Twitter Buzz

....

....

...

...

IMETOSHA!

IMETOSHA!

Featured post

KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

Makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandes De la Vega alishindwa kujizuia na kwenda kumtuza mtoto Gozbert ...

Friday 6 June 2014

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2014/15


HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA, MHESHIMIWA SAADA MKUYA SALUM (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA KWA MWAKA 2014/15

UTANGULIZI

1.       Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/15.

2.       Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya mwaka 2014/15. Aidha, natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Ninaahidi kwamba nitatekeleza jukumu hili kwa weledi na uadilifu. Vile vile, nawapongeza Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Mhe. Adam Kighoma Ali Malima (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha. Kadhalika, namshukuru pia aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janeth Zebedayo Mbene (Mb) kwa utendaji kazi wake mahiri na tunamuombea Mwenyezi Mungu ampe nguvu na afya njema katika kazi zake mpya Wizara ya Viwanda na Biashara. Nichukue pia fursa hii kumpongeza Bw. Rished M. Bade kwa kuteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

3.       Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe mwenyewe, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuongoza vyema majadiliano ya Bunge la Bajeti.

4.       Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mbunge wa Kisesa) na Makamu wake Mhe. Dunstan Luka Kitandula (Mbunge wa Mkinga) kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Mhe. Andrew John Chenge (Mbunge wa Bariadi Magharibi) pamoja na Kamati nzima kwa ushauri wao. Katika uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara kwa mwaka 2013/14.

5.       Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, Wizara ilipata pigo kwa kuondokewa na kiongozi wetu mkuu Marehemu Dkt. William Augustao Mgimwa. Tunawashukuru Viongozi wa Serikali, Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa Maendeleo, Taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kwa ushirikiano waliotupa kipindi chote cha msiba. Tumeendelea kuenzi misingi imara aliyotujengea marehemu katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Aidha, tunapenda kutoa pole kwa ndugu na jamaa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Chalinze Marehemu Saidi Ramadhani Bwanamdogo. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

6.       Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza, Mhe. Yusuf Salim Hussein Mbunge wa Chambani, Mhe. Godfrey William Mgimwa (Mbunge wa Kalenga) na Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mbunge wa Chalinze) kwa kuchaguliwa kwao.


7.       Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mhe. Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mpanda Mashariki kwa hotuba yake nzuri ambayo imetoa mwelekeo wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2014/15.

8.       Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu nitaanza kuelezea mapitio ya utekelezaji wa mipango ya Wizara katika mwaka 2013/14. Nitaelezea pia mikakati mbalimbali ambayo Wizara imeweka kwa mwaka 2014/15 ili kuendelea kuboresha utekelezaji wa majukumu yake ya msingi yakiwemo: usimamizi wa Bajeti ya Serikali; ukusanyaji mapato ya Serikali; usimamizi wa misaada na mikopo; ulipaji wa Deni la Taifa; usimamizi wa matumizi ya fedha za umma; usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa umma; usimamizi wa utekelezaji wa MKUKUTA; na usimamizi wa mashirika na taasisi za umma.

 

9. Mheshimiwa Spika, mwisho nitawasilisha bajeti ya mwaka 2014/15 kwa mafungu saba ya wizara ya fedha ambayo ni fungu 7, 10, 13, 21, 22, 23 na fungu 50 pamoja na fungu 45 la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
  
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2013/14 NA MALENGO YA MWAKA 2014/15

10.    Mheshimiwa Spika, uandaaji, utekelezaji na usimamizi wa Mpango na Bajeti ya Wizara umezingatia malengo ya Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2012/13 - 2016/17 ambao utaiwezesha Wizara kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025; Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano 2011/12 - 2015/16; Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA) pamoja na Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma – PFMRP. Aidha, Mpango na Bajeti ulizingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 pamoja na Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa (Big Results Now – BRN).

11.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara ilipanga kutekeleza yafuatayo: kuongeza mapato ya ndani kufikia uwiano wa Pato la Taifa wa asilimia 20.9 kwa mwaka 2013/14 ikilinganishwa na asilimia 17.7 kwa mwaka 2012/13; kukamilisha Ripoti za Utafiti wa Mfumo Bora wa Kodi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuandaa na kusimamia utekelezaji wa bajeti ya Serikali; kusimamia utekelezaji wa MKUKUTA-II; kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa watekelezaji wa miradi hiyo; kukamilisha Sera ya Mali ya Umma; kufanya tathmini ya usimamizi na utekelezaji wa malipo ya mishahara ya watumishi wa umma; kusimamia utekelezaji wa mipango kazi ya ukaguzi na uzingatiwaji wa miongozo ya ukaguzi katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, na Mamlaka ya Serikali za Mitaa; kuratibu na kusimamia upatikanaji wa misaada na mikopo nafuu kutoka Nchi Wahisani, Mashirika na Asasi za Fedha za Kimataifa; kuidhinisha miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP); na kukamilisha Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma.

12. Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, Wizara pia ilipanga kukamilisha miradi ya MCA-T na kukabidhi miradi iliyokamilika kwa taasisi husika; kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma Awamu ya nne (PFMRP IV); kufanya uhakiki wa Wastaafu waliopo katika Daftari la Pensheni la Hazina; kuunganisha Hazina Ndogo na Sekretarieti za Mikoa 24 katika mfumo wa malipo kwa njia ya elektroniki kupitia Benki Kuu ya Tanzania (Tanzania Inter- Bank Settlement System - TISS); kuimarisha utendaji kazi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina; na kuandaa na kuhuisha kanuni na miongozo ya utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi.


Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa

13.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, kupitia Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Wizara ya Fedha katika maabara ya utafutaji wa rasilimali fedha iliwekewa malengo yafuatayo: kuongeza mapato mapya ya kodi ya shilingi trilioni 1.16; kuongeza mapato mapya yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 96.7; kudhibiti matumizi; na kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa katika sekta zinazotekeleza miradi hiyo.

14.    Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili 2014, ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vilivyoibuliwa chini ya BRN umefikia shilingi bilioni 338 sawa na asilimia 29.14 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni

1.16.   Matokeo yasiyoridhisha yalisababishwa na baadhi ya mapendekezo ya BRN kutokutekelezwa katika mwaka 2013/14. Mapendekezo hayo ni kubadilisha mfumo wa ushuru wa bidhaa zisizo za petroli kutoka specific kwenda advalorem (makisio shilingi bilioni 386) na kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia tano kwenye bidhaa zinazotoka nje ya nchi (makisio shilingi bilioni 225.6). Kwa vile ukusanyaji wa mapato ndio msingi wa kufanikiwa kwa BRN, Serikali inachambua vyanzo mbadala vya kufidia mapato haya ili kuhakikisha lengo kuu la kuongeza mapato kwa shilingi trilioni 3.48 linafikiwa ifikapo mwaka 2015/16.


Mwenendo wa Uchumi

15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Benki Kuu iliendelea na jukumu la kuandaa, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei kwa ajili ya kuhakikisha gharama za maisha haziongezeki. Kutokana na juhudi hizi, mfumuko wa bei umeshuka kutoka wastani wa asilimia 16 mwaka 2012 hadi kufikia wastani wa asilimia 7.9 mwaka 2013. Katika kipindi hiki uchumi umeendelea kuimarika huku ukuaji halisi wa Pato la Taifa ukiongezeka kwa asilimia 7.0 katika kipindi cha mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 6.9 katika mwaka 2012. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kiasi kikubwa ni pamoja na mawasiliano asilimia 22.8, huduma za kifedha asilimia 12.2, ujenzi asilimia 8.6, na uuzaji bidhaa wa jumla na rejareja asilimia 8.3. Katika mwaka 2014/15, Wizara kupitia Benki Kuu itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha kwamba lengo la msingi la utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi linadumishwa.

Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali

16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara imeratibu uandaaji wa Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa kipindi cha 2014/15 – 2016/17 kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kusambaza kwa wadau mwezi Desemba kama ilivyopangwa. Aidha, Wizara imeandaa na kuchapisha vitabu vya bajeti ya Serikali vya mwaka 2014/15 (Volume I, II, III na IV) kama vilivyowasilishwa Bungeni kwa ajili ya mjadala wa Bunge la Bajeti la mwaka 2014/15 unaoendelea; kitabu cha tafsiri rahisi ya bajeti ya Serikali (Citizen’s Budget) kwa mwaka 2013/14; na Kitabu cha Budget Background and Medium Term Framework  2013/14  2015/16.

