Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Thursday 17 July 2014

RIWAYA TAMU: JUDITH…JUDITH…! - 20


INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)

0755 040 520 / 0653 593 546 

ILIPOISHIA:
Judith amefanikiwa kubadilisha fedha na kurejea Magomeni ambapo anaamua kupata supu. Mara anatokea Edson, kijana mtanashati na mwenye haiba ya kutosha ambaye anaomba kuketi mezani. Wote wawili nyoyo zinasabahiana na Edson anafarijika zaidi anapoambiwa na Judith kwamba hajaolewa. Huko Kigali, Rwanda Makella amechanganyikiwa baada ya kukimbiwa na Judith. Anaamua kwenda kwa Jamilla mke wa Ramadhani, mwanajeshi mwenzake, na anapofika anamkumbatia kwa nguvu mwanamke huyo ambaye anajitahidi kujinasua bila mafanikio. Ramadhani anaposikia purukushani hizo na kumuona Makella anaamua kutoka amua na bastola. Je, nini kitaendelea? Ungana na msimulizi wako …


Makella akashtuka na kumwachia Jamillah. Akageuka na kukutana uso kwa uso na Ramdhani aliyekuwa amemlenga kwa bastola. Makella akaduwaa. Akatamani kutamka neno asiweze.
Akayashuhudia macho ya Ramadhani yakimtazama bila ya kupepesa na yakitangaza jambo moja tu; NITAKUUA.
Mara akahisi kitu kikipenya kifuani, kikamzulia joto kali kisha maumivu yakaanza kumwingia kwa mbali. Nguvu zikaanza kumomonyoka maungoni, Uwezo wa macho kuona ukawa ukimkimbia kwa kasi ya kutisha. Miguu ikashindwa kuubeba mwili. Akamwona Makella akigeuka na kurudi chumbani na bastola yake.
Cha mwisho alichoambulia ni yowe kali la Jamillah na alipoanguka sakafuni hata maumivu hakuyasikia!

