Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
Dodoma. Macho na masikio ya wananchi leo
yatahamia bungeni mjini Dodoma wakati Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
atakapokuwa akisoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa
2014/15.
Mwelekeo wa Bajeti hiyo umekuwa na usiri mkubwa
kutokana na Serikali kutokuwa wazi kuieleza Kamati ya Bunge ya Bajeti,
vyanzo vyake vipya vya mapato licha ya kukutana mfululizo tangu Juni 5,
mwaka huu.
Licha ya wabunge kutaka kufahamu Serikali
itazipataje Sh19 trilioni kugharimia Bajeti ya 2014/15, wakati
imeshindwa kutimiza malengo ya kukusanya Sh18.2 trilioni kwa mwaka huu
wa fedha unaomalizika Juni 30 mwaka huu, vyanzo hivyo vimekuwa siri
kubwa. Bajeti ya mwaka huu wa fedha ina upungufu wa Sh1.8 trilioni.
Hata hivyo, habari kutoka katika kikao hicho
zinaeleza kuwa usiri huo unatokana na Serikali kutokuwa na vyanzo vya
uhakika vya mapato, jambo ambalo limewafanya kutotaka kuliweka wazi.
“Hakutakuwa na jipya katika upande wa vyanzo vipya
vya mapato, tutarajie vyanzo vilevile vya Bajeti ya mwaka 2013/14
ambavyo vilitokana na kuongeza kodi katika vinywaji baridi; soda, bia na
maji, pia katika sigara,” kilisema chanzo hicho.
Kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato
kumekwamisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika wizara zote
kwani Bajeti ya mwaka 2013/14 imetekelezwa kati ya asilimia 25 hadi
35.Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema hivi karibuni kuwa
wizara yake inakusudia kupitia upya bajeti za wizara zote ili kuhamisha
fedha kutoka katika matumizi yasiyo ya lazima ili zielekezwe katika
mahitaji muhimu.
Katika kuthibitisha hilo, Kamati ya Bajeti na
Serikali zilikubaliana kukata asilimia 7.5 ya fedha katika baadhi ya
mafungu ya matumizi mengineyo (OC) kutoka katika wizara zote ili
kuwezesha kupatikana kwa Sh230 bilioni ambazo zinahitajika kwa ajili ya
maendeleo, hasa katika sekta tatu; afya, miundombinu na kilimo.
“Tunajibana ili fedha zipelekwe katika maji,
elimu, miundombinu na afya. Zitakazobaki zitapelekwa katika maeneo
mengine,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na
Uwezeshaji), Dk Mary Nagu.
Katika Bajeti ya mwaka 2014/15, huenda Serikali
ikaja na tozo mpya ili kupata fedha za kuanzisha mfuko wa maji kutokana
na kelele zilizopigwa na wabunge, kwa maelezo kuwa ni idadi ndogo ya
Watanzania wanaopata maji salama.
Jambo jingine linalosubiriwa kwa hamu ni ahadi ya
Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi
Duniani (Mei Mosi), ya kupandisha mishahara ya wafanyakazi.
Pia Rais aligusia kupunguzwa kwa Kodi ya Mapato ya
Wafanyakazi (Paye) na kuahidi kuipunguza kutoka asilimia 13 ya sasa na
kufikia tarakimu moja.
Wafanyabiashara wakubwa nao wanaisubiri Bajeti
hiyo kujua kama watapata unafuu wa kodi ya mapato, huku wafanyabiashara
wadogo wakitaraji kuondolewa kodi.
Bajeti 2013/14
Wahisani kutoa Sh904 bilioni
Hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge kuhusu
vyanzo vipya vya mapato nayo inasubiriwa na wananchi kujua kile
kilichokuwa kikizua mjadala kati yake na Serikali.
Bajeti 2013/14
Katika Bajeti ya 2013/14, Serikali iliongeza
kiwango cha ushuru wa mafuta kutoka Sh200 kwa lita hadi Sh263 kwa lita
sawa na ongezeko la Sh63 kwa lita.
Pia ilipandisha kodi katika vinywaji baridi kutoka
Sh83 kwa lita hadi Sh91; ongezeko la Sh8 kwa lita. Pia ilianzisha tozo
ya mafuta ya petroli ya Sh50 kwa lita ambayo inakusanywa na Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya Mfuko wa Nishati Vijijini (Rea).
Mafuta ya dizeli yalipanda kutoka kiwango cha sasa
cha Sh215 kwa lita hadi Sh217 kwa lita ikiwa ni ongezeko la Sh2,
petroli ilipanda kutoka kiwango cha Sh339 kwa lita hadi Sh400. Maji ya
matunda yaliyotengenezwa kwa matunda yanayozalishwa nchini yalipanda
kutoka Sh8 kwa lita hadi Sh9 sawa na ongezeko la shilingi moja; huku
juisi iliyotengenezwa kwa matunda yasiyozalishwa nchini ikipanda kutoka
Sh100 hadi Sh110 kwa lita.
Bia inayotengenezwa kwa nafaka ya nchini na ambayo
haijaoteshwa, ilipanda kutoka Sh310 hadi Sh341 kwa lita, sawa na
ongezeko la Sh31, huku bia nyingine zote zikipanda kutoka Sh525 hadi
Sh578 kwa lita.
Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu za ndani ya nchi
kwa kiwango kinachozidi asilimia 75, ulipanda kutoka Sh145 hadi Sh160
kwa lita.
Vinywaji vikali, vilipanda kutoka Sh2,392 hadi Sh2,631 kwa lita.
Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa
kutokana na tumbaku ya nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75,
zilipanda kutoka Sh8,210 hadi Sh9,031 kwa sigara 1,000; sawa na ongezeko
la senti 82 kwa sigara.
Zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na
tumbaku inayozalishwa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75 kutoka
Sh19,410 hadi Sh21,351 kwa sigara 1,000; likiwa ni ongezeko la Sh moja
na senti 94 kwa sigara.
Sigara nyingine zenye sifa tofauti na zilizotajwa
juu zilipanda kutoka Sh35,117 hadi Sh38,628 kwa sigara 1,000; ikiwa ni
ongezeko la Sh tatu na senti 50 tu kwa sigara moja.
Wahisani kutoa Sh904 bilioni
Katika Bajeti hiyo, nchi wahisani zimeahidi kutoa Sh904 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wake.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na wahisani hao
walipokutana na Kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Bajeti na
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), katika ukumbi wa bunge wa Pius
Msekwa.
Mwenyekiti wa LAAC, Rajabu Mbarouk Mohamed alisema
katika kikao cha wahisani hao kutoka nchi sita na Benki ya Dunia (WB),
waliahidi kutoa fedha hizo.
“Kila mwaka tuna utaratibu wa kukutana na nchi
wahisani ili kujua utekelezaji wa bajeti na kama tumefikia kwa kiwango
gani katika utekelezaji,” alisema Rajabu.
Alisema katika mazungumzo hayo wafadhili hao
walisema kwa miaka 10 mfululizo wamekuwa wakitoa fedha zote wanazoahidi
kusaidia katika bajeti.
“Tuliwahoji kuhusiana na utekelezaji wa ahadi zao,
wakatuambia kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo wamekuwa wakitoa
asilimia 100 ya kile wanachoahidi,” alisema.
CREDIT: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Kitendawili-cha-Bajeti-kuteguliwa-leo/-/1597296/2345250/-/item/2/-/hu37tcz/-/index.html
CREDIT: http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Kitendawili-cha-Bajeti-kuteguliwa-leo/-/1597296/2345250/-/item/2/-/hu37tcz/-/index.html

No comments:
Post a Comment