17.    Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuanza kutumia mfumo wa Programu katika uandaaji, uidhinishaji na utekelezaji wa Bajeti. Mfumo huu utasaidia Serikali kugawa rasilimali kwa kuzingatia matokeo na kuweka viashiria vya kufikia malengo. Katika hatua za awali za maandalizi ya utekelezaji wa mfumo huu katika mwaka 2013/14, Wizara ilitenga fedha kwa ajili ya mafunzo kwa wataalam wa Wizara nane za mfano. Maandalizi haya ya kimkakati na kimfumo yataendelea katika mwaka 2014/15. Wizara zilizotengwa kwa majaribio na ambazo tayari zimefanyiwa mafunzo ni Wizara ya Maji, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Wizara ya Fedha. Wizara hizi kwa sasa zinaendelea na zoezi la kuandaa programu na viashiria vya kupima utekelezaji kabla ya mfumo kuanza kutumika.

18.    Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu kikao kazi cha wataalamu wa wizara, mikoa na halmashauri kuhusu mfumo wa ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Bajeti. Katika kipindi hicho, Wizara pia ilifanya kikao kazi kilichohusisha washiriki kutoka wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, mikoa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa lengo la kutathmini uandaaji na uwasilishwaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/13 na kufanya mkutano wa mwaka wa wadau ambao ulijumuisha Washirika wa Maendeleo kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa Bajeti ya Serikali.

19.    Mheshimiwa Spika, katika kusimamia na kudhibiti utekelezaji wa bajeti ya Serikali ikiwemo kufuatilia matumizi ya fedha za umma, Wizara ilifanya ufuatiliaji na ukaguzi wa matumizi ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya maendeleo kwa miradi ya ASDP na DASIP ikihusisha wizara nne, mikoa sita na halmashauri 33. Aidha, ufuatiliaji na ukaguzi ulifanyika kwa mapato na matumizi ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) na kwa fedha zilizotolewa kuhudumia vituo 16 vya Makazi ya Wazee katika mikoa 14 nchini.

20.    Mheshimiwa Spika, katika ukaguzi huo, Wizara ilibaini kuwapo kwa upungufu na changamoto katika maeneo haya ikiwa ni pamoja na: fedha kutowafikia walengwa kwa wakati kama ilivyopangwa; udhaifu kwenye udhibiti wa ndani wa matumizi na hivyo kusababisha kuwapo kwa huduma duni; na miradi kutokamilika kwa wakati na kuwepo kwa bakaa ya fedha za maendeleo. Aidha, zimekuwepo changamoto za kubadilika mara kwa mara bei ya kununulia nafaka na gharama za usafirishaji, hivyo kuathiri malengo yaliyopangwa ikiwemo kusababisha madeni. Wizara imewasiliana na wahusika na kutoa nyaraka za maelekezo ya kuhakikisha kwamba udhibiti wa ndani wa matumizi unaimarishwa katika ngazi zote za usimamizi na inapobidi hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.

21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara inatarajia kutekeleza yafuatayo: kupitia mfumo wa uwasilishaji wa bajeti za wizara, idara za Serikali, mikoa na halmashauri na kuhakikisha kuwa sera na mipango ya kitaifa na ile ya kisekta vyote vimezingatiwa ipasavyo katika Bajeti ya Serikali na kutengewa fedha; kufanya tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, kuendelea kuboresha mfumo wa mpangilio wa Bajeti ya Serikali kwa kuzingatia programu mbalimbali; kuimarisha mifumo ya kompyuta ya uandaaji bajeti ili kukidhi mahitaji ya taarifa mbalimbali zinazohitajika; kuendelea kujenga uwezo wa wizara, idara za Serikali, mikoa na halmashauri katika uandaaji wa Bajeti ya Muda wa Kati, usimamiaji wake na utoaji taarifa za utekelezaji ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji na tathmini kwa wakati; kutayarisha taarifa mbalimbali za utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji unazingatiwa; na kufuatilia matumizi ya fedha za umma zikiwemo fedha za mishahara, matumizi mengineyo na fedha za miradi.

Usimamizi wa Misaada na Mikopo

22. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara ilifanikisha kusainiwa kwa mikataba 18 kwa ajili ya misaada na mikopo nafuu yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 958.027 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu ukamilishaji wa Mwongozo mpya wa Ushirikiano wa Maendeleo - Development Cooperation Framework ambao utachukua nafasi ya Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA). Mwongozo huu una lengo la kusimamia ushirikiano wa maendeleo baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa MPAMITA. Lengo la ujumla ni kupatikana ufanisi katika misaada kutoka kwa Washirika wa maendeleo na kubainisha wajibu wa kila mdau wa maendeleo wakiwemo raia, wabunge, asasi zisizo za kiserikali na sekta ya habari.

23. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kuzindua Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo na kuandaa mpango kazi wake pamoja na kuhamasisha matumizi yake kwa Washirika wa Maendeleo, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Serikali za Mitaa, Taasisi Binafsi na Waheshimiwa Wabunge; kutathmini utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha toka Washirika wa Maendeleo kwa nia ya kuhakikisha kwamba thamani ya fedha inapatikana katika miradi hiyo; kushiriki kwenye majadiliano na Jumuiya za kikanda na kimataifa; na kuendelea kutafuta fedha za misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na Misaada ya Kiufundi kutoka kwa Mashirika ya Kimataifa na nchi wahisani.


Ulipaji wa Deni la Taifa

24.    Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeendelea kusimamiwa na Sheria ya Madeni ya mwaka 1974 na marekebisho yake ya mwaka 2004. Wizara imeendelea kutoa kipaumbele katika ulipaji wa madeni kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya riba. Katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014 malipo ya deni la ndani yalifikia shilingi bilioni 1,694.53 ambapo kati ya malipo hayo riba ni shilingi bilioni 581.20 na Mtaji (principal rollover) ni shilingi bilioni 1,113.33. Aidha, deni la nje limelipwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 340.22, kati ya kiasi hicho malipo ya riba ni shilingi bilioni 201.52 na deni halisi - principal ni shilingi bilioni 138.70.

25.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kulipa madeni ya ndani na nje kwa wakati ikiwa ni pamoja na kulipa kwa wakati madeni mbalimbali ambayo serikali imeingia mikataba (Contractual Liabilities) na madai ya dharura (Contingent Liabilities) pindi yanapotokea.

Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma

26. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kujenga uwezo wa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma kwa kudhamini mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 313 wa kada ya uhasibu, ugavi na kompyuta kutoka kwenye wizara, idara za serikali, sekretariati za mikoa, manispaa, halmashauri za miji na wilaya waliopo vyuoni na watumishi 218 walipewa mafunzo ya muda mfupi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma. Aidha, Wizara imeendelea kusambaza Mfumo wa Malipo wa Kielektroniki -TISS mikoani ambapo hadi sasa jumla ya mikoa 20 imeunganishwa katika mtandao huo. Mikoa iliyounganishwa kwenye mtandao huo ni Iringa, Morogoro, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Lindi, Simiyu, Mwanza, Kagera, Geita, Mara, Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Njombe, Dar es Salaam na Katavi. Vile vile, mikoa mipya ya Geita, Simiyu, Katavi na Njombe imeunganishwa kwenye mtandao wa malipo wa Serikali (Intergrated Financial Management System).

27.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na mpango wa kutekeleza mfumo wa uandaaji wa taarifa za hesabu kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Hesabu katika Sekta ya Umma - IPSAS Accrual Basis ambapo hesabu za majumuisho za mwaka 2012/13 zimeandaliwa kwa kutumia mfumo huo kwa mara ya kwanza na kuwasilishwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa wakati.

28.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, pamoja na mambo mengine, Wizara itaendelea kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kufanya yafuatayo: kuendelea kutoa udhamini wa masomo ya muda mrefu na mfupi kwa wahasibu, wakaguzi, maafisa ugavi na wataalamu wa kompyuta kutoka Serikali Kuu na serikali za mitaa; kuweka mitambo katika hazina ndogo zote ili kuwezesha sekretariati za mikoa na hazina ndogo kufanya malipo kwa kutumia mifumo ya malipo ya kielektroniki   -TISS/EFT; kuendelea kutoa mafunzo ya TISS/EFT kwa wahasibu na watumishi wa kada zingine ili kuimarisha mfumo wa malipo; na kuanza ujenzi wa jengo la ofisi ya Hazina Ndogo Arusha.

29. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15 ili kuinua kiwango cha fani ya uhasibu sambamba na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa Wahasibu Wakuu wa Serikali wa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika – ESAAG.


Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma – Public Finance Management Reform Programme (PFMRP)

30. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma imekamilisha utafiti wa mfumo wa kupeleka fedha kwenye Serikali za Mitaa, mpango wa utekelezaji wa utafiti huo umeandaliwa na utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2014/15. Aidha, utafiti juu ya mifumo ya fedha inayotumiwa na Serikali kwa lengo la kuiunganisha mifumo hiyo ili kuboresha usimamizi wake umekamilika. Vile vile, Wahasibu 522 kutoka Wizara mbalimbali, hazina ndogo na sekretarieti za mikoa walipata mafunzo juu ya Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Hesabu katika Sekta ya Umma na watumishi wengine 34 ambao wanasimamia programu hii kutoka katika wizara na taasisi walipata mafunzo ya kusimamia Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change Management and Strategic Planning. Mafunzo haya yalilenga kuwajengea uwezo wa kuandaa mipango na bajeti inayolenga katika kutekeleza maboresho ya usimamizi wa fedha za umma.

31. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kuendelea na utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Programu ya PFMRP kwa kufanya yafuatayo: kupitia na kuboresha mifumo ya kifedha na kuangalia njia bora ya kuiunganisha baada ya utafiti kukamilika; na kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani katika wizara, idara, wakala za Serikali na halmashauri za Serikali za Mitaa juu ya ukaguzi wa mifumo ya fedha, usimamizi na ukaguzi wa vihatarishi, ukaguzi wa bajeti na mishahara, na ukaguzi wa miradi.

Sera ya Ununuzi wa Umma

32. Mheshimiwa Spika, katika kusimamia Sekta ya Ununuzi wa Umma nchini, Wizara imeendelea kutekeleza yafuatayo: kuandaa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma; kuandaa mapendekezo ya muundo wa Vitengo vya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi Serikalini; na kufanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi walioko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; na kuendelea kuhuisha taarifa za maafisa ununuzi na ugavi Serikalini, ambapo taarifa za maafisa 332 katika mikoa ya Shinyanga, Kagera, Mwanza na Mara zimehakikiwa na kuingizwa katika daftari la maafisa ununuzi na ugavi.



33. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kuandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Ununuzi wa Umma na kusimamia utekelezaji wa Sera hiyo; kuhuisha muundo wa vitengo vya usimamizi wa ununuzi na ugavi serikalini; kuipitia Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.7 ya mwaka 2011 na kanuni zake za mwaka 2013; kukamilisha tathmini ya mahitaji ya mafunzo kwa maafisa ununuzi na ugavi Serikalini; na kufanya tathmini juu ya ufanisi wa ununuzi wa umma nchini.

Udhibiti wa Ununuzi wa Umma

34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma imetoa mafunzo kuhusu sheria, kanuni na taratibu za ununuzi kwa taasisi za umma 32 ambapo watumishi 747 walihudhuria mafunzo hayo. Aidha, Mamlaka ilitoa mafunzo kuhusu mfumo wa upokeaji na usimamizi wa taarifa za ununuzi nchini katika vituo vinne vya Morogoro, Arusha, Mwanza na Mbeya ambapo jumla ya washiriki 330 kutoka taasisi 191 walishiriki. Vile vile, Mamlaka imeendelea kusimamia mfumo wa upokeaji na usimamizi wa taarifa za ununuzi nchini ambapo katika kipindi hicho, taasisi 191 ziliunganishwa na kupatiwa mafunzo ya kutumia mfumo huo na hivyo kufanya jumla ya taasisi zilizounganishwa na kupatiwa mafunzo kufikia 364, sawa na asilimia 80 ya taasisi zote.

35.    Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma imefanya ukaguzi kuhusu utoaji wa zabuni na utekelezaji wa mikataba itokanayo na ununuzi wa umma katika Taasisi 120 zikiwemo wizara na idara zinazojitegemea 32, mashirika ya umma 46 na serikali za mitaa 42. Ukaguzi huu uilihusisha mikataba 5,867 yenye thamani ya shilingi bilioni 1,985.427 ikiwemo miradi 207 ya ujenzi yenye thamani ya shilingi bilioni 777.2. Ripoti ya ukaguzi inaonesha wastani wa uzingatiwaji wa sheria ya ununuzi ulikuwa ni asilimia 64 ambayo ni chini ya lengo la asilimia 80. Maeneo yaliyobainika kuwa na udhaifu mkubwa ni katika usimamizi wa mikataba na utunzaji wa nyaraka za ununuzi.