**********

MSHTUKO alioupata Judith pindi alipokutanisha macho na Edson haukuwa wa kawaida. Na alikumbuka mara ya mwisho alipoupata mshtuko wa aina hiyo ni siku alipokumbana  na Zalidi, kijana  ambaye alitokea kumvutia kwa kiasi kikubwa. Zalidi naye alikuwa Mtutsi na waliishi wote mjini Kigali, Rwanda lakini wakiwa mbalimbali kwa makazi.
Zalidi aliporusha ndoano, Judith alikosa uwezo wa kuikwepa. Akanaswa. Wakawa wapenzi. Lakini kabla hawajafikia ile hatua ambayo Zalidi aliihitaji sana, hatua ya kustarehe kimwili, mauaji yalitokea mtaani alikoishi Zalidi. Wazazi wake Zalidi pamoja na Zalidi mwenyewe, waliuawa kikatili na askari wa Kihutu.
Tangu hapo Judith hakujua kupenda wala kutamani hadi siku hii alipopata tena mshtuko huu, mshtuko ulioifanya akili yake ivurugike kiasi cha kujikuta akiwa mwepesi wa kujibu kuwa hajaolewa. Na ndipo maongezi kati yao yaliponoga, Edson akiwa kinara.
Waliachana baada ya saa tatu, maongezi baina yao yakiwa yamewaweka karibu zaidi.
Sasa Judith alijikuta akifungua ukurasa mpya. Akatamani kila wakati awe na Edson. Hata aliporudi kule gesti, mawazo yake yote yalikuwa kwa Edson. Alikuwa na hamu wawe pamoja, wakumbatiane na hatimaye kufanya kila kitu ambacho mioyo yao ingewashawishi. Kwa ujumla alimpenda na kumhitaji Edson kwa kiwango kikubwa.  Ndipo akajiwa na wazo la kumtoroka Baraki, mfadhili wake tangu Rwanda.
Alitambua fika kuwa, haitakuwa busara kumtoroka Baraki, lakini afanye nini? Huyo Baraki mwenyewe ana mke. Vipi amtegemee mtu wa aina hiyo katika maisha yake? Na pia, kiwango cha pesa alizokuwa nazo kilikuwa kichocheo kingine katika kumfanya amtoroke Baraki.
Si tu kwamba kwa kuwa amekutana na Edson na kuvutiwa naye ndiyo maana akaamua kumkimbia Baraki. La hasha. Alijua kuwa mapenzi ya Baraki hayatadumu, ni mapenzi ya muda tu, mapenzi ambayo siku yatakapoyeyuka  ndipo atakapojikuta katika dunia mpya, katika maisha mapya.
Hivyo, hakutaka kupoteza muda. Jambo la kwanza aliloamua kulifanya ni kuondoka katika gesti hiyo. Ndiyo, aondoke na kwenda kuishi popote. Kama ni suala la pesa, hilo halikuwa tatizo. Pesa anazo, tena za kuweza kumlinda kwa siku nyingi. Ni kipi kitakachoharibika? Hakuna.
Alipofika gesti tu, alitwaa kila kilicho chake na kuondoka huku akimwambia yule mhudumu kuwa Baraki amemwagiza wakutane mtaa wa pili kwenye baa moja anakopata bia.
“Ndiyo uondoke na mizigo?” mhudumu alimhoji kwa mshangao.
“Ameniagiza kuwa niende nayo,” Judith alijibu kisha akaongeza, “Kwani kuna tatizo gani? Anadaiwa?”
“Hapana, nauliza tu shemeji yangu.”
Ni hapo mtoto wa kike, msichana mrembo, msichana wa Kitutsi, Judith Ndayishimiye alipotokomea kisayansi. Usiku wa siku hiyo ukawa ni yeye na Edson, Edson na yeye. Siku mbili baadaye walikutana tena, hatimaye ikawa haipiti siku bila ya kuonana. Uhusiano wao ukazaa uchumba kamili. Na ni katika muungano huo ndipo Judith alipoamua kumtobolea ukweli kuhusu historia ya maisha yake.
Ilikuwa ni hadithi iliyomsononesha sana Edson. Na akaahidi kuitunza siri hiyo.
“Usihofu, Judith,” alimwambia. “Lakini nakuahidi kuwa hutapata shida yoyote. Cha muhimu, ni wewe kujitahidi kutomropokea mtu yeyote kuhusu mkasa huo. Pole sana, mpenzi. Hayo ni mapito tu. Huenda Mungu alipanga wewe usiuawe na uje kuishi huku Tanzania. Uje kumwondolea upweke Edson.”
Mwaka mmoja baadaye, ndoa kati ya Judith na Edson ilifanyika. Sherehe kubwa ikafuata. Watu wakala, watu wakanywa na kusaza.

**********

SIKU moja, ikiwa ni miaka mitatu baada ya Edson na Judith kufunga ndoa, Judith alikuwa eneo la Kariakoo na mwanaye, Jerome ambaye wakati huo alikuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu. Alikwenda huko kutafuta nguo zake na za mwanaye kwa ajili ya sikukuu ya Krismasi. Alipita mtaa huu na ule, akiingia duka hili na lile, akiangalia nguo hii na ile.
Hatimaye, katika pitapita yake hiyo, aliingia katika duka moja Mtaa wa Kongo. Duka hilo lilisheheni watu. Humo alitulia akiangalia kwa makini nguo nyingi zilizokuwa katika mauzo. Kulikuwa na wahudumu wawili ambao waliwasikiliza wateja huku mmiliki wa duka, mzee wa Kihindi akiwa ameketi kitini, meza iliyosheheni makabrasha ikiwa mbele yake.
Judith alijisogezasogeza hadi mbele na kumgusa mhudumu mmoja huku akimwambia, “Kaka, nipatie ile blauzi nyekundu.”

No comments:

Post a Comment