Mwandishi wa brotherdanny5.blogspot, Arusha
WAFADHILI kutoka Ubeligiji wamekabidhi mradi wa umeme wa jua wenye gharama ya shilingi milioni 55 kwa shule ya sekondari ya wazazi Leguruki lengo likiwa ni kuwawezesha wanafunzi waweze kusoma nyakati za usiku .
Pia wafadhili hao wameweza kutoa kompyuta sita shuleni hapo ili kuwawezesha walimu nao waweze kuendesha shuguli zao za kiofisi kwa haraka zaidi tofauti na hapo awali.
Shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na umeme wa kuaminika kwa kipindi cha muda mrefu hali iliyokuwa inapekea kuwanyima watoto shuleni hapo kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao kutokana na kutokuwepo kwa umeme wa kuaminika.
Akikabidhi mradi huo shuleni hapo mkurugenzi wa kampuni ya Energy Assistance kutoka Ubeligiji Frederic Madry alisema kuwa walipata wazo la kusaidia shule hiyo mara baada ya kutembelea na kubaini kuwa shule hiyo inakabiliwa na tatizo la umeme .
Alisema kuwa kupatikana kwa mradi huo ambao ni wa kisasa zaidi kunatokana na muungano wa watu wengi kutoka ubeligiji pamoja na mkuu wa shule hiyo ambapo alikuwa nao bega kwa bega kuhakikisha kuwa unakamilika kwa haraka.
Naye mkuu wa shule hiyo Emanuel Loy akizungumza mara baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo aliwashukuru wafadhili hao na kusema kuwa mradi huo utakuwa chachu kubwa ya kuongeza kiwango kizuri cha ufaulu shuleni hapo.
“Mradi huu wa umeme wa jua tuliokabidhiwa utasaidia sana hii shule maana madarasa pamoja na mabweni yalikuwa hayana umeme jambo ambalo lilikuwa likiwanyima hata watoto wetu kusoma nyakati za usiku kutokana na kutokuwepo kwa umeme wa uhakika,” alisema Loy.
Aliongeza kuwa kupitia umeme huo utawasaidia kujifunza kompyuta walizopewa ,kuweza kuendeshea hata ofisi pamoja na kuwafanya wanafunzi wasome usiku tofauti na hapo awali.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wilaya ya meru Jeremia Kaaya aliwataka walimu wa shule hiyo kuulinda na kutunza mradi huo wa umeme ili uweze kutumika kwa vizazi vya sasa na hata baadae.
No comments:
Post a Comment