36.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: kuandaa mpango kazi wa usimamizi wa utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2011; kuelimisha wadau mbalimbali kuhusu Sheria mpya na kanuni zake; kuendelea na maandalizi ya kuanzisha mfumo wa ununuzi kwa njia ya kielektronic (e-procurement system); kufungua ofisi za kanda Dodoma, Mbeya na Mwanza; kushirikiana na TAMISEMI ili kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye vitengo vya ununuzi vya halmashauri mbalimbali; kufanya kazi na Asasi za Kiraia na Wanahabari ili kuongeza uelewa wa masuala ya Ununuzi wa Umma kwa wananchi; na kuendelea kusimamia ununuzi katika sekta ya Umma.


Huduma ya Ununuzi Serikalini

37.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini imetekeleza yafuatayo: kuongeza vifaa vya huduma mtambuka kutoka 86 vilivyokuwepo hadi 181; kuendelea na ujenzi wa Ofisi na ghala katika mkoa wa Manyara; kuendelea na ujenzi wa kituo cha mafuta mkoa wa Dodoma; na kununua magari mawili makubwa yenye uwezo wa kubeba lita 45,000 za mafuta kila moja kwa ajili ya kusafirisha mafuta toka kwa wazabuni kwenda mikoani. Aidha, Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini, imeanza kufunga Mfumo wa Udhibiti na Usimamizi wa Mafuta ya Magari ambao utaanza kwa majaribio Agosti, 2014 katika mkoa wa Dar es Salaam ili kudhibiti matumizi ya mafuta katika magari ya Serikali.

38.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara kupitia Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini imepanga kutekeleza yafuatayo: kukamilisha kazi ya kufunga Mfumo wa Udhibiti na Usimamizi wa Mafuta ya Magari katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma, Iringa na Mbeya; kuanza kazi za Ujenzi wa Ofisi katika mikoa ya Njombe na Mara; kukamilisha ujenzi wa visima vya mafuta katika mikoa ya Geita, Katavi na Wilaya ya Ileje; na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mafuta kufikia wastani wa lita 50,000 katika vituo vya mikoa ya Arusha, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Lindi, Tabora, Pwani, Tanga na Ruvuma. Aidha, Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini itahuisha muundo wake ili kuweza kutoa huduma ngazi ya wilaya na kuanza kutekeleza utaratibu wa ununuzi wa magari kwa pamoja.

Rufaa za Zabuni za Umma

39. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma imepokea jumla ya mashauri 35, kati ya hayo mashauri matatu yaliondolewa na walalamikaji kabla ya kusikilizwa; mashauri 17 walalamikaji walishinda; mashauri 11 walalamikaji walishindwa; mashauri mawili yalifutwa kufuatana na sheria; shauri moja halikutolewa uamuzi kutokana na ukomo wa muda wa kulisikiliza; na shauri moja lipo kwenye hatua ya kusikilizwa. Aidha, katika mwaka 2014/15, Mamlaka itaendelea kusikiliza na kutolea maamuzi malalamiko na rufaa katika Ununuzi wa Umma na kuelimisha umma na wadau juu ya kuwasilisha pingamizi za zabuni kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011.

Usimamizi wa Mali ya Serikali

40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara iliendelea kuandaa Sera ya Mali ya Umma. Lengo la sera hii ni kusimamia na kutoa miongozo ya udhibiti wa mali ya umma. Aidha, Wizara ilifanya uthamini wa mali ya Serikali katika mikoa mitano na wizara mbili, hivyo kufanya wizara, idara zinazojitegemea na wakala wa Serikali zilizofanyiwa uthamini kufikia 42. Katika kipindi hicho, usimikaji wa mfumo wa uhakiki wa mali ya umma ulikamilika. Vile vile, Wizara iliendelea na zoezi la kuondosha mali chakavu katika wizara na idara za Serikali ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.58 zilikusanywa kutokana na mauzo ya vifaa hivyo na shilingi milioni 12.83 kutokana na utoaji wa leseni za udalali.

41.    Mheshimiwa Spika, Wizara ilifanya uhakiki wa mali ya Serikali katika wizara, idara zinazojitegemea na wakala za Serikali kwa lengo la kudhibiti matumizi ya mali katika taasisi hizo. Aidha, Wizara imefanya uhakiki maalum katika Bohari Kuu ya Madawa ambapo ushauri ulitolewa wa namna ya kupunguza hasara inayotokana na madawa, vifaa tiba na vitendanishi kuisha muda wake wa matumizi kabla ya kutumika.

