TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Kikwete akusudia kushika chaki tena
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa
anakusudia kurejea darasani kushika tena chaki kwa kuwa mhadhiri kwenye
Chuo cha Taifa cha Ulinzi – National Defence College (NDC) cha Dar Es Salaam.
Rais Kikwete amelieleza hilo mchana wa leo, Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the Nation) mbele ya wanafunzi wa Chuo hicho kilichoko Kunduchi, Dar Es salaam.
Rais Kikwete amewaambia wanafunzi wa kozi ya pili ya Chuo hicho kutoka nchini na nchi za jirani za Uganda, Kenya na Rwanda: “Najisikia
mwenye raha sana kuweza kurudi darasani kutoa mhadhara huu. Tukio hili
linanikumbusha enzi zangu katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli (TMA). Ni
matarajio yangu pia kuwa nitaweza kurudi kuwa mhadhiri katika Chuo hiki
baada ya kukamilisha kazi yangu ya sasa.”
Rais
Kikwete ambaye alizungumza kwa kiasi cha saa mbili, alianza mhadhara
wake baada ya kupata maelezo kuhusu maendeleo ya Chuo hicho na baadaye
akajibu maswali ya wanafunzi ambao walimwuuliza kuhusu mambo mbali mbali
yanayohusiana na usalama wa nchi.
NDC
kilianzishwa rasmi Septemba 2, mwaka 2012 na Chuo hicho kilizinduliwa
Rais na Rais Kikwete Septemba 10, mwaka huo huo, 2012 wakati
alipotembelea Chuo hicho kwa mara ya kwanza kufuatia juhudi kubwa za
uongozi wake kuhakikisha kuwa chuo cha namna hiyo na cha aina yake
kinaanzishwa nchini. Rais pia alifungua kozi ya kwanza ya Chuo hicho.
Kundi
la wanafunzi wa kwanza kwenye Chuo hicho lilimaliza mafunzo yake Julai
23, mwaka 2013 na sasa chuo hicho kinaendesha kozi ya pili yenye
wanafunzi 30. Chuo hicho tayari kimepata usajili kamili wa NECTA ambako
kina uwezo wa kutoa shahada ya uzamili katika masomo ya Strategic Studies.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
20 Juni, 2014


No comments:
Post a Comment