Uwanja wa Corinthians jijini Sao Paulo ambapo leo fainali za Kombe la Dunia zinafunguliwa rasmi kwa mchezo baina ya wenyeji Brazil na Croatia.
Na James Truman, brotherdanny5.blogspot
Sao Paulo, Brazil: FAINALI za Kombe la
Dunia zinaanza rasmi leo nchini Brazil ambapo wenyeji wanafungua dimba na
Croatia kwenye Uwanja wa Corinthians unaomeza mashabiki 65,000 mara moja.
Wachunguzi wa masuala
ya soka wanasema fainali za mwaka huu zitakazovutia mashabiki zaidi ya milioni
tatu ndizo zilizoweka rekodi ya pekee kuanzia maandalizi yake hadi mapato.
Rekodi hizo ni pamoja
na zawadi ya Dola 35 milioni (takriban Shs. 57.8 biloni) kwa shirikisho ambalo
timu yake itatwaa ubingwa, Dola 4 bilioni (Shs. 6.6 trilioni) zitakazotokana na
matangazo ya biashara kwa FIFA, na Dola 14 bilioni (Shs. 23.1 trilioni) kama
mapato kwa Brazil, yaani nchi mwandaaji.
Kwa ujumla, fainali
hizi ni tayari zimekwishauzwa, kwa saabu tiketi zote milioni 3 zilizotengwa na
FIFA kwa ajili ya mechi 64 zinaonekana zimekwisha tangu zilipoanza kuuzwa
Oktoba 2013.
"Tumepata
mafanikio ya kiuchumi,” Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke aliwahi kukaririwa akisema.
“Kuna mafanikio makubwa sana katika mauzo ya tiketi, hatujawahi kuuza tiketi
nyingi namna hii."
Lakini furaha ya FIFA
iko tofauti na hali halisi nchini Brazil.
Walipa kodi ndio
wanaokamuliwa zaidi, katika taifa lenye watu milioni 200 ambao gharama za vitu
zimepanda zaidi ya maradufu kutokana na uenyeji wa fainali za mchezo huo wenye
waumini wengi duniani.
Kiasi cha Dola 14
bilioni ni jumla ya fedha ambazo zimetumiwa na Brazil katika ujenzi na
ukarabati waviwanja 12 vitakavyotumika kwa mashindano hayo, kuboresha miundombinu
ya jiji na maeneo mengine ya kiserikali pamoja na kuhakikisha usalama wa timu
zote 32 na watazamaji 600,000 watakaokwenda huko, ambao tayari wengi
wamekwishawasili.
Matumizi hayo makubwa
yamesababisha vurugu nchini Brazil, na ilianza kujionyesha Juni 2013 wakati wa
Kombe la Mabara ambapo wananchi walilalamika kwamba hawana shule bora,
hospitali zinazofaa huku serikali nayo ikituhumiwa kwa rushwa.
"Wakati Brazil
ilipoomba uenyeji wa Kombe la Dunia ilikuwa na bajeti ya kufanya hayo," alisema
Valcke.
Katika fainali hizi FIFA
itatumia Dola 2 bilioni (Shs. 3.3 trilioni), ikiwa ni pamoja na gharama za
kamati ya maandalizi.
Lakini hayo yote
yataipita Brazil. Hata kama nchi hiyo mwenyeji itapata hundi ya ubingwa Julai
13, fedha zitakazosalia Dola 323 milioni katika fungu la zawadi la FIFA
zitakwenda kwa mataifa mengine 31 yanayoshiriki.
Shirikisho la Soka la
Brazil pia linapata fungu kutoka kwenye Dola 48 milioni za FIFA kwa maandalizi,
na Dola 70 milioni zinakwenda kwenye klabu (karibu zote za Ulaya) za Ulaya ambazo
wachezaji wake wanawakilisha nchi zao.
Zawadi ya Dola 35
milioni (Shs. 57.8 bilioni) kwa bingwa wa dunia ni chini ya asilimia moja ya
mapato ya FIFA iliyoyapata katika kipindi cha miaka minne ya fainali hizi.
Watangazaji na
wadhamini wanalipa sehemu kubwa ya Dola 4 bilioni ambazo FIFA inatakiwa kupata.
Mtandao wa
televisheni wa Ulaya umelipa sehemu kubwa ya fedha hizo karibu Dola 1.7 bilioni
ili kupata haki ya kutangaza fainali hizo.
Wadhamini sita wakuu —
Adidas, Coca-Cola, Emirates, Hyundai, Sony, Visa — kwa pamoja wanalipa Dola 177.125
milioni kila mwaka. Hiyo ni karibu Dola 708.5 milioni kwa miaka minne.
Wadhamini nane
wanaofuatia — Budweiser, Castrol, Continental, Johnson & Johnson,
McDonald's, Moy Park, Oi, Yingli — kwa pamoja wanalipa Dola 524 milioni. Karibu
Dola 120 milioni zimevunwa kutoka kwa watangazaji wa ndani wa Brazil, kwa
mujibu wa ripoti za mapato za FIFA za mwaka 2011-13.
FIFA pia inapata
mamia ya mailioni kutoka kwa mashabiki wanaonunua tiketi kwa ajili ya kuingia
viwanjani, ikiwa ni pamoja na taasisi zinazonunua viti maalum vya hisani na
bidhaa zinazouzwa humo.
Matangazo kadhaa
nchini Brazil yanaonyesha kwamba mapato ya FIFA hayatozwi kodi hapa. Wadhamini wa
Kombe la Dunia na vyombo vya habari navyo vimesamehewa kodi.
FIFA, hata hivyo,
imewekeza sana Brazil. Iliipatia kamati ya maandalizi Dola 221.6 milioni, na Februari
mwaka huu FIFA ililipia karibu Dola 20 milioni kwa ajili ya umeme wa majenereta
kwa shughuli za matangazo.
Uwekezaji wa FIFA
unahusisha makumi ya mamilioni kwa vituo vya TV.
Mwaka 2010 kule
Afrika Kusini, mchezo wa fainali baina ya Hispania na Uholanzi ulitazamwa na
watu 530.9 ulimwenguni kote. Zaidi ya watu milioni 900 wala walitazama dakika
moja ya mchezo huo nyumbani, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, na kwa ujumla
upo uwekezano wa watu bilioni moja kutazama walau sehemu ya mchezo huo.
FIFA inatumia fedha
nyingi katika soka, ambapo Dola 1.4 bilioni ni kwa ajili ya kulifanya
shirikisho hilo liendeshe shughuli zake pale Zurich na kuandaa mashindano
mbalimbali – yakiwemo Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake, mashindano ya
dunia ya vijana chini ya miaka 17 na 20, Olimpiki ya Kiangazi, na Kombe la
Dunia la Klabu.
Asilimia 75 ya mapato
ya FIFA yanazama kwenye soka, ikiwemo mgawo wa Dola 250,000 kila mwaka kwa nchi
209 wanachama wake. Mashirikisho sita ya mabara yanapata Dola 2.5 milioni kila
moja, na Dola 25 milioni zilitumika mwaka 2013 kwa shughuli za maendeleo,
ikiwemo ujenzi wa viwanja.
Gharama za maandalizi
Rekodi
zinaonyesha kwamba, fainali za mwaka huu ndizo zilizogharimu fedha nyingi zaidi
kuliko zilizopita.
Brazil,
kama ilivyoelezwa hapo juu, imetumia Dola 14 bilioni kwa mwaandalizi ya mwaka
huu, wakati ambapo katika fainali za 2010, Afrika Kusini ilitumia Dola 4
bilioni; fainali za 2006 Ujerumani ilitumia Dola 6 bilioni; fainali za 2002
Korea Kusini na Japan kwa pamoja zilitumia Dla 5 bilioni; fainali za 1998
Ufaransa ilitumia Dola 340 milioni; na fainali za 1994 Marekani ilitumia Dola
30 milioni, pengine kwa sababu viwanja vyake vingi vilikuwa na hadhi kubwa.
Zawadi
Jumla
ya zawadi zitakazotolewa na FIFA kwenye mashindano hayo ni Dola 576 milioni
(ikiwemo Dola 70 milioni kwa klabu zenye wachezaji wanaoshiriki), likiwa ni
ongezeko la asilimia 37 kulinganisha na zilizotengwa kwenye fainali ya mwaka
2010.
Kabla
ya mashindano, kila timu shiriki kati ya 32 ilipatiwa Dola 1.5 milioni (Shs.
2.5 bilioni) kwa ajili ya gharama za maandalizi.
Mchanganuo
unaonyesha kwamba, kila timu itakayotolewa katika hatua ya makundi itakomba
Dola 8 milioni (Shs. 13.2 bilioni) wakati timu itakayoishia hatua ya mtoano
itapata Dola 9 milioni (Shs. 14.9 bilioni) huku ile itakayoishia robo fainali
ikilamba Dola 14 milioni (23.1 bilioni).
Aidha,
timu itakayoshika nafasi ya nne itapata Dola 20 milioni (Shs. 31.2 bilioni),
mshindi wa tatu atapata Dola 22 milioni (Shs. 36.3 bilioni), mshindi wa pili
Dola 25 milioni (Shs. 41.3 bilioni), na bingwa atanyakua Dola 35 milioni (Shs.
57.8 biloni).
Ni
utajiri mtupu.
Endelea
kufuatilia blog hii kwa habari mbalimbali…

No comments:
Post a Comment