42.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka, 2014/15, Wizara imepanga kukamilisha Sera ya Mali ya Umma na kuisambaza kwa wadau kwa ajili ya kupata maoni kabla ya kuanza utekelezaji wake. Aidha, Wizara imepanga kufanya uthamini wa mali katika mikoa saba na taarifa zake kuingizwa kwenye Daftari la Mali ya Serikali. Vile vile, Wizara itaendelea kuondosha mali chakavu, mali zilizokwisha muda wake na vifaa sinzia kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Fedha za Umma; kushughulikia taarifa za ajali na potevu za mali ya Serikali; na kuendelea kuchambua, kufanya majadiliano na wadai na kulipa madai ya fidia na kifuta machozi yanayotokana na amri ya Mahakama. Kadhalika, Wizara itaendelea na uhakiki wa mali katika wizara, idara zinazojitegememea na wakala za Serikali.

Mpango wa Millenium Challenge Account  Tanzania (MCA-T)

43. Mheshimiwa Spika, Programu ya Millenium Challenge Account Tanzania iliendelea na ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, nishati ya umeme na maji. Miradi yote ya barabara imekamilika isipokuwa sehemu ya Laela- Sumbawanga katika barabara ya Tunduma- Sumbwanga ambayo inatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2014. Miradi ya umeme na maji imekamilika na ipo katika kipindi cha uangalizi. Aidha, kutokana na utekelezaji wa kuridhisha, Tanzania imekidhi vigezo na hivyo itanufaika na awamu ya pili ya msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC). Katika awamu ya pili, miradi itakayofadhiliwa ni ya umeme na barabara za vijijini Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Ukaguzi wa Ndani

44. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara imetekeleza yafuatayo: kutoa Mwongozo wa Kamati za Ukaguzi katika Sekta ya Umma kwa lengo la kuhakikisha utendaji wenye tija kwa Kamati zote za Ukaguzi; kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani 458, wajumbe wa Kamati za Ukaguzi na wadau wa ukaguzi wa ndani wapatao 567; kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo 11; ukaguzi wa orodha ya malipo ya mishahara; na kuhakiki madai mbalimbali yaliyowasilishwa wizarani kabla ya kulipwa.


45.    Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza juhudi za Serikali za kudhibiti ubora wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Wizara imenunua vifaa vya kuhakiki ubora wa miundombinu. Vifaa hivyo vitatumika katika ukaguzi wa miradi inayotekelezwa na Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Halmashauri za Serikali za Mitaa katika kuhakikisha kuwa miradi na miundombinu inayotekelezwa inakuwa na ubora unaokidhi viwango na hatimaye kupata thamani ya fedha. Hatua hii itaenda sambamba na kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani Serikalini katika kufanya ukaguzi wa kiufundi kwa miradi inayotekelezwa katika taasisi zao.

46.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kusimamia kada ya ukaguzi wa ndani na kamati za ukaguzi; kufanya ukaguzi wa Mfumo wa ulipaji Mishahara Serikalini; kuhakiki madai mbalimbali ya Serikali kabla ya kuyalipa; na kufuatilia utekelezaji wa miongozo mbalimbali iliyotolewa. Aidha, Wizara inatarajia kutoa miongozo ifuatayo: Mwongozo wa Usimamizi wa Viashiria Vya Udanganyifu; Mwongozo wa Udhibiti wa Ndani; Mwongozo wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Usimamizi wa Vihatarishi; Mwongozo wa Ukaguzi wa Ununuzi; na Mwongozo wa Ukaguzi wa Mikataba. Vile vile, wizara kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali itaendelea kuimarisha ofisi za Mkaguzi Mkuu wa ndani kwa lengo la kusimamia matumizi ya fedha.
  
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali

 47.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imetekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria. Ofisi imeendelea kuwa mshirika katika Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa katika kukagua taasisi za Umoja wa Mataifa. Aidha, Ofisi imeendesha mafunzo kwa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali na Kamati ya Bajeti kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kuimarisha uwajibikaji na utawala bora. Vile vile, ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu unaendelea.

 
48.    Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuondoa wakaguzi katika majengo ya wakaguliwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imekodi majengo ya ofisi katika mikoa ya Mwanza, Tabora, Tanga, Iringa, Kagera na Geita. Aidha, ujenzi wa ofisi katika mkoa wa Dodoma unaendelea ukiwa katika hatua za mwisho. Vile vile, Ofisi imeendelea na uunganishaji wa ofisi zake zilizoko mikoani na makao makuu kwa njia ya mtandao mpana. Kwa mwaka huu ofisi 4 zimeunganishwa na hivyo kufanya ofisi zilizounganishwa kufikia 14.

49.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014/15, Ofisi inatarajia kufanya yafuatayo: kukagua mafungu yote 49 ya Wizara na Idara za serikali, hesabu za Mikoa yote 25 ya Tanzania Bara, Hesabu za Halmashauri zote 161 za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, Mashirika ya Umma 177, Balozi zote 32 zilizoko nje ya nchi na Wakala 33 za Serikali pamoja na kufanya ukaguzi wa thamani ya fedha katika maeneo sita; kuendelea na ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vyote vya siasa; kuanza ukaguzi katika sekta ya gesi na mafuta pamoja na ukaguzi wa miradi mikubwa inayoendeshwa kwa ubia wa sekta ya Umma na Sekta binafsi; kuendelea kushiriki kikamilifu katika jukumu la kukagua taasisi za Umoja wa Mataifa sanjari na wanachama wengine wanaounda Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.
  
50. Mheshimiwa Spika, mambo mengine yatakayotekelezwa katika mwaka 2014/15, ni pamoja na: kuendelea na zoezi la kuwaondoa wakaguzi katika maeneo ya wakaguliwa katika wizara zote na katika mikoa 6 iliyobaki; kuendelea kuzijengea uwezo kwa njia ya mafunzo Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali na Kamati ya Bajeti katika maeneo ya kuelewa kwa undani taarifa za ukaguzi wa hesabu zinazoandaliwa na wakaguliwa; kukamilisha ujenzi wa ofisi katika mkoa wa Rukwa pamoja na kuanza ujenzi wa ofisi katika mikoa ya Mara na Iringa; na kutoa mafunzo kwa watumishi ili kuimarisha uwezo wao katika kutumia mfumo wa TeamMate ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika ukaguzi wa kisasa.

 Uratibu wa Utekelezaji wa MKUKUTA

51. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa MKUKUTA II kwa kufanya ufuatiliaji, tafiti, na tathmini na kuandaa taarifa ya utekelezaji na hali ya Umaskini nchini ili kuwezesha maamuzi ya kisera, kibajeti na kiutekelezaji. Kazi ya uandaaji wa Taarifa ya Mwaka ya Utekelezaji wa MKUKUTA II imekamilika na kuwekwa katika tovuti ya Wizara. Aidha, Wizara inaendelea kukamilisha Taarifa ya Maendeleo ya Malengo ya Milenia. Taarifa ya awali inaonesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara ni asilimia 28.2 ambapo kwa Dar es Salaam ni asilimia 4.2, maeneo mengine ya mjini ni asilimia 21.7 na maeneo ya vijijini ni asilimia 33.3. Umaskini wa chakula ni asilimia 9.7 ambapo kwa Dar es Salaam ni asilimia 1.0, maeneo mengine ya mjini ni asilimia 8.7 na maeneo ya vijijini ni asilimia 11.3.

52. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: kukusanya na kuchambua taarifa mbalimbali kutoka katika Wizara, Idara na Wakala za Serikali ili kuandaa Taarifa ya mwaka ya Utekelezaji wa MKUKUTA II; kuandaa taarifa ya mwisho ya kutathimini utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia; kufanya mapitio ya MKUKUTA II; kukamilisha Mpango wa Utekelezaji wa Kinga ya Jamii pamoja na kuainisha viashiria vya upimaji juhudi za kinga ya jamii; na kuratibu mkutano wa kitaifa wa kujadili sera za kupambana na Umaskini nchini. Pia Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaandaa mapendekezo ya hatua zitakazofuata baada MKUKUTA II kufikia kikomo mwezi Juni, 2015.

 
53. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mradi wa SELF II imeendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali ambapo hadi kufikia Aprili 2014, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 8.6 ilikopeshwa kwa wajasiriamali 4,943 kupitia Asasi ndogo 103. Kati ya waliokopeshwa, wanawake ni 2,040 sawa na asilimia 41 na wanaume ni 2,903 sawa na asilimia 59. Kwa wastani, urejeshwaji wa Mikopo ya Mradi wa SELF umeendelea kuwa wa ufanisi

No comments:

Post a Comment