajumbe 65 hawakupiga kura, huku waliopiga kwa upande wa  Tanzania Bara wakiwa ni 335 na ambao hawakupiga kura ni 76.

Dk. Kashilillah alianza kwa kutangaza matokeo ya kura za Zazibar, ambapo alisema kuwa katika siku ya kwanza wajumbe saba walipiga kura ya wazi ya hapana na mmoja kura ya siri ya hapana kwa sura zote kuanzia ya kwanza hadi ya kumi, pamoja na ibara zake, huku wajumbe 107 wakipiga kura ya wazi ya ndiyo na wengine 39 wakipiga kura ya siri ya ndiyo.

Katika siku ya pili, wajumbe sita kutoka Zanzibar walipiga kura ya wazi ya hapana, wajumbe 108 walipiga kura ya wazi ya ndiyo, 39 walipiga kura ya siri ya ndiyo  na hakuna aliyepiga kura ya siri ya hapana.

Alisema kuwa kwa matokeo hayo kila sura na Ibara ilikuwa imepata theluthi mbili ya kura zote za wajumbe kutoka Zanzibar na hivyo kukidhi matakwa ya kisheria.

SHANGWE, VIGEREGEREBaada ya kutangaza matokeo hayo, ukumbi mzima ulilipuka kwa shangwe, vifijo na vigelegele, huku wabunge wengi wakiinuka kutoka kwenye viti vyao na kujimwaga katikati ya ukumbi kushangilia, wakiimba na kucheza nyimbo na mitindo ya aina mbalimbali.

Hali hiyo ilisababisha shughuli za BMK kusimama kwa zaidi ya dakika 20 ambapo wajumbe walikuwa wakikumbatiana kwa maana ya kupongezana, kucheza na kuimba nyimbo mbalimbali hususan taarab.

Baada ya wajumbe hao kutulia, Mwenyekiti wa BMK, alimwita Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ili atoe hoja ya kupitisha Katiba inayopendekezwa.

Baada ya hoja kutolewa na Chenge, kabla ya kuwahoji wajumbe, Mwenyekiti alitoa nafasi ya kusema neno kwa baadhi ya wajumbe na nafasi ya kwanza akapewa Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid.

Rashid alisema kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, watanzania wamepata fursa ya kukaa pamoja kuandika katiba, hivyo akawaomba watanzania kutumia fursa hiyo kuipokea na kuikubali Rasimu ya Katiba ili kudumisha amani na utulivu wa taifa.

Alisema kuwa wapo baadhi ya watu waliosema kuwa katiba haitapatikana wakidhani kuwa wanamiliki kura za wazanzibar, lakini kwa ushindi uliopatikana umeonyesha kuwa kura za wazanzibar ni wale waliokuwa ndani ya Bunge.

“Wako watu walisema kuwa wao ni wazanzibari kuliko wazanzibari wengine, waliwataka wazanzibar hao wapate mafuta yao, lakini waliwatetea Kibanda Maiti, walitaka wazanzibari wapate mikopo wakope bila matatizo, lakini waliwatetea kibanda maiti, walitaka wazanzibar rais wetu atambuliwe katika Jamhuri ya Muungano kama ilivyokuwa kwenye hati ya Muungano lakini walifanya hayo Kibanda Maiti, lakini nawambia wazanzibar halisi wanaowatetea wapo ndani ya nyumba hii na wataendelea kuwatetea mpaka mwisho,” alisema Hamad Rashid.

Mjumbe mwingine aliyepewa nafasi ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano), Stephen Wassira, ambaye anawapongeza watu wote walifanikisha upatikanaji wa Katiba inayopendekeza, lakini pia anawapa pole wale ambao walikuwa hawalali wakitaka BMK livunjike kwa wameshindwa.

Aliwataka Watanzania sasa kushikamana na kushirikiana wakati wa kupiga kura za maoni ili kuhakikisha kuwa Katiba hiyo inapita na kuanza kutumika.

“Ujumbe wangu kwa Watanzania wote, kwamba tushikamane ili ushindi upatikane tutakapopitisha katiba hii katika kwakura ya maoni, wapo waliosema wao ndiyo wanaowasemea sana Watanzania, wamesema wao ndiyo wasemaji wakuu, lakini hawasemi walichaguliwa na nani kuwasemea, wamekataa kuja kuwasemea katika bunge hili wameenda kuwasemea mtaani, na hata baada ya kushindwa wamesema wataenda mtaani na mimi nawakaribisha mitaani, tutaonana huko maana huko ndiko tunakoishi,” alisema Wassira.

Alisema kuwa watahakikisha wananchi wanaelimishwa juu ya Rasimu hiyo, Ibara kwa Ibara na manufaa yake kwa maisha yao na kuwa anao uhakika kuwa baada ya wananchi kuelimishwa wataipigia kura ya ndiyo.

Mwenyekiti pia alitoa nafasi kwa wajumbe wengine kutoa michango yao ambapo wengi wao walikuwa wakitoa hotuba za kuipigia debe Rasimu hiyo ili ili iweze kukubaliwa na wananchi kupitia kura za maoni.

Waliopewa nafasi walikuwa ni Sheikh Thabit Jongo, Anna Abdallah, John Cheyo, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru, Paul Makonda na Jeska Msambatavangu.

Bunge hilo lilimaliza shughuli zake jana na Mwenyekiti ataikabishi rasimu hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamde Shein, Oktoba 8, mwaka huu.

SITTA ALIA NA WAANDISHIKatika hatua nyingine, Sitta amehamishia vita yake aliyoianzisha dhidi ya maaskofu kwa waandishi wa habari nchini kwa kuwakejeli kuwa wanalipwa kidogo hali inayosababisha waandike kwa kutumia tindikali badala ya wino.

Akihutubia bungeni jana, muda mfupi kabla ya kuvunja BMK., Sitta  aliwatuhumu waandishi wa habari kuwa wanalipwa hfedha kidogo, badala ya kutumia kalamu za kawaida kuandika habari wanaandika kwa kutumia kalamu zenye wino wa tindikali.

Wakati akishukuru watumishi mmoja mmoja na makundi mengine ya watu walioshiriki kuwezesha BMK kukamilisha shughuli zake, anayoamini kuwa yalichangia bunge hilo kufanikisha kazi ya kuboresha Rasimu ya Pili na kuandika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, baadhi ya Wabunge walipaza sauti zao wakitaja waandishi wa habari bila shaka wakidhani alikuwa amelisahau.

“Nawashukuru sana wanaotuhudumia kwenye kantini zetu, walinzi, sasa baada ya maelezo hayo kwakuwa leo ni siku ya mwisho,  tusimame tuimbe wimbo, eeh nimekumbushwa hapa kuna ndugu zangu madereva ambao wengine wamekuwa wakisubiri mpaka saa 8:00za usiku,” Sitta alieleza.

“Waandishi wetu nadhani, kama tukiendelea hivi watu wakilipwa pesa kidogo badala ya kutumia wino, wanatumia tindikali kuandika na kutuletea chuki, lakini TBC naipa dole ipo juu kabisa na Zanzibar televisheni wanafanya kazi nzuri sana, nawapongeza,” alieleza mwenyikiti huyo.

Imeandaliwa na Emmanuel Lengwa, John Ngunge na Editha Majura, Dodoma
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment